Tafuta

Vatican News
Wakimbizi na wahamiaji wakiokolewa nchini Hispania. Wakimbizi na wahamiaji wakiokolewa nchini Hispania.  (AFP or licensors)

Jengeni mshikamano wa upendo na wahamiaji pamoja na wakimbizi

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kisiwa cha Lampedusa mwaka 2013; ushuhuda wa upendo na mshikamano kwa wananchi wa Rohingiya, huko Bangaladesh ni mwelekeo unaohimiza ujenzi wa utamaduni wa mshikamano na watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vita, majanga asilia, nyanyaso na mipasuko ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu, usalama na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kuweza kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linaloendelea kuwagawa na kuwasambaratisha viongozi mbali mbali duniani. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta; hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kuliko kule walikokuwa wanaishi.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano, ili kusikiliza na kujibu kwa vitendo kilio cha wakimbizi na wahamiaji; changamoto ambayo kwa sasa inapigwa danadana kwenye jukwaa la kimataifa. Kanisa kama Mama na Mwalimu anateseka sana na anapenda kuwahangaikia wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kudhulumiwa na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kisiwa cha Lampedusa mwaka 2013; ushuhuda wa upendo na mshikamano kwa wananchi wa Rohingiya, huko Bangaladesh ni mwelekeo unaohimiza utamaduni wa mshikamano na watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anaendelea kufuatilia kwa ukaribu changamoto ya wakimbizi na wahamiaji huko nchini Marekani, ambako watoto wametenganishwa na wazazi pamoja na walezi wao, hali inayotishia usalama, malezi na makuzi ya watoto hawa kwa sasa na kwa siku za usoni. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaopoteza maisha kwa utupu jangwani au kwa kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania na kusahaulika huko daima.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu na Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 25 Mei 1968. Baba Mtakatifu Francisko ameonesha umuhimu wa maisha ya ndoa na familia, dhamana iliyotekelezwa kwa umakini mkubwa na watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, ambao, Kanisa limewakumbuka kwa namna ya pekee, tarehe 26 Julai 2018.

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu ameonesha umuhimu wa kutoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na tatu, umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale wote waliokata tamaa ya maisha kutokana sababu mbali mbali. Ni fursa makini ya kuwaimarisha watu katika imani kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Imani, iwawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi, ustawi na maisha bora zaidi.

Tofauti msingi zinazojitokeza miongoni mwa binadamu ni amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaopaswa kufumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu na kamwe kisiwe ni chanzo cha kuwagawa na kuwasambaratisha watu. Kanisa Katoliki nchini Canada ni sehemu ya urithi mkubwa wa utume wa kimisionari, amana, utajiri na matumaini kwa Kanisa la Kiulimwengu. Huu ndio mwelekeo unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa wakati huu, kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican.

Mama Kanisa anapoendelea kuwekeza katika maisha na utume kwa vijana wa kizazi kipya, anawahimiza pia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwathamini, kuwaheshimu, kuwatunza na kuwahudumia wazee, ambao kwa miaka mingi wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo katika jamii. Ni kundi ambalo limechangia sana katika malezi, elimu na makuzi ya vijana wa kizazi kipya; mambo ambayo yanapenya hadi kwenye sakafu ya maisha ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni kiongozi mahiri sana katika kuwafikishia watu wa Mungu ujumbe anaokusudia kwa kutumia lugha nyepesi inayogusa undani wa maisha ya watu, kiasi hata cha kumwelewa mara moja. Kwa njia hii anaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini; Injili ya familia, haki na amani; upendo, umoja na mshikamano kati ya watu. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya watu wanaoteseka kutoka na umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, vita na mipasuko ya kijamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Kardinali Marc Ouellet amehitimisha mahubiri yake, kwa kuwataka waamini wanapoadhimisha Mafumbo ya Kanisa, yawe kweli ni chemchemi ya: amani na utulivu wa ndani; imani na matumaini katika hija ya maisha; kwa kuwasaidia kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, ili kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji, wanaokimbia: umaskini, vita, nyanyaso na dhuluma, ili waweze kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Kardinali Marc: Canada

 

27 July 2018, 17:02