Tafuta

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tamko Kuhusu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 Ya Ukristo: 2025-2026

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Yesu aliye hai na mbaye pia ni Mlango wa uzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini. Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani. Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325. Nanga ya matumaini katika maisha ya uzima wa milele yanayopata chimbuko lake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu; Ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; hukumu ya Mungu na mwaliko kwa waamini kujitakasa; Rehema na Sakramenti ya Upatanisho; Wamisionari wa huruma ya Mungu. Bikira Maria ni shuhuda wa hali ya juu kabisa wa matumaini, Nyota ya Bahari na kwamba, hija ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iwasaidie waamini kujikita katika Maandiko Matakatifu.

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anafafanua kwa kina fadhila ya matumaini kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji usiokuwa na kizuizi wala mipaka, ili watu wote wapate kusikia Habari Njema ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha Habari Njema ya Matumaini na utimilifu wa ahadi za Baba wa milele na hivyo kumwingiza mwamini katika mawimbi ya utukufu wa furaha inayosimikwa katika upendo ambao kamwe haudanganyi. Matumaini yanapata chimbuko lake katika upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki, ili kuhesabiwa haki, kupatanishwa na hatimaye kuokolewa. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini matumaini mapya na kwamba, hakuna anayeweza kuwatenga na upendo wa Kristo. “Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Rum 8: 35-39.

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025: Matumaini
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025: Matumaini

Hii ni kwa sababu matumaini yanasimikwa katika imani na kurutubishwa katika upendo! Yaani matumaini kwa Neno la Mungu yawawezeshe waamini: kuamini, kutumaini na kupenda. Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa katika maisha na utume wake alikumbana na mateso, madhulumu, kiasi hata cha kutoeleweka, lakini akagundua ndani mwake kwamba, nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ilikuwa inatoka katika Msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, kiasi cha kuvuka yote haya kwa uvumilivu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni wavumilivu wanapokumbana na matatizo na changamoto za maisha kama anavyoshuhudia Mtakatifu Francisko wa Assisi katika utenzi wake wa kazi ya uumbaji. Hii ni kwa sababu Mungu ni mwenye saburi na faraja na kwamba, Roho Mtakatifu anapyaisha matumaini na kuyaimarisha kwa fadhili na mtindo wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni hija ya matumaini ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya msamaha na maadhimisho mbalimbali ya Jubilei kama yalivyojitokeza kwenye Jubilei ya kwanza iliyoadhimishwa kunako mwaka 1, 300. Maadhimisho haya ni mwendelezo wa nguvu na msamaha wa Mungu unaowasindikiza na kuwaambata waamini katika hija ya maisha yao ya kiroho. Hija ni kati ya mambo msingi yanayofumbatwa katika maadhimisho ya Jubilei na katika muktadha huu, waamini wanahimizwa kuwa ni mahujaji wa matumaini, ili kuonesha uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kuna waamini wanaoendelea na hija ya maisha yao kama sehemu ya Njia ya Msalaba, kwao hawa wote ni ujumbe wa matumaini kwamba, wanapendwa na Mama Kanisa na kamwe hatawaacha bali ataendelea kutembea pamoja nao. Maadhimisho ya Jubilei ni matukio ya neema na baraka: Yaani Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Kanisa liliadhimisha kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu; Jubilei ya Mwaka 2015 ilipania pamoja na mambo mengine, kuwafunulia waamini “Uso wa huruma ya Mungu” kiini cha Habari Njema ya Wokovu, kwa kukazia imani, upendo na matumaini.

Kauli mbiu Spes non confundit
Kauli mbiu Spes non confundit

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yatafunguliwa rasmi tarehe 24 Desemba 2024 sanjari na Makanisa makuu yote sehemu mbalimbali za dunia. Dominika tarehe 29 Desemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko atafungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 1700 tangu Kanisa hili lilipotabarukiwa. Tarehe Mosi Januari 2025 Baba Mtakatifu atafungua lango la Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Mama wa Mungu na tarehe 5 Januari atafungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta. Makanisa yote haya yatapaswa kufungwa rasmi tarehe 28 Desemba 2025. Katika maadhimisho yote haya, Rehema itatolewa kwa waamini watakaofuata masharti; Neno la Mungu litapewa kipaumbele cha pekee na sehemu za Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 zinapaswa kusomwa. Maadhimisho ya Jubilei yatahitimishwa tarehe 6 Januari 2026. Baba Mtakatifu anatamani kuona kwamba, mwanga angavu wa matumani unawafikia watu wote wa Mungu kama ujumbe wa upendo na Kanisa liwe ni shuhuda aminifu wa ujumbe huu wa upendo kila pembe ya dunia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanalitaka Kanisa kusoma alama za nyakati kwa mwanga wa Injili, ili ziweze kutafsiriwa kuwa ni alama za matumaini. Alama ya kwanza ni amani, waamini wanahimizwa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa amani, dhidi ya utamaduni wa kifo unaowakatisha watu tamaa ya kuzaa watoto. Vijana wahamasishwe kufunga ndoa ili wapate watoto, kielelezo cha matumaini yanayonogesha matumaini. Jubilei iwe ni alama ya matumaini kwa wafungwa magerezani, kwa kupewa msamaha, au kupunguziwa adhabu zao na wafungwa wenyewe wawe ni mashuhuda wa utekelezaji wa sheria. Baba Mtakatifu anasema anatarajia kufungua lango la moja ya magereza kama kielelezo cha matumaini mapya. Alama ya matumaini waoneshwe wagonjwa majumbani na hospitalini; waoneshwe vijana wa kizazi kipya; wakimbizi na wahamiaji; wazee na maskini. Ikumbukwe kwamba, maskini mara nyingi ni wahanga.  

