Tafuta

Katika muktadha wa Maadhimisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sanjari na Sikukuu ya 'Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D., Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetuma ujumbe wa salam na heri kwa Waislam duniani kote. Katika muktadha wa Maadhimisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sanjari na Sikukuu ya 'Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D., Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetuma ujumbe wa salam na heri kwa Waislam duniani kote. 

Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya Eid El Fitr 1445H./2024: Amani

Katika muktadha wa Maadhimisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sanjari na Sikukuu ya 'Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D., Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetuma ujumbe wa salam na heri kwa Waislam duniani kote, unaonogeshwa na kauli mbiu: “Wakristo na Waislamu: Zima Moto wa Vita na Washa Mshumaa wa Amani.” Ujumbe unakazia umuhimu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Imani, amani na matumaini ni fadhila ambazo zinapata chanzo na utimilifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini binadamu amedhaminishwa tunu hizi ili kuzifanyia kazi katika maisha yake hapa duniani; kwa kuchagua na kuambata mapenzi ya Mungu, ili hatimaye, aweze kusimama kidete kulinda na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kujichotea: hekima, amana na utajiri kutoka katika Vitabu vitakatifu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, majadiliano ya kidini yataweza kuzaa matunda mengi ya ushirikiano na mshikamano sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Hija ya pamoja katika majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya waamini wa dini mbalimbali ili kuweza: Kufahamiana, kuheshimiana na kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Huu ni mchakato wa ujenzi wa fadhila ya upendo wa kidugu kati ya watu kwani Mungu ni asili na hitimisho la upendo. Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbalimbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya upendo kwa Mungu na jirani. Kizazi baada ya kizazi kinapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapaswa kupendwa kwa moyo wote, kwa roho yote na kwa nguvu zote. Upendo huu kimsingi, unapaswa pia kuelekezwa kwa jirani ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ujumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa
Ujumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya chuki na uhasama; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya: haki, amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Waamini wa dini mbalimbali wanao wajibu na dhamana ya kulinda uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini pamoja na kujikita katika mchakato wa kutunza mazingira nyumba ya wote! Katika muktadha wa Maadhimisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani sanjari na Sikukuu ya 'Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D.”, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetuma ujumbe wa salam na heri kwa Waislam duniani kote, unaonogeshwa na kauli mbiu: “Wakristo na Waislamu: Zima Moto wa Vita na Washa Mshumaa wa Amani.” Katika ujumbe huu, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linakazia umuhimu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na waamini wa dini hizi mbili kuendelea kujielekeza zaidi katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kuna sababu msingi za kutaka kuyatawala Mataifa mengine, sababu za kisiasa, kijiografia na kiuchumi, lakini sababu kubwa ni kuendelea kushamiri kwa biashara haramu ya silaha ulimwenguni kutokana na faida kubwa, lakini kwa gharama ya damu ya watu wasiokuwa na hatia. Ikumbukwe kwamba, haki, amani na usalama ni mambo ambayo yamekita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo za watu wenye mapenzi mema. Madhara ya vita sehemu mbalimbali za dunia yanaonekana na wengi: vifo, uharibifu wa miundo mbinu na mazingira sanjari na uzalishaji wa wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Hakuna vita vitakatifu, isipokuwa amani peke yake ndiyo takatifu.

Wakristo na Waislam washa mshumaa wa amani
Wakristo na Waislam washa mshumaa wa amani

Dini nyingi duniani zinatangaza na kusimamia ukweli kwamba, maisha ya kila mtu ni matakatifu yanapaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa na kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa kwa kukataa vita na kuenzi amani duniani. Mwenyezi Mungu ndiye asili ya maisha na amani na kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini wakati mwingine inamshirikisha na kumwajibisha mwanadamu, ili kuhakikisha kwamba, anaunda na kujenga mazingira ya amani. Wakristo na Waislam, kwa pamoja wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni wajumbe wa matumaini na amani, tayari kushirikiana kuwasha mshumaa kielelezo cha amani. Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hatimaye, maadhimisho ya Sikukuu ya ya 'Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D., yawe ni chemchemi amani, matumaini na furaha. Itakumbukwa kwamba, katika dini ya Kiislamu, kuna nguzo kuu tano ambazo ni muhimu katika imani yao, nazo ni: Shahada (kukiri Imani), Sala, Zakat, Sawm, na Hija. Kalenda ya dini ya Kiislamu inaanza baaada ya Hija ya Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam – amani iwe kwake) kutoka Mecca kwenda Medina mwaka 622 AD na kuanzisha jumuiya ya kwanza ya Kiislamu (Ummah). Huo ndio mwaka mpya wa Kiislamu 622 (Anno Hegirae AH). Kwa hiyo kalenda ya dini ya Kiislamu inajulikana kama Hijri au Lunar kwa vile inafuata mwandamo wa Mwezi. Hii ndiyo inayotumika katika matukio ya imani na tamaduni zao, kama sikukuu na mfungo. Ramadhani inatokana na neno la Kiarabu “ان‎, Ramida au ar-ramad” likimaanisha, ukavu. Ramadhani ni kati ya miezi muhimu sana katika dini ya Kiislamu. Ramadhani ni mwezi mtukufu kwa waamini wa dini ya Kiislam kwa sababu ni katika mwezi huu Mungu (Allah) alimpa Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam) sura ya kwanza ya Kuruani Tukufu mwaka 610. Sura hiyo al fatihah yaani ufunguzi, inasomwa yote katika kila sala kwa mwamini wa dini ya Kiislam. Hivyo ni maarufu kama Mama wa Kitabu au Mama wa Kuruani (Umm al Kitabu au umm al kuruani).

