Tafuta

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Maria Madgalena wa Canossa 1 Machi 1774-2024. Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Maria Madgalena wa Canossa 1 Machi 1774-2024.  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 250 Tangu Kuzaliwa Kwa Mtakatifu Magdalena wa Canossa: 1774-2024

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 250 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Madgalena wa Canossa 1 Machi 1774-2024, Muasisi wa Shirika Dogo la Mapadre wa Canossa “Figli della carità, “Congregatio Filiorum a Caritate.” Ni Mtakatifu aliyekuwa jasiri katika ulimwengu uliosheheni magumu ya maisha, lakini akajitosa kimasomaso ili kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anapendwa na kufahamika. Ni Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Upendo wa Canossa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mama Kanisa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia.

Papa Francisko anakazia umuhimu wa maadhimisho ya Mikutano mikuu
Papa Francisko anakazia umuhimu wa maadhimisho ya Mikutano mikuu

Mikutano inayoadhimishwa wakati huu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana katika maisha na utume wa kila Shirika la Kitawa na Kazi za Kitume, ili kulinda, kutunza na kuendeleza karama za waanzilishi wa Mashirika haya. Huu ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikilizana; kuchunguza ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili, ili kubaini masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu mamboleo. Rej, Gaudium et spes, 4. Huu ni muda muafaka kwa kila mwanashirika kujikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha yake binafsi na ule wa kijumuiya, tayari kujikita katika maendeleo ya Shirika kwa sasa na kwa siku usoni. Tangu mwanzo wa Kanisa wamekuwepo watu kwa kutekeleza mashauri ya Injili walinuia kumfuasa Kristo Yesu kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu ambao unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, na unaojitoa kabisa kwa Mungu na kwa msukumo wa Roho Mtakatifu, wanaamua kumfuata Kristo Yesu kwa karibu zaidi kwa kujisadaka na kuonesha upendo kwa Mungu, anayepaswa kupendwa kuliko vitu vyote. Rej. Perfectae caritatis, 1 na KKK, 916.

Watawa wajitahidi kusoma alama za nyakati
Watawa wajitahidi kusoma alama za nyakati

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Madgalena wa Canossa 1 Machi 1774-2024, Muasisi wa Shirika Dogo la Mapadre wa Canossa “Figli della carità, “Congregatio Filiorum a Caritate.” Ni Mtakatifu aliyekuwa jasiri katika ulimwengu uliosheheni magumu ya maisha, lakini akajitosa kimasomaso ili kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anapendwa na kufahamika. Shirika Dogo la Mapadre wa Canossa, F.d.C.C., linaadhimisha mkutano wake mkuu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Chi non arde non incendia” yaani "Asiyechoma hawashi moto" kwa kuhakikisha kwamba, zawadi na karama ya Mungu iliyoko ndani mwao wanaitolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni ushuhuda ambao umetolewa na Shirika hili takribani kwa miaka mia mbili iliyopita, kwa kusimikwa na kutajirishwa na karama za wanashirika kutoka katika nchi kumi wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi saba, huku wakishirikiana kwa karibu sana na Masista wa Shirika la Mabinti wa Upendo wa Canossa pamoja na waamini walei wanaoshiriki karama, maisha na utume wao.

Ushirikiano na waamini walei ni muhimu sana.
Ushirikiano na waamini walei ni muhimu sana.

Huu ni utume unaobeba ndani mwake magumu na changamoto za maisha, lakini Mtakatifu Magdalena wa Canossa aliweza kuvuka changamoto zote hizi, kwa kujiaminisha kwa Kristo Yesu aliyefungua mikono yake ili kuwakumbatia: wale waliokuwa wamesukumizwa pembezoni mwa jamii, maskini na wagonjwa, ili kuwaganga, kuwaelimisha na kuwahudumia kwa furaha. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Shirika Dogo la Mapadre wa Canossa, F.d.C.C., Jumatatu tarehe 29 Aprili 2024. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wanapokabiliana na shida pamoja na changamoto za maisha, wajitahidi kumwiga Mtakatifu Maria Magdalena wa Canossa kwa kumwangalia Kristo Yesu Msulubiwa, madonda ya maskini na kwa taratibu wataweza kuona majibu yatakayo wanyooshea njia katika nyoyo zao na hivyo kuwa wazi zaidi.

Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mt. Maria Magdalena wa Canossa
Miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mt. Maria Magdalena wa Canossa

Baba Mtakatifu Francisko amekutana pia na wanashirika wa Shirika la Ndugu wa Mtakatifu Gabrieli lililoanzishwa na Mtakatifu Luigi Maria Grignion de Montfort na Padre Gabriel Deshayes kunako mwaka 1929. Leo hii Shirika lina wanachama 1250 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 34 zilizogawanywa kwenye kanda 15. Hili ni Shirika ambalo limejikita katika utoaji wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya, likichota amana na utajiri wake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili. Shirika linalojihusisha na Katekesi pamoja na shughuli za kichungaji hasa kwa walemavu: vipofu na viziwi. Shirika linaadhimisha Mkutano mkuu unaonogeshwa na kauli mbiu "Sikiliza na utende kwa ujasiri” mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume. Hii ni changamoto kwa Wanashirika kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia karama ya ujasiri, daima wakithamini amana na utajiri walioachiwa yaani Msalaba uliochongwa kwenye Moyo Safi wa Bikira Maria. Shirika linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 350 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Luigi Maria Grignion de Montfort changamoto na mwaliko kwa wanashirika kujenga na kudumisha umoja na mshikamano unaofumbatwa katika karama na mapaji kutoka katika nchi mbalimbali, ili kujenga umoja katika tofauti zao msingi, karama msingi ya kinabii na zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Umoja katika utofauti ni kikolezo cha ukuaji na maendeleo. Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika ni tukio muhimu sana kwa Shirika na Kanisa katika ujumla wake kama kikolezo cha wokovu. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Canossa

 

29 April 2024, 16:28