Tumaini Halitahayarishi
Tumaini Halitahayarishi

Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani. Itakumbukwa kwamba, kuna deni kubwa la ikolojia linalopaswa kufutwa ili kukoleza amani, kukuza na kudumisha haki pamoja na kuwalisha wenye njaa. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo itakuwa ni fursa kwa Wakristo kumtangaza na kumshuhudia Mungu katika umoja wao. Nanga ya matumaini katika maisha ya uzima wa milele yanayopata chimbuko lake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Msimamo wa Kanisa mbele ya ukani Mungu “Ukikosekana msingi wa kimungu na tumaini la uzima wa milele, basi hadhi ya binadamu inaudhiwa sana, kama inavyoonekana mara nyingi siku za leo. Hoja za maisha na mauti, za dhambi na uchungu, huendelea kuwa mafumbo yasiyo na ufumbuzi, kiasi kwamba, mara nyingi wanadamu huzama katika kukata tamaa.” Gaudium et spes, 21. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kiini cha imani ya Kanisa, matumaini ya watu wa Mungu kwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wajitahidi kulipokea fumbo la kifo katika maisha yao kwa imani na matumaini. Mashuhuda wa imani ni amana na utajiri wa Kanisa, changamoto na mwaliko wa Makanisa yote ya Kikristo kuwaadhimisha kwa pamoja. Waamini wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya kweli, kwa kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu mwenyezi.

Baadhi ya wawakilishi wakipokea Tamko la Maadhimisho ya Jubilei
Baadhi ya wawakilishi wakipokea Tamko la Maadhimisho ya Jubilei

Waamini baada ya kuhitimisha hija ya maisha yao hapa duniani, watakabiliwa na hukumu ya Mungu inayofumbatwa katika katika ukweli kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo na kwamba upendo kwa jirani ni kipimo cha hukumu ya Mungu. Kumbe, kuna haja kwa waamini kujitakasa na kusali ili kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliohitimisha safari ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi; hii ni hija ya mshikamano na kwamba, rehema na msamaha wa dhambi unapania kutolewa kwa waamini marehemu. Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendo na huruma ya Mungu haina mipaka. Baba Mtakatifu anakazia msamaha unaoweza kuleta mabadiliko kwa siku za usoni, kwa kuishi bila kutaka kulipiza kisasi na hivyo kuwa na amani na utulivu wa roho. Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” aliwathibitisha Wamisionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume wa “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anafafanua kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani.

Jubilei ya Mwaka 2025- 6 Januari 2026
Jubilei ya Mwaka 2025- 6 Januari 2026

Hawa ni Mapadre ambao wamepewa mamlaka ya kuwaondolea waamini dhambi ambazo kwa kawaida zilikuwa zinaondolewa tu na Kiti cha Kitume. Mapadre hawa hasa ni ishara hai ya namna Baba mwenye huruma anavyowapokea wale wanaotafuta huruma na msamaha wake. Hawa ni wamisionari wa huruma ya Mungu kwa sababu wao ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo, tayari kutweka hadi kilindini ili kuanza maisha mapya ya Ubatizo. Wamisionari hawa katika utume wao wanaongozwa na kauli mbiu “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rej. Rom. 11: 32) na Rej. Misericordiae vultus 18-19. Baba Mtakatifu Francisko anasema kila mwamini anayo haki ya kupata msamaha wa dhambi na faraja kutoka kwa Mungu. Bikira Maria ni shuhuda wa hali ya juu kabisa wa matumaini, Nyota ya Bahari, Mama wa matumaini na kwamba, hija ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo iwasaidie waamini kujikita katika Maandiko Matakatifu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu!

Kristo Yesu ni Mlango wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mlango wa uzima wa milele

Baba Mtakatifu anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Madhabahu yawe ni vituo vya: Sala, Sakramenti za Kanisa na mahali pa tafakari ya Neno la Mungu tayari kupyaisha matumaini na faraja kwa wale wote wanaokimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo ni fursa ya kuendelea kupyaisha imani, matumaini na mapendo; kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya watu wa Mungu; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; haki, amani na maridhiano. Mzaburi anasema, “Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.” Zab 27:14. Baba Mtakatifu anahitimisha Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa kumwomba, Mwenyezi Mungu awakirimie waja wake nguvu ya matumaini ili iweze kuujaza uwepo wao nyakati hizi, huku wakingojea kwa imani kurudi kwa Kristo Yesu anayepaswa kusifiwa na kutukuzwa sasa na milele yote!

Mwaka wa Jubilei 2025
09 May 2024, 18:10