Tafuta

Mwadhama Kardinali Ángel Fernández Artime, tarehe 20 Aprili 2024 amewekwa wakfu kuwa Askofu. Mwadhama Kardinali Ángel Fernández Artime, tarehe 20 Aprili 2024 amewekwa wakfu kuwa Askofu. 

Mwadhama Kardinali Ángel Fernández Artime: Awekwa Wakfu Kuwa Askofu

Askofu ana wajibu na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji mkuu anayeunda na kuliongoza Kanisa; Kristo Yesu ndiye nguzo na mhimili mkuu wa Kanisa lake. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mipango ya Kristo mchungaji mwema. Mwadhama Kardinali Ángel Fernández Artime: Awekwa Wakfu Kuwa Askofu

Na Padre Philemon Chacha, SDB, - Vatican.

Askofu ana wajibu na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji mkuu anayeunda na kuliongoza Kanisa; Kristo Yesu ndiye nguzo na mhimili mkuu wa Kanisa lake. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mipango ya Kristo mchungaji mwema. Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Uwepo wa karibu wa Mungu ni chemchemi ya utume wa Askofu kama unavyofunuliwa katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo makini cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Ili kuonja ukaribu wa Mungu kuna umuhimu wa kupata mang’amuzi ya wema, huruma na upendo kwa waja wake. Maaskofu wajenge utamaduni wa kusali na kutafakari mbele ya Kristo Yesu, ili kuwawezesha kuishi kati ya watu wa Mungu. Katika shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kiaskofu, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kukimbilia katika sala na tafakari, ili kujenga tena: imani na matumaini mapya, kwa kumtegemea na kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Ukaribu wa Mungu unajionesha kati ya watu wake kwa njia ya utambulisho wa Maaskofu, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kama sadaka safi inayotolewa Altareni. Maaskofu ni mkate unaomegwa kwa ajili ya maisha ya ulimwengu. Kristo Yesu anataka kuwa kati pamoja na watu wake kwa njia ya Maaskofu. Ukaribu wa Mungu unajionesha katika Neno na maadhimisho ya Mafumbo mbalimbali ya Kanisa. Lakini zaidi, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kupenda bila kujibakiza pamoja na kuendelea kujizamisha katika huruma na upendo wa Mungu.

Maaskofu wanaitwa na kutumwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu
Maaskofu wanaitwa na kutumwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuonesha ukaribu wa Mungu kwa waja wake kwa kujitosa kimaso maso katika huduma ya upendo kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, ili waweze kuona, kusikiliza na kujibu kwa vitendo kilio na mahangaiko ya watu wa Mungu kama alivyofanya yule Msamaria mwema: Alipomwona, alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai na hatimaye, akamtunza. Haya ni maneno msingi katika maisha na utume wa Askofu anayetembea bega kwa bega na watu wake, tayari kushirikishana nao mateso na matumaini ya maisha. Maaskofu wawe na ujasiri wa kutekeleza dhamana, wajibu na utume wao bila ya kuogopa. Makanisa yao, yawe ni alama na utambulisho wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Kipimo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake ni huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kumezwa na malimwengu. Maaskofu waguswe na umaskini pamoja na mahangaiko ya watu wao, ili kuinua na kusimamia utu, heshima na haki zao msingi. Maaskofu wawe karibu zaidi na watu wao, ili waweze kusikiliza mapigo ya nyoyo zao. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Maaskofu watembelee Parokia na waamini wao, ili kuwapelekea faraja, imani, matumaini na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu waoneshe ukaribu wa Mungu kwa mapadre wao, kwa kuwakumbatia, kuwashukuru na kuwapongeza kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Maaskofu wawapende na kuwaheshimu Mapadre wao; wawafuatilie na kuwatia shime, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo makubwa zaidi.

Urithi wa Kitume juu ya amana na utajiri wa Maaskofu
Urithi wa Kitume juu ya amana na utajiri wa Maaskofu

Ni katika muktadha huu, Jumamosi Tarehe 20 Aprili 2024, familia ya Wasalesiani na Kanisa kwa ujumla lilishuhudia wana wawili wa Mtakatifu Yohane Bosco wakipata Daraja Takatifu ya Uaskofu. Kardinali Ángel Fernández Artime, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani ulimwenguni na Askofu Mkuu mteule wa Ursona, Pamoja na Askofu Mkuu Giordano Piccinotti, Askofu Mkuu mteule wa Gradisca na Raisi wa Rais wa Utawala wa Mali nchini Vaticani. Maadhimisho haya yalifanyika katika Kanisa kuu la kipapa la Maria Major kuanzia majira ya saa tisa na nusu mchana. Mwadhimishaji Mkuu wa Ibada ya kuwaweka wakfu mapadre hawa kuwa maaskofu alikuwa Mwadhama Kardinali Emil Paul Tscherrig, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Italia na Jamhuri ya San Marino, pembeni yake alisaidinana na Kardinali Cristóbal López Romero, SDB, Askofu Mkuu wa Rabat, Morocco; na Mons. Lucas Van Looy, SDB, Askofu Mstaafu wa Ghent, Ubelgiji. Pamoja nao tulishuhudia Idadi kubwa ya viongozi wa Kanisa, makardinali na baaadhi ya wakuu wa idara mbalimbali nchini Vatican, na wageni muhimu walishiriki katika Ibada ya Ekaristi, Pamoja nao Halmashauri Kuu ya Kiongozi Mkuu wa Shirika, baadhi ya wakuu wa Kanda za Shirika kutoka sehemu mbalimbali duniani, mapadri, wawakilishi wa familia ya wasaleisani, familia za Mapadri Wapya waliowekwa wakfu, marafiki, wafadhili, wakiungana na wageni maalum wa kiserikali.

