Tafuta

Alhamisi tarehe 4 Aprili 2024 Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Alhamisi tarehe 4 Aprili 2024 Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Umuhimu wa Majadiliano ya Kidini: Kuthamini Tofauti, Kutunza Mazingira na Kulinda Amani

Alhamisi tarehe 4 Aprili 2024 Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amejikita katika mambo makuu yafuatayo: Umuhimu wa kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zilizopo; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kulinda na kudumisha amani. Huu ni wito wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yasaidie kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni sehemu ya hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa sanjari na ujenzi wa siasa ya amani duniani inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, majadiliano pamoja na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa iwekeze katika uchumi fungamani unaojali na kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake!

Hija ya Kichungaji nchini Kazakhstan 13-15 Septemba 2022
Hija ya Kichungaji nchini Kazakhstan 13-15 Septemba 2022

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alishiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililoadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Kongamano hili lilinogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hili ni Jukwaa lililowaleta pamoja viongozi wa kidini, kisiasa, kitamaduni na wale walioko kwenye tasnia ya mawasiliano ya jamii. Hizi ni juhudi zinazopaswa kukumbukwa na kuheshimiwa, kwa kuiheshimisha Kazakhstan kuwa ni nchi ya kuwakutananisha watu. Ilikuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Kazakhstan pamoja na kukutana na hatimaye, kuzungumza na viongozi wa Kazakhstan.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Alhamisi tarehe 4 Aprili 2024 Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amejikita katika mambo makuu yafuatayo: Umuhimu wa kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zilizopo; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kulinda na kudumisha amani. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa viongozi wa kidini kusimama kidete kulinda, kuendeleza na kukuza amani kati ya dini, makabila na tamaduni mbalimbali. Heshima kwa tofauti msingi ni kikolezo cha demokrasia na maridhiano, ikiwa kama serikali ni ya kisekulari; Serikali inayotenganisha kati ya dini na siasa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya pande zote mbili; Serikali inayotambua dhamana na mchango wa dini katika jamii kwa ajili ya huduma na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amani na utulivu wa kijamii, usawa wa kikabila, kidini na kitamaduni ni muhimu katika kuhakikisha kwamba, nafasi za ajira zinapatikana kwa wote, sanjari na kuruhusu raia kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na kijamii, ili kamwe asiwepo mtu anayejisikia kwamba anatengwa au anapendelewa kutokana na hali pamoja na utambulisho wake.

Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana
Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana

Baba Mtakatifu anasema, ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” ni nyaraka zinazozungumzia utunzaji bora wa mazingira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani. Ni nyaraka ambazo zimetumiwa pia katika “Hati ya Dhana ya Maendeleo Kwa Mwaka 2023-20233” iliyotungwa nchini Kazakhstan kwa kuweka mkazo wa pekee kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuonesha upendo kwa kazi ya Uumbaji, amana na urithi mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya, mchango wa pekee katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha amani kwa nyakati hizi, sauti nyingi zinazosikika ni kuhusu vita na mirindimo ya silaha za kivita, limekuwa ni jambo la kawaida masikioni mwa wengi. Kuna chuki na uhasama unaoendelea kupandikizwa na watu wengi wanaendelea kupoteza maisha kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kumbe, kuna haja ya watu kuanza kuzungumzia amani, kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi ni mfano bora wa kuigwa, kama sehemu ya mchakato wa kutajirishana, kwa kuheshimiana kama zawadi na kikolezo cha ukuaji wa pamoja. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia ujenzi mwema wa udugu wa kibinadamu, urafiki wa kijamii, ustawi na maendeleo na kwamba, waendelee kushirikishana matunda ya kazi zao.

Majadiliano ya kidini
04 April 2024, 14:51