Cerca

Vatican News
Huruma na upendo wa Mungu vinamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Huruma na upendo wa Mungu vinamwilishwa katika uhalisia ya maisha ya watu  (Vatican Media)

Mafundisho makuu ya Papa Francisko: Huruma, upendo na haki jamii!

Nyaraka kuu tatu za Papa Francisko, kimsingi ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika mshikamano wa huruma, upendo na haki jamii; katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Furaha ya injili kwa watu wa mataifa pamoja na kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amelizawadia Kanisa Nyaraka kuu tatu ambazo kimsingi ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika mshikamano wa huruma, upendo na haki jamii; katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Furaha ya injili kwa watu wa mataifa pamoja na kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Kwa ufupi huu ndio muhtasari wa mafundisho makuu yaliyomo kwenye Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Misericordia et misera” “Huruma na amani” “Evangelium gaudium” “Furaha ya Injili” pamoja na “Amoris laetitia” “Furaha katika upendo ndani ya familia”. Hii ni changamoto ambayo iliibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ikavaliwa njuga na Mwenyeheri Paulo VI na kumwilishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyewataka walimwengu kujenga na kushuhudia utamaduni wa upendo.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushuhudia: Furaha ya Injili inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Hivi ndivyo Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia anavyopembua kwa kina na mapana Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” mintarafu mwelekeo wa huruma ya Mungu katika maisha ya kijamii.

Utamaduni wa upendo ni maneno yaliyotumiwa kwa mara ya kwanza na Mwenyeheri Paulo VI, wakati wa mahubiri yake kwenye Sherehe ya Noeli ya Mwaka 1975 sanjari na kufunga Mwaka wa Jubilei kwa kuwataka waamini kumwilisha utamaduni wa upendo ili kuyachachua na kuyageuza malimwengu ili yaweze kuwa na chapa ya upendo wa Kikristo, ili hatimaye, kuondokana na uchoyo, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yamekuwa ni chanzo cha vita, kinzani na migogoro sehemu mbali mbali za dunia.

Ujenzi wa utamaduni wa upendo unajikita katika haki na amani kama tunu msingi zinazotegemeana na kukamilishana katika maisha ya kijamii na kama sehemu ya ujumbe wa Injili unaopaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kumwilishwa katika maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Wokovu wa Kristo unamwambata mtu mzima: kiroho na kimwili, ndiyo maana Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kitume “Dives in misericordia” yaani “Tajiri wa huruma” anakazia mambo makuu matatu: upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu; huduma makini kwa maskini, wadhambi na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya haki inayofikia utimilifu wake katika msamaha kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu una nguvu zaidi kushinda dhambi na ubaya unaoendelea kumwandama mwanadamu katika historia na maisha yake.

Changamoto hii anasema Kardinali Bassetti, inamwilishwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume: huruma na upendo, lengo ni kujenga utamaduni wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Utamaduni wa huruma unafumbatwa katika ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, kufahamiana na kusaidiana katika maisha. Ni utamaduni unaofumbatwa katika maisha ya sala kwa kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza vyema na hatimaye, kumwilisha sala hii katika matendo, kielelezo cha imani tendaji!

Utamaduni wa huruma ya Mungu unajengwa kwa maisha na shuhuda za watakatifu wa Mungu pamoja na kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Maskini anasema Baba Mtakatifu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu! Utamaduni huu unasimikwa katika upendo, toba na wongofu wa ndani, pale dhambi inapoweka na huruma kubaki na kumwandama mwanadamu kama ilivyotokea kwa yule mwanamke mzinzi aliyeponea chupuchupu kutwanga kwa mawe hadi kufa, lakini akakutana na Uso wa huruma ya Mungu, dhambi ikatoweka, akabaki mtu mpya akitembea katika mwanga wa huruma na upendo wa Mungu.

Kardinali Basetti anendelea kufafanua kwamba, Uinjilishaji mpya unajikita katika ushuhuda wenye mguso na mashiko; toba na wongofu wa ndani, ili kweli waamini waweze kutambua uwepo wa dhambi katika maisha yao, tayari kutubu na kumwongokea Mungu. Ikumbukwe kwamba, dhambi ina madhara yake si tu katika maisha ya kiroho, bali hata katika maisha ya kijamii, ndiyo maana huruma ya Mungu inapata pia mwelekeo wa kijamii kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Upendo ni sumaku inayomuunganisha Mungu na binadamu, changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Leo hii, maskini wanaonekana kuwa kero kwa Jumuiya ya Kimataifa, watu wasiokuwa na utu wanaochezewa kama “mpira wa danadana” na kukandamizwa chini kama “soli ya kiatu”! Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi, ameamua kuanzisha Siku ya Maskini Duniani, itakayoadhimishwa na Mama Kanisa kuanzia sasa kila Jumapili ya XXXIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kabla ya maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu inayofunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa.

Kardinali Bassetti anakaza kusema, Siku ya Maskini Duniani inapaswa kuwa ni siku ya kutafakari jinsi ya kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, kwa kujenga na kudumisha matendo ya huruma: kiroho na  kimwili. Huu utakuwa ni mwendelezo sahihi wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha neema na baraka. Ni wakati wa kufungua akili na nyoyo za watu ili kuangalia ni kwa jinsi gani huruma ya Mungu inaweza kumwilishwa katika matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji na ushuhda wenye mvuto na mashiko wa Uinjilishaji mpya. Upendo unaongoza, sheria inatekeleza!

Mafundisho makuu ya Papa Francisko

 

 

25 July 2018, 09:16