Tafuta

Viongozi wakuu wa Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END” Jumamosi, tarehe 4 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Viongozi wakuu wa Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END” Jumamosi, tarehe 4 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.   (Vatican Media)

Waamini Simameni Kidete Kulinda na Kutetea Tunu Msingi za Maisha ya Ndoa na Familia

Viongozi wakuu wa Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END” Jumamosi, tarehe 4 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na PapaFrancisko na katika amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete ili kupambana na tamaduni zinazotishia tunu msingi za maisha ya ndoa. Wawasaidie vijana kutambua uzuri wa wito wa maisha ya ndoa na familia, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linapaswa kuwa makini ili kuwasaidia wanandoa kudumisha maisha yao ya ndoa mintarafu Mafundisho ya Kanisa kama ambavyo Mtakatifu Paulo anavyofafanua uhusiano kati ya Kristo Yesu na mchumba wake Kanisa, ambaye amejisadaka hata kufa kwa ajili yake pale Msalabani. Kwa njia hii, mapenzi ya Mungu kwa ajili ya familia nzima ya binadamu yakatendeka. Maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa yanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha. Huu ni mwaliko wa kutembea kwa pamoja na Kanisa ndani ya Kanisa kwa kujikita na kuambata njia ya utakatifu wa maisha. Ndoa kadiri ya Agano Jipya ni safari ya imani. Kumbe, familia ya Kikristo inapata chimbuko lake katika maisha ya ndoa ambayo ni ushirikiano wa agano la upendo kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika hija hii ya maisha ya kiroho kuna haja kuwa na wachungaji watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia wanandoa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao. Ndoa na familia ni utume unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa; unapaswa kukita mizizi yake katika ari na mwamko wa kimisionari; ili kuwawezesha wanandoa kuwa wakarimu, tayari kupokea maisha mapya kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ili wanandoa waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, wanapaswa kupata maandalizi makini yanayogusa masuala ya kisaikolojia, upendo wa dhati, mahusiano na mafungamano yao katika maisha ya unyumba ili kuwasaidia kupata ukomavu na hatimaye udumifu katika maisha yao. Wanandoa na familia wanapaswa kukuza na kudumisha ndani mwao wito wa ndoa, ili hatimaye, kusimama kidete, kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya ndoa na familia katika mazingira ya kifamilia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla wake. Wanandoa wanapaswa kutangaza na kushuhudua uzuri, utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa na familia kama kielelezo chenye mvuto na mashiko.

Waamini simameni kidete kulinda na kutetea tunu msingi za ndoa
Waamini simameni kidete kulinda na kutetea tunu msingi za ndoa

Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END” kilizaliwa kunako mwishoni mwa miaka 1930, kama mpango wa wanandoa kukutana kila mwezi chini ya uongozi wa Padre Henri Caffaril, ili kuzama kwa undani zaidi katika maana ya Sakramenti ya ndoa, ili kujiingiza katika jamii kama familia na wenza wa Kikristo. Kukua kwa utume wa ndoa na familia kulisaidia kuibua vuguvugu la wanandoa kutaka kuzama zaidi katika wito na maisha ya ndoa na hivyo kurasimishwa na kutangazwa, tarehe 8 Desemba 1947, Chama cha Kitume cha “Équipes Notre-Dame, END” pamoja na mambo mengine kinapania kuongeza uzoefu wa maisha ya ndoa kwa mwanga wa Neno la Mungu, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Na ilipogota tarehe 19 Aprili 1992 Baraza la Kipapa la Walei lilitangaza kutambuliwa kwa “Equipes Notre-Dame kama Chama cha Kimataifa cha Waamini Walei chenye hadhi na haki ya Kipapa. Viongozi wakuu wa Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END” Jumamosi, tarehe 4 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete ili kupambana na tamaduni zinazotishia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wawasaidie vijana kutambua uzuri wa wito wa maisha ya ndoa na familia, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa sababu ndoa ya Kikristo inadumu maisha yote, kwa kusaidiana katika hija ya maisha na kwamba, ndoa ya Kikristo ni amana na utajiri unaopaswa kulindwa na kuendelezwa. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaishi wito wa maisha ya ndoa na familia kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ndoa ni wito, vijana wafundishwe na namna ya kuishi wito huu.
Ndoa ni wito, vijana wafundishwe na namna ya kuishi wito huu.

Katika ulimwengu mamboleo kuna dhoruba kali inayotishia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, changamoto na mwaliko wa kulinda tunu msingi za maisha ya ndoa, ili kulinda: upendo, mahusiano na mafungamano ya familia, tayari kuyatolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko wa kuwapenda, kuwathamini na kuwatunza wazazi, kwa sababu wao ni chanzo na asili ya maisha yao. Waamini wawasaidie vijana kutambua kwamba ndoa ya Kikristo ni wito wa Mungu kwa mwanaume na mwanamke, ili waweze kuishi kwa pamoja na kuzaa watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, kwa kutambua kwamba, wao ni Sakramenti. Upendo wa wanandoa ni kielelezo cha upendo wa Kristo kwa waja wake na kwamba, ni Kristo Yesu anayewatia shime kuendelea kukua na hatimaye, kukomaa kwa pamoja, huku wakiwa wameunganika katika kifungo cha upendo wa maisha ya ndoa. Huu ni upendo kati ya wanandoa na upendo kati yao na Kristo Yesu; upendo unaodumu maisha yote. Watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye mlango naye anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Yn 10:9.

Uaminifu na udumifu katika maisha ya ndoa na familia
Uaminifu na udumifu katika maisha ya ndoa na familia

Wanandoa wanapaswa kuheshimiana, kupendana na kuthaminiana hadi kifo kitakapowatenga. Baba Mtakatifu Francisko amekitaka Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END” kuwasimamia na kuwaongoza wanandoa wapya, ili waweze kuishi kwa ukamilifu tasaufi ya maisha ya ndoa na familia; wasaidiwe kutambua umuhimu wa zawadi ya imani katika maisha ya mtu binafsi na kama wanandoa, huku wakijitahidi kutoa nafasi kwa Kristo Yesu katika Neno, Sakramenti na huduma makini kwa jirani zao. Washirikiane na Mapadre parokiani, ili kuziwezesha familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ziwe ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Wanandoa waheshimiane, wapendane na kuthaminiana
Wanandoa waheshimiane, wapendane na kuthaminiana

Familia zisaidiane kukuza na kudumisha wito wa maisha ya ndoa na familia pamoja na wito wa kipadre; ili wote kwa pamoja wajitahidi kujenga na kudumisha utume wa Kanisa la kimisionari na kisinodi; kwa kushirikishana karama na zawadi walizokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Wajenge na kudumisha mtandao wa familia, kama Kanisa dogo la nyumbani, kwa kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki. Chama cha Kitume Kimataifa cha “Équipes Notre-Dame, END”, Mwezi Julai 2024 kitafanya mkutano wa Kimataifa mjini Torino, mwaliko kwa wanachama kuanza kujenga Jumuiya ya Kisinodi kwa kujikita katika utamaduni wa kusikilizana, kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati itakayopitishwa kwa pamoja. Kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anawataka wanandoa na familia kujenga utamaduni wa kusali pamoja kama familia; sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024.

Wito wa ndoa
05 May 2024, 14:47