Nyumba ya Mungu
Nyumba ya Mungu

Hii ni Sura inayomwalika mwamini wa dini ya Kiislam kutambua Ukuu wa Mungu muweza wa yote, kuomba ulinzi na huruma yake na kuendelea kumsifu. Ramadhani ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya dini ya Kiislamu, ambapo Waislamu wanaalikwa kufunga, kuacha anasa na kusali zaidi ili kuwa karibu na Mwenyezi Mungu (Allah). Japo Waislamu wanasali kila siku tena mara tano inaaminika sala katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inabeba uzito zaidi, kwa kuwa ni katika mwezi huu Mtume alikutana na Allah. Ramadhani inaanza rasmi baada ya kiongozi wa dini kutangaza kuona mwezi mpya. Hiki ni kipindi kwa Waislamu cha kusoma Kuruani, kutafakari na kukua kiroho yaani kupata thawabu. Sala ya usiku katika kipindi hiki kadiri ya ahadi ya Mwenyezi Mungu anayeisali kwa imani na kuomba rehema, dhambi zake za nyuma zote zitafutwa. Ramadhani ni kipindi cha kujenga umoja kwa kuonesha mshikamano kwa Waislamu wote duniani kwa njia ya mfungo na sala. Kufunga ni nguzo ya nne ya imani ya dini ya Kiislamu. Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwamini wa dini ya Kiislam anapaswa kufunga, kuacha chakula na maji kuanzia jua linapochomoka mpaka linapozama. Kwa tamaduni mfungo huvunjwa kwa maji na tende jua linapozama, mlo wa kuvunja mfungo unaitwa iftar (futari). Mfungo unawakumbusha Waislamu kwamba, mtu siyo mwili tu bali roho pia. Ramadhani ni kipindi cha Waislamu kutoa huduma kwa jamii mfano kusaidia maskini na kushirikishana kile walichojaliwa na wahitaji. Wanaalikwa kuadhimisha kila Ramadhani kwa uadilifu kama ndio ya mwisho kwa kila mwamini, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwasamehe maovu waliyotenda. Ili mfungo ufanikiwe ni lazima kuweka "niyyah" na kufuata sheria za mfungo (Surat Al-Baqarah, aya 183). Kama mwamini ambaye amevunja mfungo mfano wanawake kwenye siku zao basi inabidi kulipizia baada ya kumaliza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sikukuu ya Eid El Fitr
Sikukuu ya Eid El Fitr

Mwezi wa tisa katika Kalenda ya dini ya Kiislamu unajulikana kama mwezi wa Ramadhani au Ramazan. Mwezi huu mtukufu unaadhimishwa kama mwezi wa mfungo wa waamini wa dini ya Kiislam. Kushika saumu katika mwezi huu kunachukuliwa kuwa moja ya nguzo tano za dini ya Kiislam. Kuanzia mwezi mpevu unapoonekana kwa mara ya kwanza hadi siku inayofuata, sherehe za Ramadhani Kareem hudumu kwa takriban siku 29 au 30. Mwezi huu mtukufu kimsingi ni mfano wa nidhamu ya kibinafsi ambapo watu sio tu kwamba wanakata tamaa ya maji na chakula lakini pia hutumia wakati huu kuzama zaidi katika sala, matendo mema, hisani na huduma za jamii ambazo kimsingi huwasogeza waamini karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Mwezi mtukufu wa Ramadhan ukizingatiwa kuwa nguzo ya nne ya dini ya Kiislam umejengwa juu ya kanuni kama vile kujirekebisha, utakaso wa mawazo, kuwasaidia wenye shida na kupyaisha imani. Kwa mujibu wa Quran tukufu, huu ni mwezi wa maana sana kwani Mtume Mohammad alipokea aya za kwanza za Maandiko Matukufu. Kwa hiyo, mwezi huu unatajwa kuwa wakati muafaka wa kufunga na kusali kwa bidii na shauku kubwa. Kwa mujibu wa dini ya Kiislam, matendo mema yanayotekelezwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani huleta ustawi na mafanikio. Pia, inaaminika kuwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, milango ya mbinguni hufunguliwa na mashetani hufungwa minyororo.

Eid El Fitr 2024

 

10 April 2024, 16:55