Tafuta

Ni katika muktadha wa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji Maaskofu Katoliki kutoka Colombia, Costa Rica na Panamà kuanzia tarehe 19 hadi 22 Machi 2024 wanakutana mpakani kati ya Colombia na Panamà. Ni katika muktadha wa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji Maaskofu Katoliki kutoka Colombia, Costa Rica na Panamà kuanzia tarehe 19 hadi 22 Machi 2024 wanakutana mpakani kati ya Colombia na Panamà.  (ANSA)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Maaskofu wa Amerika ya Kusini: Wakimbizi na Wahamiaji

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maaskofu hawa anakazia kuhusu: Wakimbizi na wahamiaji Amerika ya Kati; Ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, Shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji; Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2023 yamenogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki”, Umuhimu wa kuwa na wahudumu wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni katika muktadha wa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji Maaskofu Katoliki kutoka Colombia, Costa Rica na Panamà kuanzia tarehe 19 hadi 22 Machi 2024 wanakutana mpakani kati ya Colombia na Panamà, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Sherehe ya Pasaka Na Ndugu Zetu Wahamiaji.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maaskofu hawa anakazia kuhusu: Wakimbizi na wahamiaji Amerika ya Kati; Ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, Shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji; Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2023 yamenogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki”, Umuhimu wa kuwa na wahudumu wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.
Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mkutano wa tisa unaowaunganisha Maaskofu kutoka Amerika ya Kati, wakati huu wa maandalio ya Karamu ya Pasaka ya Bwana: “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Mt 26: 17. Leo hii, Mama Kanisa anafanya hija ya kiroho na wakimbizi pamoja na wahamiaji, huku akishuhudia vifo na machozi yanayowaunganisha watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini wanaopitia katika msitu mnene wa Tapòn del Darièm ambao umegeuka na kuwa ni njia ya Msalaba, ambayo kuna baadhi ya watu wanaitumia kama chambo cha kujichumia fedha ya haraka haraka kutokana na biashara haramu ya binadamu. Mara nyingi wakimbizi na wahamiaji hawa wanakataliwa kuingia katika baadhi ya nchi, kwa lengo la kujipatia hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, huku wakiwa na tumaini la kuweza kuunganika tena na familia zao.

Wakimbizi wanahitaji upendo na mshikamano
Wakimbizi wanahitaji upendo na mshikamano

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi na wahamiaji, ili kuonesha mshikamano wa Kanisa na Wakimbizi na wahamiaji, kwamba, Kanisa ni Mama wa wote na wala hana mipaka kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Watu wa Mungu katika nchi hizi wameendelea kuonesha udugu wa kibinadamu lakini kuna wengine, ambao wameonesha ugumu wa mioyo kwa kushindwa kuwapokea na kuwakaribisha. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu waweze kushikamana ili kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanaoneshwa ukarimu na udugu wa kibinadamu, kwa kuwapokea na kuwalisha na kuwanywesha pamoja na kupyaisha matumaini yaliomo ndani mwao, kwa kuunda mazingira ya urafiki na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anatambua na kukiri ukarimu wa watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini na kwamba, kuna haja ya kuunda na kuimarisha utume wa shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji; kujenga vituo vya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji vitakavyosaidia kutoa huduma ya msaada na dharura; huduma ya afya na msaada wa kisaikolojia; huduma ya ukarimu na upendo.

Wakimbizi wanahitaji usalama, hifadhi na matumaini ya maisha.
Wakimbizi wanahitaji usalama, hifadhi na matumaini ya maisha.

Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2023 yamenogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Kauli mbiu hii inapania pamoja na mambo mengine kukuza tafakari na ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe. Kuna sababu nyingi ambazo zinapelekea watu kulazimika kuyahama makazi na nchi zao, ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Haki ya kubaki nchini mwako ina mizizi yake katika maisha ya mwanadamu, kwani hii ni haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni haki inayomwezesha mtu kuishi kwa kuzingatia utu, heshima na haki zake msingi na hivyo kujipatia pia maendeleo fungamani. Haki inapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wa Amerika ya Kusini kuunganisha nguvu zao sanjari na kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa kuhakikisha kwamba, watu wanabaki katika nchi zao wenyewe, huku wakiwa na maisha mazuri na amani. Hija ya wakimbizi na wahamiaji inawahitaji wahudumu wa shughuli za kichungaji ili kuvuka vikwazo na kuwarejeshea tena wakimbizi na wahamiaji matumaini ya maisha. Hii itasaidia kujenga Kanisa moja lenye: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” kwa kutambua na kuthamini haki zao msingi na hivyo kuwajengea uwezo wakimbizi na wahamiaji kuweza kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Wakimbizi na Wahamiaji
21 March 2024, 14:52