Tafuta

Huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu.  

Maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu: Ujumbe wa Mt. Sr. Faustina Kowalska: Huruma

Huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo. Huu ndio ujumbe katika maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini kurejea tena kwenye ujumbe wa huruma ya Mungu kama ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo.

Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka!
Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 3 Aprili 2024 anasema huu ndio ujumbe makini katika maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu, mwaliko kwa watu wa Mungu kurejea tena kwenye ujumbe wa huruma ya Mungu kama ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma. Ni mwaliko wa kuombea haki na amani ya kudumu sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2020 alisema, Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, alijitahidi kuwafunulia watu, huruma na upendo wa Mungu, kama Kristo Yesu alivyomfunulia Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma. Mwaka 1993 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na mwaka 2000 akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mtakatifu. Ni mtakatifu anayependwa na wengi kutokana na jitihada zake za kukuza na kueneza: Tasaufi na Ibada ya Huruma ya Mungu, chemchemi ya upendo wa Mungu kwa waja wake. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, aliwaonesha walimwengu jinsi ya kutafuta wokovu kwa njia ya huruma ya Mungu, Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska anasema huu ni wakati wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa sababu rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha!

Dominika ya Huruma ya Mungu
Dominika ya Huruma ya Mungu

Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” anatafakari kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu wote na kwamba, kazi hii inatoa mwangwi wake kwenye maisha ya kiroho yanayosimuliwa na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, Bikira, ambaye kwa njia ya zawadi kubwa kutoka mbinguni, alibahatika kukutana na Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu Baba na akawa shuhuda na chombo cha kutangaza na kueneza Ibada ya Huruma ya Mungu. Mtakatifu Faustina alizaliwa Głogowiec, karibu na mji wa Łódź, nchini Poland kunako mwaka 1905 na kufariki dunia huko Cracovia kunako mwaka 1938. Mtakatifu Faustina alibahatika kuishi katika Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma kwa muda mfupi. Alionesha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wito na zawadi mbalimbali za maisha ya kiroho, akajitahidi kuishi kwa uaminifu mkubwa kwa zawadi zote hizi. Katika Shajara ya moyo wake, Madhabahu ambayo aliyatumia kukutana na Kristo Yesu, mwenyewe anasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomwezesha kwa ajili ya faida ya watu wengi zaidi. Kwa kumsikiliza Kristo Yesu ambaye ni Upendo na Huruma aliweza kutambua kwamba, hakuna dhambi yoyote ya binadamu ambayo ingeweza kushinda huruma ya Kristo inayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu. Na tangu wakati huo, akawa ni muasisi wa Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo leo hii imeenea sehemu mbalimbali za dunia. Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu, wakati wa Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Huruma ya Mungu imefunuliwa katika Kiti cha Maungamo.
Huruma ya Mungu imefunuliwa katika Kiti cha Maungamo.

Tokea hapo, Jina la Mtakatifu Faustina likapata umaarufu wa ajabu kutoka sehemu mbali mbali za dunia mwitikio wa kutangaza na kushuhudia Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo imeleta mageuzi makubwa katika maisha ya waamini. Ni kutokana na muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na baada ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu amana na utajiri wa maisha ya Mtakatifu Faustina, ameridhia na kutamka kwamba: Mtakatifu Maria Faustina (Helena) Kowalska, Bikira aingizwe kwenye Kalenda ya Kirumi na atakuwa anakumbukwa na waamini wote tarehe 5 Oktoba ya kila mwaka, kama Kumbukumbu ya Hiyari.

Huruma ya Mungu
04 April 2024, 15:16