Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 70 ya Chama Cha Skauti ya Wakatoliki Italia: Injili ya Uhai

Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI, kinaadhimisha kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuasisiwa kwake kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maisha zaidi kwa ajili ya maisha”: “Più vita alla vita.” Changamoto na mwaliko wa kushughulikia Injili ya uhai hadi ukamilifu wake. Vifaa tiba kwa ajili ya kituo cha huduma ya kwanza na mapokezi cha Lampedusa; Ujenzi wa Kituo cha Useremala kwa ajili ya ujenzi wa boti Zambia na huoteshaji wa misitu huko Argenta na Romagna.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI, “Movimento Adulti Scout Cattolici Italiani” kilianzishwa na Mario Mazza pamoja na Padre Ruggi D’Aragona kunako tarehe 20 Juni 1954. Lakini Chama cha “Knights of St. George” kilikuwepo kwa takribani muongo mmoja kwa lengo la kutoa ushuhuda wa mambo msingi katika kanuni, sheria na taratibu za Skauti maishani. Kanuni hizi zikafafanuliwa kwa ufasaha zaidi mintarafu kanuni maadili na utu wema; mambo msingi ambayo Chama cha Skauti ni warithi, walezi na waendelezaji katika ulimwengu mamboleo hususan katika masuala ya: kijamii, elimu, huduma na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni katika muktadha huu, Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI, kinaadhimisha kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuasisiwa kwake kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maisha zaidi kwa ajili ya maisha”: “Più vita alla vita.” Changamoto na mwaliko wa kushughulikia Injili ya uhai hadi ukamilifu wake. Ni katika maadhimisho haya kwa vitendo, Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI, kimetoa vifaa tiba kwa Kituo cha Huduma ya Kwanza na Mapokezi cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia; Ujenzi wa Kituo Useremala kwa ajili ya ujenzi wa boti nchini Zambia pamoja na kuotesha misitu huko Argenta na Romagna, matukio ambayo yanabeba kumbukumbu hai pamoja na tunu msingi za maisha ya kijamii.

Kumbukizi ya Miaka 70 ya Chama cha Skauti ya Wakatoliki Italia
Kumbukizi ya Miaka 70 ya Chama cha Skauti ya Wakatoliki Italia

Umri wa wastani wa maisha ya raia wa Italia ni kati ya miaka 46 na umri wa wastani wa mtu kuishi kutoka Albania ni umri wa miaka 23. Kuna changamoto kubwa kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia, ikilinganishwa na idadi ya watu wenye umri mkubwa, hali inayoonesha kwamba, binadamu amesahau dhamana na wajibu wa kuwahudumia watu wengine pengine hata kupoteza ladha ya maisha. Upendo kati ya Bwana na Bibi hauna budi kulindwa na kudumishwa kwani hapa ni mahali patakatifu ambapo uhai wa mwanadamu unapata chimbuko lake, tayari kushiriki katika kazi ya uumbaji, ambayo Mwenyezi Mungu amemdhamisha mwanadamu. Familia kadiri ya mpango wa Mungu haina budi kukuzwa na kudumishwa, kwa kuwasaidia na kuwasindikiza wanandoa watarajiwa na wanandoa wapya katika hija ya maisha yao, wanapojitahidi kujenga familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Kumbe, msaada wa vifaa tiba kwa Kituo cha Huduma ya Kwanza na Mapokezi cha Lampedusa ni muhimu sana kama kielelezo cha upendo kwa ajili ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; uhai ambao unatamaniwa na wengi. Hii ni sehemu ya tafakari ya kina kuhusu maisha yanayozaliwa, kama ilivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Aprili 2024 alipokutana na kuzungumza na Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI, “Movimento Adulti Scout Cattolici Italiani” kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.

Kauli mbiu: Maisha zaidi kwa ajili ya maisha
Kauli mbiu: Maisha zaidi kwa ajili ya maisha

Ujenzi wa Kituo Useremala kwa ajili ya utengenezaji wa boti nchini Zambia, kwa Wakristo hiki ni kielelezo cha cha uchaguzi ambao Mwana wa Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, alijiandalia mahali pa kutekeleza utume wake kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Mwana wa Mungu alifanya kazi kwa mikono ya kibinadamu. Leo hii, kitega uchumi kinachozalisha faida kubwa ulimwenguni ni utengenezaji na biashara ya silaha. Hii ni changamoto kwa binadamu kurejea tena katika wito wake wa asili, ili kuhakikisha kwamba, zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa amani, usawa na udugu wa kibinadamu, mwaliko kwa binadamu kufanya kazi kwa ajili ya utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huoteshaji wa misitu huko Argenta na Romagna unawakumbusha binadamu dhamana na wajibu wao wa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote, tabia pekee ya Skauti tangu kuanzishwa kwake, changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kukosekana na ugawaji mzuri wa rasilimali za dunia. Katika muktadha huu, Chama cha Skauti ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kuheshimu ikolojia, jambo ambalo litasaidia kupata njia ya kiikolojia ambayo inajali nafasi ya pekee ya wanadamu humu duniani na uhusiano wake na mazingira anamoishi. Re. Laudato si, 15. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekitaka Chama cha Skauti ya Wakatoliki wa Italia, MASCI, kutembea kwa pamoja sanjari na ujenzi wa jumuiya ambayo iko wazi, tayari kupokea, kusikiliza na kuwasindikiza wale wote wanaokutana nao katika njia ya maisha yao. Hii haina budi kuwa ni Jumuiya ya Kinabii inayotangaza kwa ujasiri Injili ya Kristo Yesu, tayari kuwaendea na kuwakumbatia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Skauti Italia Miaka 70
13 April 2024, 15:08