Tafuta

Vatican News
ETHIOPIA ERITREA DIPLOMACY ETHIOPIA ERITREA DIPLOMACY  (ANSA)

AMECEA msikubali kupekenywa na ukabila na udini!

Askofu mkuu Protase Rugambwa amewaambia Mababa wa AMECEA kwamba, umoja na mshikamano viwe ni dira na mwongozo wa watu wa Mungu Barani Afrika. Usawa na tofauti kati ya watu ni sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu ili kushirikishana, kutajirishana na kukamilishana katika utu na tamaduni mbali mbali! Tofauti kati ya watu ni utajiri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Tumewashirikisha kwa kina kuhusu hotuba ya Askofu mkuu Rugambwa Katibu  wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, juu ya mchango mkubwa uliotolewa na Mwenyeheri Paulo VI, katika Waraka wake wa kitume “Africae Terrarum” yaani “Bara la Afrika” uliochapishwa kunako tarehe 29 Oktoba 1967.

Mwenyeheri Paulo VI, anakazia pamoja na mambo mengine: Utajiri, amana na urithi mkubwa wa Mapokeo kutoka Barani Afrika sanjari na mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, leo, tunapenda kuzama zaidi katika mambo msingi yaliyojiri katika hotuba yake elekezi inayopaswa kufanyiwa kazi na Mababa wa AMECEA ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mungu katika Nchi za AMECEA, vinginevyo nyaraka hizi zitaendelea kuhifadhiwa kwenye makabati bila kuzaa matunda yanayokusudiwa!

Askofu mkuu Rugambwa amekaza kwamba, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni dhamana na utume wa Kanisa unaobubujika kutoka katika Injili inayopania kumkomboa mwanadamu: kiroho na kimwili kwa kujikita katika haki na kujenga mfumo wa kijamii unaosimikwa katika haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wakristo wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya umoja, haki na amani  na kamwe wasikubali ukabila na udini kuwa ni chanzo cha kashfa ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, bali wasaidie kuganga na kuponya kashfa hii inayoendelea kulipekenyua Bara la Afrika.

Umoja, udugu na mshikamano viwe ni dira na mwongozo wa watu wa Mungu Barani Afrika. Askofu mkuu Rugambwa amechambua kwa kina na mapana kuhusu usawa na tofauti kati ya watu kama sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu na kwamba, tofauti hizi ziwe ni chachu ya kushirikishana na kutajirishana karama, fadhila na wema, ili kukamilishana katika utu na tamaduni zao. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima, usawa na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kudumishwa na wote kama msingi wa ujenzi wa Injili ya amani duniani.

Likini ikumbukwe kwamba, amani inafumbatwa katika mambo makuu manne: ukweli, haki, upendo na uhuru. Mambo haya msingi yawe ni chachu ya maendeleo endelevu na fungamani kwa watu wa Mungu Barani Afrika ili kuweza kupambana na: baa la njaa, umaskini, ujinga na magonjwa, mambo yanayohatarisha amani na mafungamano ya kijamii. Kuna haja ya kusimama kidete anasema Askofu mkuu Rugambwa kujenga na kudumisha amani katika Jumuiya ya Kimataifa, kwa kukuza na kudumisha umoja na mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni, msamaha sanjari na kufutilia mbali mashindano ya silaha na badala yake, Jamii iwekeze zaidi katika mchakato wa kupambana na umaskini.

Mwenyeheri Paulo VI alikuwa na mchango mkubwa sana kwa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, kwani ni muasisi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ambayo ilianzishwa kunako mwaka 1969 na hapo mwakani, 2019, SECAM inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Iwe ni fursa ya kufanya rejea tena katika Waraka wa Kitume Africae Terrarum, yaani “Bara la Afrika” inayowataka waafika kuwa ni wadau wa maendeleo yao wenyewe na wamisionari Barani Afrika. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika mchakato wa umoja na mshikamano; kwa kushirikiana na kushirikishana rasilimali watu, fedha na karama kwa ajili ya ustawi, maendeeo na mafao ya Bara la Afrika.

Askofu mkuu Protase Rugambwa anawataka Mababa wa AMECEA kufanya marekebisho makubwa katika miundo mbinu yake mintarafu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “ Furaha ya Injili anayekazia umuhimu wa kulipyaisha Kanisa kwa kujikita katika wongofu wa kimisionari na kichungaji; majadiliano katika ukweli na uwazi. Kwa kuendelea kujikita katika kutangaza na kushuhudia Injili; kwa kuimarisha utume wa Parokia na Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo; kwa kuendeleza umoja wa kimisionari na urika kati ya Maaskofu pamoja na kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea. Mchakato huu uiwezeshe AMECEA kutemba kwa pamoja kwa kusoma alama za nyakati na kuzijibu kwa mwanga wa Injili.

Askofu mkuu Rugambwa amekumbusha kwamba, tarehe 30 Novemba 2019, Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume “Maximum Illud” unaopembua mchakato mzima wa shughuli za kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Ni waraka unaokazia umuhimu wa maandalizi ya wamisionari na wakleri katika maisha na utume wa Kanisa; umuhimu wa mapadre, watawa na waamini walei kuchuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wanashirikishwa kwa namna ya pekee utume wa kimisionari kwa njia ya sala; kwa kusaidia kutegemeza miito mbali mbali ndani ya Kanisa sanjari na kuchangia kikamilifu katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa Mahalia.

Maandalizi ya maadhimisho ya kipindi hiki maalum cha kutangaza na kushuhudia Injili kilisaidie Kanisa kuwa daima katika mchakato wa kujiinjilisha kwanza. Jumuiya za waamini ziwe ni jumuiya za matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kuwashirikisha wengine. Ziwe ni Jumuiya za upendo wa kidugu; zenye utamaduni wa kusikilizana daima sanjari na kuamini kuhusu matumaini yanayofumbatwa katika Amri mpya ya upendo kwa Mungu na jirani.

Familia ya Mungu, kuna wakati inashawishiwa na kujikuta ikimezwa sana na malimwengu. Kumbe, kuna haja kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kusikiliza matendo makuu ya Mungu yakitangazwa tena mbele yake; kwamba, wanahamasishwa kumwongokea Mwenyezi Mungu na wanaalikwa kuungana naye tena kwani daima familia ya Mungu inapaswa kuinjilishwa, ili kujichotea nguvu ya ya kutangaza na kushuhidia Injili. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jubilei ya miaka 100 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume “Maximum illud”, Mwezi Oktoba, 2019 kitakuwa ni kipindi cha sala pamoja na shuhuda za watakatifu na wafia dini.

Sikiliza

 

17 July 2018, 16:06