Tafuta

Vijana Wakatoliki Italia, Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Vijana Wakatoliki Italia, Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.   (Vatican Media)

Chama cha Vijana Wakatoliki Italia: Mashuhuda wa Tunu Msingi za Kiinjili

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia zaidi kwenye kauli mbiu: “Mikono wazi” tayari kuonesha ukarimu, lakini hii ni mikono inayokosekana na matokeo yake kumejengeka, tabia ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine; hii ni mikono inayookoa kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili yaani: Imani, ujasiri na upatanisho na kwamba, hii ni mikono inayoleta mabadiliko katika maisha kwa kujikita katika matumaini na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja na Utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, “L'Azione Cattolica Italiana, AC au ACI” kilianzishwa kunako mwaka 1867 ili kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Sala, matendo na sadaka.” Chama cha Vijana Wakatoliki Italia pamoja na mambo mengine, kinapania kuwajengea uwezo vijana ili wawe ni wadau na mashuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, mchakato unaotekelezwa kwa kuwawezesha vijana kuwa wajenzi wa urafiki wa kijamii, wakarimu kwa kuonja na kuguswa na shida na mahangaiko ya jirani zao; daima wakiendelea kujikita katika utamaduni wa kusikilizana sanjari na kukutana na familia na jumuiya ya waamini kama sehemu muhimu sana ya malezi na majiundo yao ya kiimani. Vijana Wakatoliki Italia, Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Takwimu zinaonesha kwamba, idadi yao ilikuwa ni vijana 60, 000 kutoka sehemu mbalimbali za Italia, waliokuwa wamesheheni furaha na matumaini lakini wanapaswa kutowasahau wale wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali za maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia zaidi kwenye kauli mbiu: “Mikono wazi” tayari kuonesha ukarimu, lakini hii ni mikono inayokosekana na matokeo yake kumejengeka, tabia ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine; hii ni mikono inayookoa kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili yaani: Imani, ujasiri na upatanisho na kwamba, hii ni mikono inayoleta mabadiliko katika maisha kwa kujikita katika matumaini na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Chama cha Vijana Italia mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Chama cha Vijana Italia mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Baba Mtakatifu anasema, mikono wazi ni kielelezo cha mang’amuzi na uzoefu wa kibinadamu, kielelezo cha ukarimu katika hija ya maisha ya binadamu, hadi pale anapokata roho na kurejea kwa Muumba wake. Mikono wazi ya Mwenyezi Mungu ni kielelezo cha upendo wenye huruma, kama inavyojionesha kwenye Injili ya Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu. Rej. Lk 15: 1-3; 11-32. Mikono wazi ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, mikono wazi ambayo haipo ni kielelezo cha uchoyo na ubinafsi dhidi ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kukoleza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Kumbe, mikono wazi isiyokuwepo ni alama ya kinzani, matumizi ya nguvu, na mipasuko ya kijamii; na wakati mwingine, mwelekeo kama huu ndio chanzo cha vita na migogoro inayosimikwa katika dhana ya maamuzi mbele, tabia ya kuwakataa watu wengine na hivyo kushindwa kuwakubali, kiasi hata cha kuwaona kuwa ni maadui, kama inavyojionesha sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya Vijana Wakatoliki Italia kwa njia ya ushuhuda wa uwepo wao na shughuli zao mbalimbali wanaweza kuwahakikishia walimwengu kwamba, mikono wazi ndio njia ya maisha. Baba Mtakatifu anasema, mikono wazi inayookoa, ni ile inayojikita katika tunu msingi za maisha kama vile imani, ujasiri na upatanisho mintarafu mwanga wa imani. Itakumbukwa kwamba, kiini cha maisha ya waamini ni mikono ya huruma ya Mungu inayookoa, Baba mwema aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu na kwamba, huu ni Uso unaoonesha huruma ya Mungu, msamaha, uponyaji, uhuru na huduma. Rej. Yn 13:1-15 mambo msingi yanayobubujika katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwamba, yanapata utimilifu wake kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Ni Uso wa huruma ya Mungu aliyethubutu kuwasamehe hata watesi wake. Rej. Lk 23: 34.

Vijana zaidi ya 60, 000 wamekutana na Papa Francisko mjini Vatican.
Vijana zaidi ya 60, 000 wamekutana na Papa Francisko mjini Vatican.

Huu ni mwaliko kwa waamini kujifunza na kujitahidi kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, tayari kumkumbatia na kumwambata Kristo Yesu, kama watoto wadogo na kwa njia hii, wajibidiishe kuwakumbatia jirani zao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mikono wazi inaleta mabadiliko katika maisha kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na kwamba, kuna watakatifu wengi ambao wameacha alama za kudumu na kati yao ni Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyeacha yote na kuamua kufuasa Kristo Yesu, mara baada ya kuguswa na mtu mwenye Ukoma, changamoto na mwaliko wa kukumbatia matumaini katika upendo. Kwani upendo kwa Mung una jirani ndio mhuri aliotiwa kila mfuasi wa kweli wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwakumbatia na kuwaambata maskini, wahitaji zaidi na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hii ni dhamana na wajibu wa waamini walei kupyaisha maisha na utume wao mintarafu mwanga wa Injili na hivyo kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho na haki; ujenzi wa ushirika na uwajibikaji, ili kujenga leo na Kesho inayosimikwa katika msingi wa amani. Huu ndio utamaduni wa mikono wazi.

Vijana Wakatoliki Italia wakutana na Papa Francisko
Vijana Wakatoliki Italia wakutana na Papa Francisko

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni mahujaji wa matumaini kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, hivi karibuni waliweza kuishi kikamilifu mchakato wa maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu katika ngazi mbalimbali. Maadhimisho haya yasaidie kujenga na kudumisha ushirika, uwajibikaji wa pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amekishukru Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, “L'Azione Cattolica Italiana, AC au ACI” kwa kazi na ushuhuda wanaoendelea kuutoa katika maisha na utume wa Kanisa.

Vijana Wakatoliki
25 April 2024, 16:22