Tafuta

Mradi huu, unasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC. Mradi huu, unasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC.  (Vatican Media)

Mfumo Mpya wa Kazi Ili Kuleta Usawa; Kukazia Utu na Haki Jamii

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amejikita katika mambo makuu matatu: yaani kazi zenye staha pamoja na viwanda vya uziduaji, ili viweze kuwa na manufaa kwa nchi ambazo zina rasilimali zikiwemo madini, gesi na mafuta sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Kazi zenye staha na uhakika wa usalama wa chakula; Kazi zenye staha na Wimbi kubwa la Uhamiaji. Amekazia umuhimu wa jamii kujikita katika haki jamii ili kudumisha usawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wafanyakazi wa Mashirika ya Kazi Kimataifa, Wawakilishi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki  sehemu mbalimbali za dunia, Watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Wawakilishi wa Madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na viongozi wa vyama na mashirika yasiyo ya Kiserikali, ambao wamejikita katika kulinda, kutetea na kutunza kazi kwa siku za usoni, mara baada ya utekelezaji wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”  Jumatano tarehe 8 Mei 2024, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, wajumbe hawa wamekuwa wakishiriki kikamilifu majadiliano, tafiti pamoja na kuweka mbinu mkakati kwa ajili ya upyaisho wa ajira, ili kuleta usawa katika mfumo wa ajira duniani, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi sehemu mbalimbali za dunia. Mradi huu, unasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC, iliyoanzishwa na Papa Pio XII kufuatia athari kubwa za Vita kuu ya Pili ya Dunia na Katiba yake ikapitishwa rasmi kunako mwaka 1951, ili kusaidia mchakato wa kuwahudumia wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa, kama vile: Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR pamoja na Mashirika ya Kiraia. Tume hii inashirikiana kwa karibu sana na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao wana: utu, heshima na utambulisho wao kama binadamu kama anavyokazia kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Upyaisho wa sera na mikakati ya kazi, ili kulinda na kudumisha utu na haki
Upyaisho wa sera na mikakati ya kazi, ili kulinda na kudumisha utu na haki

Katika mkutano wao kwa siku za hivi karibuni, wajumbe hawa wataongozwa na kauli mbiu: "Utunzaji ni kazi, kazi ni utunzaji." Kujenga jumuiya yenye mabadiliko ya Kimataifa.” Huu ni utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huu mkubwa baada ya kukamilisha mradi wa kwanza wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Lengo ni kuweza kuratibu rasilimali zote muhimu kwa kuzihusisha Taasisi mbalimbali ili hatimaye kuwa na sera na mwelekeo utakaotumia nguvu zilizopo kubaini mifumo ya kijamii inayoweza kugeuka kuwa ni majanga hatari kijamii. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amejikita katika mambo makuu matatu: yaani kazi zenye staha pamoja na viwanda vya uziduaji, ili viweze kuwa na manufaa kwa nchi ambazo zina rasilimali zikiwemo madini, gesi na mafuta sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Kazi zenye staha na uhakika wa usalama wa chakula; Kazi zenye staha na Wimbi kubwa la Uhamiaji.

Utunzaji ni kazi na kazi ni utunzaji
Utunzaji ni kazi na kazi ni utunzaji

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi zenye staha pamoja na viwanda vya uziduaji, ili viweze kuwa na manufaa kwa nchi ambazo zina rasilimali zikiwemo madini, gesi na mafuta sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote zinapaswa kulinda usalama pamoja na afya ya kimwili na kiakili. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2023 zaidi ya watu milioni 280 kutoka katika nchi 59 walikabiliwa na ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula, kiasi kwamba, watu hawa wote wanahitaji msaada wa chakula cha dharura, ili kukabiliana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha bila kusahau athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika janga la umaskini pamoja na kuendelea kutegemea msaada wa chakula kutoka nje, hali inayoiacha miundombinu mingi ikiwa katika hali ya hatari sana. Maeneo ya Ukanda wa Gaza na Sudan ya Kusini yameathirika sana kutokana na vita inayoendelea katika maeneo haya.

Utu, heshima na utambulisho wao kama binadamu ni muhimu
Utu, heshima na utambulisho wao kama binadamu ni muhimu

Baba Mtakatifu anasema, kuna uhusiano wa karibu kati ya kazi zenye staha na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Watu wanakimbia kutoka katika nchi zao ili kutafuta fursa za ajira, lakini hawa ni watu wanaokumbana na vikwazo vingi, vikiwemo maamuzi mbele, itikadi na mawasiliano duni. Lakini kimsingi hawa ni watu wanaochangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kiuchumi na kijamii kwa kuchangia nguvu kazi kutokana na idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa sanjari na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa. Licha ya wakimbizi na wahamiaji kuchangia kwenye uchumi, lakini bado ni watu wanaochukuliwa kuwa ni “watu wa kuja” kwani hawana haki katika huduma za afya kijamii, kiuchumi na hata katika huduma za kisaikolojia. Haki jamii ni kati ya mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuondoa kabisa mfumo ya kibaguzi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa wafanyakazi na haki zao msingi. Kumbe, kazi zenye staha zinapaswa pia kuendelea kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Zote hizi ni changamoto pevu anasema Baba Mtakatifu Francisko zinazohitaji kupyaishwa kwa kutengeneza mkataba mpya wa kazi, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili hatimaye, kujenga mshikamano katika jumuiya ya binadamu.

Upyaisho wa Kazi
08 May 2024, 15:23