Wasalesian wa Don Bosco wakiwa na Maaskofu wapya.
Wasalesian wa Don Bosco wakiwa na Maaskofu wapya.

Mwadhama Kardinali Emil Paul Tscherrig, katika mahubiri yake yaliyojaa tafakari nzito, alikazia mambo muhimu huku akieleza chimbuko na jukumu la Maaskofu, "Tumekusanyika hapa kusherehekea moja ya miujiza mikubwa zaidi ya Kanisa: Urithi wa Mitume. Tangu wakati wa Mitume, urithi huu umekuwa ukiendelea kwa kuwekewa mikono na kuomba Roho Mtakatifu. Neema ya Huduma ya Uaskofu imekuwa ikipitishwa daima kutoka kwa askofu mmoja hadi mwingine, na urithi huu usiovunjika unaendelea hadi leo.” Hivyo ni wazi kuwa Maaskofu wanatenda na kutekeleza wajibu huu kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Na hivyo wamepewa jukumu la kufundisha imani, maadili na utu wema, huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Akimnukuu Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Tscherrig alisema, "Kuwa Askofu kunamaanisha kuchagua kuwa shuhuda wa kweli wa Kiinjili, uchaguzi ambao una uwezo wa kubadilisha kila kitu." Alihimiza kwamba wale wanaokubali jukumu la kuwa wachungaji katika kundi la Kristo wanapaswa kujifunza kuona na kuwaangalia watu kwa macho ya Kristo, kufikiri kama Yeye, na kupenda kama Yeye.

Maaskofu wanaitwa na kutumwa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza
Maaskofu wanaitwa na kutumwa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza

Akimnukuu tena Baba Mtakatifu Francisko, alisema, "Maisha hukua kwa kujitoa yenyewe, na hudhoofika kwa kujitenga, kuishi kwa kuridhika na starehe. Kwa njia hii, wale wanaofurahia maisha zaidi ni wale wanaokuwa na hamu ya kutangaza uzima na maisha kwa wengine." Kardinali Tscherrig alimalizia kwa kukazia kwamba urithi wa Askofu si heshima au nguvu, bali ni Mungu pekee. Mchungaji mwema hutoa maisha yake kwa kundi, akifuata mfano wa Yesu Kristo, hivyo Maaskofu hawa wapya wanaitwa kumwiga Yeye kabisa. Naye Mwadhama Kardinali Ángel Fernández Artime, katika neno lake la shukrani aliweza kuwashukuru watu na makundi mbalimbali lakini kwa namna ya pekee alimshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumuamini na kumpatia jukumu la Uaskofu. Aliendelea kukazia na kusema kwamba upo umoja na ushirikiano thabiti kati ya Wasalesiani na Kanisa kwa ujumla chini ya Khalifa wa Mtakatifu Pietro. Ushirikiano huu unatokana moja kwa moja na Don Bosco mwenyewe. Don Bosco kwa unyenyekevu na uhakika mkubwa, alitamka kwamba wataendelea kutumikia Kanisa na watu wake, hasa maskini.

Mapadre wakishiriki katika Ibada ya Misa takatifu
Mapadre wakishiriki katika Ibada ya Misa takatifu

Itakumbukwa kwamba Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateua Makardinali wapya 21 kati yao alikuwepo Kardinali Ángel Fernández Artime, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani ulimwenguni. Makardinali wapya walisimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Baada ya Daraja hili ya Uaskofu, Baba Mtakatifu ameridhia kuwa Kardinali Angel, ataenedelea kuwa Mkuu wa Shirika la Wasalesiani mpaka mwezi Agosti 2024, ndipo Baba Mtakatifu Francisko atakapompangia majukumu mapya. Wakati huo Msaidizi wa Mkuu wa Shirika ulimwenguni Padri Stefano Martoglio ndiye atakayeshikilia wadhifa huo mpaka Februari 2025 wakati Shirika litakapokuwa na Mkutano wake Mkuu wa 29 unaobeba kauli mbiu: SHAUKU KWA YESU KRISTO, KUJITOA KWA VIJANA. Kusimikwa kwa Maaskofu hawa ambao ni wana wa Mtakatifu Yohane Bosco ni furaha kwa familia nzima ya wasalesiani ulimwenguni na Kanisa kwa ujumla. Tunaalikwa kumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya Maaskofu wapya ndani ya Kanisa, tuendelee kuwaombea ili waweze kutimiza majukumu yao vyema hasa katika kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu.

Daraja ya Uaskofu
25 April 2024, 15:49