Tafuta

Kuna haja ya kukuza na kudumisha haki jamii katika ulimwengu wa wafanyakazi; kwa kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti na hasa zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii Kitaifa na Kimataifa. Kuna haja ya kukuza na kudumisha haki jamii katika ulimwengu wa wafanyakazi; kwa kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti na hasa zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii Kitaifa na Kimataifa.  (ANSA)

Ni Muhimu Kulinda Utu, Heshima na Haki Msingi za Wafanyakazi

Mkutano huu unaadhimishwa kwa kuzingatia mtindo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa na utamaduni wa kusikilizana, kufanya mang’amuzi ya pamoja na hatimaye, utekelezaji wake, daima mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza kwa kutambua kwamba, wote wana utu sawa na uhuru unaosimikwa katika upendo. Matokeo ya tafiti ni muhimu sana katika kujenga na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wafanyakazi wa Mashirika ya Kazi Kimataifa, Wawakilishi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki  sehemu mbalimbali za dunia, Watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Wawakilishi wa Madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na viongozi wa vyama na mashirika yasiyo ya Kiserikali, ambao wamejikita katika kulinda, kutetea na kutunza kazi kwa siku za usoni, mara baada ya utekelezaji wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”  Jumatano tarehe 8 Mei 2024, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, wajumbe hawa wamekuwa wakishiriki kikamilifu majadiliano, tafiti pamoja na kuweka mbinu mkakati kwa ajili ya upyaisho wa ajira, ili kuleta usawa katika mfumo wa ajira duniani, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi sehemu mbalimbali za dunia. Mradi huu, unasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC, iliyoanzishwa na Papa Pio XII kufuatia athari kubwa za Vita kuu ya Pili ya Dunia na Katiba yake ikapitishwa rasmi kunako mwaka 1951, ili kusaidia mchakato wa kuwahudumia wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa, kama vile: Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR pamoja na Mashirika ya Kiraia. Tume hii inashirikiana kwa karibu sana na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao wana: utu, heshima na utambulisho wao kama binadamu kama anavyokazia kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kuna umuhimu wa kulinda utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi
Kuna umuhimu wa kulinda utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi

Ni katika muktadha huu, Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika hotuba yake ya ufunguzi, amewashukuru wajumbe wote kwa sadaka na majitoleo yao yanayopania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha haki jamii katika ulimwengu wa wafanyakazi; kwa kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti na hasa zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii Kitaifa na Kimataifa. Mkutano huu unaadhimishwa kwa kuzingatia mtindo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa na utamaduni wa kusikilizana, kufanya mang’amuzi ya pamoja na hatimaye, utekelezaji wake, daima mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza kwa kutambua kwamba, wote wana utu sawa na uhuru unaosimikwa katika upendo. Matokeo ya utafiti huu ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika kutafuta na kudumisha ustawi na mafao ya wengi; jambo ambalo wanapaswa kuendelea kulivalia njuga. Huu ni mwaliko wa kujenga umoja na utofauti ili kuleta mageuzi yanayokusudiwa kuanzia katika ngazi ya chini kabisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, matatizo ya kijamii yanapaswa kuangaliwa na mfumo jamii na sio ujumla wa matendo mazuri ya watu binafsi. Wajibu huu utamletea mwanadamu madai makubwa ambayo yeye mwenyewe asingeweza kuyafikia kwa nguvu zake au hata kwa kujumuisha jitihada za binadamu wengine waliolelewa kwa njia ya kibinafsi. Kazi ya kuutawala ulimwengu inahitaji umoja wa ustadi na mafanikio, inayoweza kukua na kutokana na fikra au mtazamo tofauti kabisa. Ikolojia wongofu inayohitajika kuleta mabadiliko ya kudumu ni ile ya wongofu wa jumuiya pia. Rej. Laudato si, 219.

Wongofu wa kiikolojia ni muhimu kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi
Wongofu wa kiikolojia ni muhimu kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi

Katika mkutano huu, wajumbe hawa wameongozwa na kauli mbiu: "Utunzaji ni kazi, kazi ni utunzaji." Kujenga jumuiya yenye mabadiliko ya Kimataifa.” Huu ni utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huu mkubwa baada ya kukamilisha mradi wa kwanza wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Lengo ni kuweza kuratibu rasilimali zote muhimu kwa kuzihusisha Taasisi mbalimbali ili hatimaye kuwa na sera na mwelekeo utakaotumia nguvu zilizopo kubaini mifumo ya kijamii inayoweza kugeuka kuwa ni majanga hatari kijamii. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amejikita katika mambo makuu matatu: yaani kazi zenye staha pamoja na viwanda vya uziduaji, ili viweze kuwa na manufaa kwa nchi ambazo zina rasilimali zikiwemo madini, gesi na mafuta sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Kazi zenye staha na uhakika wa usalama wa chakula; Kazi zenye staha na Wimbi kubwa la Uhamiaji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi zenye staha pamoja na viwanda vya uziduaji, ili viweze kuwa na manufaa kwa nchi ambazo zina rasilimali zikiwemo madini, gesi na mafuta sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote zinapaswa kulinda usalama pamoja na afya ya kimwili na kiakili. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2023 zaidi ya watu milioni 280 kutoka katika nchi 59 walikabiliwa na ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula, kiasi kwamba, watu hawa wote wanahitaji msaada wa chakula cha dharura, ili kukabiliana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha bila kusahau athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika janga la umaskini pamoja na kuendelea kutegemea msaada wa chakula kutoka nje, hali inayoiacha miundombinu mingi ikiwa katika hali ya hatari sana. Maeneo ya Ukanda wa Gaza na Sudan ya Kusini yameathirika sana kutokana na vita inayoendelea katika maeneo haya.

Kazi zenye staha na uhakika wa usalama wa chakula ni muhimu.
Kazi zenye staha na uhakika wa usalama wa chakula ni muhimu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna uhusiano wa karibu kati ya kazi zenye staha na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Watu wanakimbia kutoka katika nchi zao ili kutafuta fursa za ajira, lakini hawa ni watu wanaokumbana na vikwazo vingi, vikiwemo maamuzi mbele, itikadi na mawasiliano duni. Lakini kimsingi hawa ni watu wanaochangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kiuchumi na kijamii kwa kuchangia nguvu kazi kutokana na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa sanjari na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa. Licha ya wakimbizi na wahamiaji kuchangia kwenye uchumi, lakini bado ni watu wanaochukuliwa kuwa ni “watu wa kuja” kwani hawana haki katika huduma za afya kijamii, kiuchumi na hata katika huduma za kisaikolojia. Haki jamii ni kati ya mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuondoa kabisa mfumo ya kibaguzi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa wafanyakazi na haki zao msingi. Kumbe, kazi zenye staha zinapaswa pia kuendelea kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Zote hizi ni changamoto pevu anasema Baba Mtakatifu Francisko zinazohitaji kupyaishwa kwa kutengeneza mkataba mpya wa kazi, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili hatimaye, kujenga mshikamano katika jumuiya ya binadamu.

Kazi
09 May 2024, 17:23