Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 2 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa Anglikan. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 2 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa Anglikan.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Viongozi Wakuu wa Kanisa Anglikan

Papa Francisko ameonesha furaha ya kukutana mara kwa mara na Askofu Justin Welby kama kielelezo cha ushirikiiano wa kidugu; amegusia mchango wa Tume ya Pamoja ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikan katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Wakatoliki na Waanglikan wanaitwa kusali na kusikilizana ili kujenga ushirika na Kristo na umoja kati ya waamini; Ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi, lengo ni kujenga umoja wa Kanisa la Kristo Yesu Mfufuka! Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika: Damu ya mashuhuda na waungama dini ya Kikristo; Uekumene wa sala unaofumbatwa katika tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu ili kujenga umoja na udugu katika Kristo Yesu; Uekumene wa maisha ya kiroho unaojikita katika kuthaminiana; na hatimaye, Uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Hawa ni wakimbizi na wahamiaji, pamoja na maskini wa hali na kipato! Ni katika muktadha huu wa majadiliano ya kiekumene, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Sherehe ya Pasaka, Kristo Mfufuka jioni siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Kristo Mfufuka na kuwaondolea hofu na kuwakirimia amani na Roho wake Mtakatifu; akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Rej. Yn 20:19-23, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 2 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa Anglikan chini ya uongozi wa Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani.

Askofu mkuu Justin Welby akibadilishana zawadi na Papa Francisko
Askofu mkuu Justin Welby akibadilishana zawadi na Papa Francisko

Baba Mtakatifu katika hotuba yake ameonesha furaha yake kwa kuweza kukutana mara kwa mara na Askofu Justin Welby kama kielelezo cha ushirikiiano wa kidugu kwa niaba ya Injili, amegusia mchango wa Tume ya Pamoja ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikan katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Wakatoliki na Waanglikan wanaitwa kusali na kusikilizana ili kujenga ushirika na Kristo na umoja kati ya waamini; Ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi, lengo ni kujenga umoja wa Kanisa la Kristo Yesu Mfufuka. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wakiangalia historia ya maisha yao, wanatambua kwamba, Kristo Mfufuka yupo pamoja na kati yao, ili kuwakirimia amani na Roho wake Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasema, amekuwa akishirikiana kwa karibu sana na Askofu mkuu Justin Welby katika sala na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu. Sala hii imekuwa ni wakati ule Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, lengo ni kuendeleza mchakato wa upatanisho, ili kujenga umoja wa Kanisa moja la Kristo, kielelezo makini cha ushirikiano wa kidugu kwa niaba ya Injili. Kristo Yesu anawahamasisha wafuasi wake kujenga na kudumisha ushirika kati yao, kwa kutembea kwa pamoja katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa: katika shughuli za kichungaji, kitamaduni na kijamii, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya Kristo Yesu, kwa kutambuana kuwa ni ndugu katika Kristo kwa njia ya Ubatizo mmoja. Baba Mtakatifu ameupongeza mchango wa Tume ya Pamoja ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikan katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, na hivyo kusaidia kutatua changamoto na vikwazo vilivyokuwa vinagumisha mchakato wa umoja wa Kanisa kwa kutambua na kukiri imani inayofumbatwa katika imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Ubatizo Mmoja kwa maondoleo ya dhambi, Maandiko Matakatifu, Kanuni ya Imani ya Nicea, Mafundisho ya Mtaguso wa Chaledonia pamoja na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, amana, utajiri na urithi wa pamoja.

Wakuu wa kanisa Anglikan wakizungumza na Papa Francisko
Wakuu wa kanisa Anglikan wakizungumza na Papa Francisko

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi hiki cha Pasaka, Maandiko Matakatifu yanaelezea imani na udugu wa Wakristo, ujasiri katika kukabiliana na madhulumu; furaha ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; dhamana na wajibu wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wakristo wasisahau kwamba, hata katika Kanisa la Mwanzo, hali ya kutoelewana miongoni mwa Mitume, ilikuwepo, lakini jambo la msingi ni kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza, ili kukoleza ari na moyo wa majadiliano, umoja na mshikamano, ili kujenga ushirika na Kristo Yesu na kuendeleza umoja kati ya wafuasi wake. Dhamana na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni kumfanya Kristo aweze kufahamika na wengi sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia tunu msingi za Ufalme wa Mungu. Rej. Mdo 3:6. Kuna uhusiano wa karibu zaidi kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikan, hasa kutokana na ujasiri wa Papa Gregory Mkuu aliyemtuma Mtakatifu Augustino kama mmisionari mahiri nchini Uingereza. Khalifa wa Mtakatifu Petro ni Mtumishi wa watumishi wa Mungu “Servus servorum Dei.”, kielelezo cha madaraka na huduma, changamoto na mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene katika hali ya utulivu katika tema ya “Askofu mkuu wa Roma. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa matokeo mazuri ambayo yamekwisha kufikiwa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikan kwani Ukulu wa Askofu wa Jimbo kuu la Roma ni zawadi ya kushirikishana. Baba Mtakatifu amekaza kusema, Kanisa Katoliki liko katika mchakato wa Madhimisho ya Sinodi yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Umoja na ushuhuda wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.
Umoja na ushuhuda wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.

Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Baba Mtakatifu anampongeza Askofu mkuu Justin Welby kwa kushiriki katika mkesha wa ufunguzi wa kiekumene wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, mwezi Oktoba, 2023. Dhamana na utume wa Askofu wa Roma ni kati ya matunda yanayotarajiwa na Kanisa baada ya maadhimisho ya Sinodi. Tamko la Pamoja kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikan, lilihimiza umuhimu wa kukoleza majadiliano ya kiekumene, kwa kujiaminisha chini ya neema ya Mungu na Roho Mtakatifu, ili aweze kuwafungulia malango ya maarifa ili kuutambua ukweli, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa na kwamba, upendo na unyenyekevu; huduma makini kwa watu wa Mungu ni mambo msingi yatakayowezesha kukamilisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Ni fadhila ya upendo itakayowaunganisha pamoja kama ndugu wamoja na miundo mbinu itakuja baadaye.

Kanisa Anglikan
02 May 2024, 13:35