Tafuta

Vatican News
Baraza la Kiapapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu limechapisha kitabu kufafanua mchakato huo. Baraza la Kiapapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu limechapisha kitabu kufafanua mchakato huo.  (Vatican Media)

Mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu

Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu katika chapisho la hivi karibuni linaonesha kwamba, hii ni dhamana nyeti inayotekelezwa na Mama Kanisa kwa uangalifu mkubwa katika utambuaji wa matukio kuwa ni muujiza kwa maombezi ya watumishi wa Mungu au wenyeheri. Ni kweli bado kuna mijujiza duniani!

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, hivi karibuni limetoa chapisho la nne la Prospero Lambertini, kwa heshima ya Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa miaka kumi sasa, na ambaye mnamo tarehe 8 Juni 2018 katimiza miaka 80 ya kuzaliwa. Prospero Lambertini ambaye baadae alikuwa Baba Mtakatifu, tangu 1740 – 1758, na kubeba jina la Benedikto XIV, aliandika sana juu ya mchakato wa kutangaza waamini wenyeheri ama watakatifu ndani ya Kanisa.

Chapisho lililotolewa sasa limeitwa De servorum Dei beatificatione et beatorum canonizatione, yaani Watumishi wa Mungu kutangazwa wenyeheri na wenyeheri kutangazwa watakatifu. Sehemu ya kwanza ya chapisho hilo la Prospero Lambertini lililotafsiriwa kwa lugha ya kiitalia, imejikita zaidi katika masuala ya miujiza. Lambertini, na baadae Papa Benedikto XIV aliamini kwamba Kanisa, na kwa namna ya pekee Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu linafanya kwa uangalifu na umakini mkubwa utambuaji wa matukio kuwa ni miujiza inayotokea kwa maombezi ya watumishi wa Mungu ama wenyeheri.

Pili, chapisho linaonesha umuhimu wa nafasi ya madaktari na watendaji wataalamu wa afya kuthibitisha miujiza hiyo, hasa kuhusu ukubwa wa ugonjwa na uponyaji wake kimuujiza. Mwishoni chapisho linazungumzia uponyaji wa kipekee kabisa wa viwete na wasioweza kutembea. Sehemu hii inasimulia pia mfano wa mtoto wa miaka mine ambaye tangu kuzaliwa hakuwahi kutembea mbali ya juhudi ya tiba zilizofanyika. Kisha akiwa na umri wa miaka mine alipelekwa kwenye nyumba ya kitawa aliyokuwa akiishi Mt. Theresa wa Avila. Siku ya mwisho ya Novena mtoto huyo alipona na akaanza kutembea.

Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu limetoa chapisho hili kwa heshima ya Kardinali Angelo Amato, kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa mwanataalimungu ndani ya Kanisa, na kwa namna ya pekee akiwa Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa miaka kumi sasa. Katika kipindi hicho, wametangazwa watakatifu 100, na wenyeheri 1233, kati yao ni pamoja na Yohane Paulo II, Yohane XXIII, Mama Theresa wa Calcutta, watoto Francisko na Yasinta waliotokewa na Bikira Maria kule Fatma, Ureno, na tarehe 14 Oktoba 2018, watatangazwa watakatifu Paolo VI na Oscar Romero.

Kardinali Angelo Amato alizaliwa Molfetta, Italia mnamo tarehe 8 Juni 1938, akajiunga na Shirika la Wasalesiani la Don Bosco, akajifunza falsafa katika chuo cha Mt. Gregory huko Catania, baadae akahamishiwa Roma kwa ajili ya shahada ya uhimili kwenye masomo ya falsafa na taalimungu katika chuo kikuu cha Salesiana. Alipata Daraja Takatifu ya Upadre mnamo tarehe 22 Disemba 1967. Baada ya shahada ya Uzamili katika taalimungu kutoka chuo kikuu cha Gregoriana, alitumwa Athen Ugiriki kujifunza tasaufi ya Umoja wa wakristo. Baada ya majiundo hayo alirudi Roma na kuwa mkufunzi katika chuo kikuu cha Salesiana.

Tarehe 19 Disemba 2002, Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafunzo Tanzu ya Kanisa, kwa zaidi ya miaka 20 alifanya utume huo chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza Kardinali Joseph Ratzinger. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu mnamo tarehe 6 Januari 2003, na tarehe 2 Julai 2008, Papa Mstaafu Benedikto XVI alimteua kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Sasa ameng’atuka kutoka madarakani kutokana na umri baada ya kulitumikia Kanisa kwa weledi na sadaka kubwa katika maisha yake!

Sikiliza

 

19 July 2018, 09:03