Tafuta

Mapadre wapya kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma. Mapadre wapya kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma. 

Mapadre Ni Wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa

Ni katika muktadha wa mkesha wa Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024, Kardinali Angelo De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Papa Francisko anasema, hii ni amana na utajiri mkubwa wa Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu watu walioko safarini mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Sala kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 anasema sala ndiyo nguvu na ufunguo wa malango ya matumaini. Waamini ni mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani na kwamba, lengo kuu la safari ya maisha ni kuishi kwa haki, amani na upendo na kwamba, lengo na wito ni kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; umoja, amani na udugu. Kila mwamini ajitahidi kugundua wito wake sahihi katika Kanisa na Ulimwengu, kwa kuwa hujaji wa matumaini na wajenzi wa amani.

Mapadre ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa
Mapadre ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa

Wakati huo huo, Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa Kipindi cha Kwaresima cha mwaka 2011 ulinogeshwa na kauli mbiu "aliye mkubwa na awe mtumishi." Mt. 20:26. Msingi wa utumishi wa Wahudumu wa Daraja Takatifu, ni Kristo Yesu mwenyewe aliyekuja kutumika na kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengi. Ekaristi Takatifu wanayoiadhimisha kila siku iwakumbushe kwamba, “chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa hukaa hali iyo peke; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yn 12:24). Kristo ndiye chembe ya ngano ya Mungu na kutoka kwa Mungu ameshuka katika ulimwengu. Padri anapoadhimisha Ekaristi Takatifu, anagusa kwa mikono yake Mkate wa ngano ya Mungu ambaye ndiye Kristo Yesu mwenyewe, ambaye kutokana na kifo chake, chembe ya ngano imekuwa mkate kwa ajili ya ulimwengu mzima. Kwa hiyo, kwa mhudumu wa Daraja Takatifu, Ekaristi Takatifu, licha ya kuwa ishara kuu ya mavuno, furaha ya karamu ya harusi ambako watakuja wengi kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini (taz. Mt 8:11), vile vile ni ishara ya Msalaba, kiwango cha juu kabisa cha utumishi.

Mapadre wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu
Mapadre wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu

Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha jinsi kuhani anavyopaswa kuwa chembe ya ngano ya Mungu. Hapaswi tu kuridhika kutoa maneno na matendo ya nje, bali anapaswa kujibidisha katika maisha yake, akijitoa kwa kutumikia mpaka tone la damu. Wahudumu wa Daraja Takatifu wawajibike, awali ya yote, kuihubiri Injili ya Mungu kwa watu wote wakiushika utume wa Bwana asemapo: “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe” (taz. Mk 16:15). Watu wote wanayo haki ya kulitafuta Neno la Mungu kutoka midomoni mwa mhudumu wa Daraja Takatifu ambaye anapaswa kulihubiri wakati ufaao na wakati usiofaa (taz. 2Tim 4:2). Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema kwamba, Mapadri wanaitwa na kuwekwa wakfu ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza… na watende kazi kama wahudumu wa Yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu kwa njia ya Roho wake. Wahudumu wa Daraja Takatifu wamepewa mamlaka ya kutoa huduma hii bila ya mastahili yao na tena wamepewa bure (Mt 10:8.)

Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, wanamshukuru Kard. De Donatis
Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, wanamshukuru Kard. De Donatis

Kwa hiyo, wahudumu wa Daraja Takatifu wanapaswa kutoa huduma yao ya utumishi kwa bidii na kwa nguvu zao zote bila masharti wala ubaguzi. Hata hivyo, kwa namna ya pekee, wamekabidhiwa hasa walio maskini na wanyonge zaidi. Ni vizuri viongozi wa Daraja Takatifu wakatafakari namna na jinsi wanavyotekeleza agizo hilo. Namna wanavyotoa huduma za kichungaji katika Jumuiya, Kigango, Parokia na pengine hata nje ya majimbo yao. Ni aina gani ya watu wanaokuwa nao karibu zaidi? Je? Maskini na wanyonge wanayo nafasi mioyoni mwao? Wahudumu wa Daraja Takatifu, inabidi wawe tayari kila wakati kutafuta siyo mapenzi yao binafsi, bali mapenzi ya yule aliyewatuma (taz. Yn 4:34; 5: 30; 6:38.) Kazi ya Kimungu ambayo walichukuliwa na Roho Mtakatifu kwayo, inapita nguvu na uwezo pia hekima ya wanadamu; kwa sababu: “Mungu alivichagua vitu vidhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu” (1Kor 1:27.) Kwa hiyo, mhudumu wa Daraja Takatifu anapaswa kutambua udhaifu wake na kufanya kazi kwa unyenyekevu, akijihakiki ni nini impendezayo Bwana na, hali amefungwa na Roho, anaongozwa katika yote na mapenzi yake yule anayetaka watu wote waokolewe; nayo mapenzi ya Mungu ataweza kuyagundua na kuyafuata katika mambo ya kila siku akiwatumikia kwa unyenyevu wote waliokabidhiwa kwake na Mungu kutokana na dhima anayotakiwa kutekeleza, na matukio mbalimbali ya maisha yake.

Mapadre ni: Makuhani, Wafalme na Manabii
Mapadre ni: Makuhani, Wafalme na Manabii

Kimsingi Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo! Ni katika muktadha wa mkesha wa Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024, Kardinali Angelo De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ilikuwa ni nafasi yake ya kuagana na watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma baada ya Baba Mtakatifu hivi karibuni kumteuwa kuwa Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume “Paenitentiaria Apostolica.”

Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma wanampongeza Kard. De Donatis
Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma wanampongeza Kard. De Donatis

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malkia wa mbingu, Dominika tarehe 21 Aprili 2024, akigusia kuhusu maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mtakatifu ndani ya Kanisa yaliyonogeshwa na kauli mbiu  “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani” amesema kwamba, hii ni fursa ya kugundua tena amana na utajiri mkubwa unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa wingi wa karama kwa ajili ya huduma ya Injili. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kuwapongeza Mapadre wapya waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Roma na amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza Mapadre wapya kwa sala na sadaka zao. Kardinali Angelo De Donatis ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa urafiki katika huduma, iliyomwezesha kupata mang’amuzi mapana ya maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Roma. Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma wamemshukuru na kumpongeza Kardinali Angelo De Donatis kwani tangu alipowekwa wakfu kuwa Padre amekuwa ni mwanga angavu wa upendo wa Mungu katika malezi na huduma parokiani, kama Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma na hatimaye, kama Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Kwa hakika amekuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu.

Mapadre Wapya Roma
23 April 2024, 17:27