Tafuta

Vatican News
Papa Francisko wakati wa Sala ya Kiekumene kuombea haki na amani Mashariki ya Kati. Papa Francisko wakati wa Sala ya Kiekumene kuombea haki na amani Mashariki ya Kati.  (Vatican Media)

Kanisa linafuatilia kwa makini hatima ya Wakristo Mashariki ya Kati!

Mashariki ya Kati ni Ukanda ambao kwa sasa umegeukwa kuwa ni uwanja wa vita, mateso na mahangaiko matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kanisa litaendelea kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu huko Mashariki ya Kati kama alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Makanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anaendelea kuonesha jicho la pekee kutokana na fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kuwakumba watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, Ukanda ambao kwa sasa umegeukwa kuwa ni uwanja wa vita, mateso na mahangaiko matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kanisa litaendelea kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu huko Mashariki ya Kati kama alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko, viongozi wa Makanisa pamoja na wakuu wa Jumuiya za Kikristo huko Mashariki ya Kati, hapo tarehe 7 Julai 2018 mjini Bari, Kusini mwa Italia.

Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Leonardo Sandri, wakati wa safari yake ya kikazi nchini Marekani, kwa mwaliko wa Kanisa la Wamaroniti wa Marekani, ili kushiriki mkutano wa wakleri, watawa na waamini walei kutoka Lebanon. Jumuiya hii imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamia; kwa kuimarisha utume wa vijana na watoto, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na hali zao za maisha. Utume wa familia; umuhimu wa kusimama kidete: kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; malezi na majiundo ya awali na endelevu kwa wakleri na watawa ni kati ya mambo zilizopembuliwa kwa kina wakati wa mkutano huo.

Kardinali Leonardo Sandri amewataka waamini kukuza na kudumisha imani, matumaini na mapendo kwa kujikita katika Neno la Mungu, Liturujia na Mapokeo ya Kanisa; ili hatimaye, kuwawezesha waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kanisa la Kristo ambalo kwa asili ni la kimisionari, kwani linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu anapenda kuona yakifanyiwa kazi huko Mashariki ya Kati.

Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa na jicho la pekee sana kwa shida, mahangaiko na matumaini ya watu wa Mungu walioko Mashariki ya Kati. Anataka kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika uekumene wa ushuhuda wa damu, maisha ya kiroho na sala, lakini zaidi, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Huu ni umoja wa Kanisa unaofumbatwa katika tofauti, lakini unafungamanishwa na imani moja kwa Kristo na Kanisa lake.

Uwepo wa Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kutambua kwamba, kutokana na vita na machafuko ya kisiasa nchini Siria, Serikali nyingi zilifunga balozi zake, lakini, Kardinali Sandri yupo kati pamoja na wananchi wa Siria, kielelezo cha mshikamano na ushuhuda wa uekumene wa dam una wananchi hao! Kanisa linaendelea pia kujikuta katika mchakato wa majadiliano ya kidini na hapa kwa namna ya pekee kabisa, amekumbukwa Kardinali Jean Louis Tauran, aliyefariki hivi karibuni, kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza na kudumisha: haki na uhuru wa kuabudu; utu na heshima ya binadamu.

Kanisa linapenda kuonesha umoja na mshikamano unaofumbatwa katika Injili ya huruma na mapendo kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi wanaohudumiwa huko Lebanon na Yordan nchi ambazo kwa hakika zimekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Kardinali Sandri anakaza kusema, licha ya matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza siku kwa siku, lakini waamini wanapaswa kusimama kidete: kulinda, kutangaza na kutetea imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watambue kwamba, wanayo dhamana na utume maalum ndani ya Kanisa Katoliki.

Akiwa nchini Marekani, Kardinali Leonardo Sandri amekutana pia na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani pamoja na viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo bila kuwasahau wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Marekani wanaoendelea kutoa ushuhuda wa pekee katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum huko Mashariki ya Kati.

Sikiliza mwenyewe kwa raha zako!

 

30 July 2018, 15:19