Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika Salam, Baraka na Ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, tarehe 31 Machi 2024 Baba Mtakatifu Francisko katika Salam, Baraka na Ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, tarehe 31 Machi 2024  

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko "Urbi et Orbi" Pasaka 2024: Mawe!

Ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu: “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, tarehe 31 Machi 2024 amegusia kuhusu: Fumbo la Pasaka: Mawe yanayo vuruga matumaini ya binadamu; Kristo Yesu ni njia; Waathirika wa vita sehemu mbalimbali za dunia; Nchi za Balkan ya Magharibi zinazowania kujiunga na Umoja wa Ulaya, Watu wanaoteseka kutokana na vita, ukosefu wa usalama wa chakula pamoja na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Kristo Mfufuka awe ni faraja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Salam, Baraka na Ujumbe kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” ulianza kutolewa kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1974. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujumbe huu unawafikia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mfumo wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya satellite saba. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe za Pasaka ya Bwana ameongoza kwanza: Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika Salam, Baraka na Ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, tarehe 31 Machi 2024 amegusia kuhusu: Fumbo la Pasaka: Mawe yanayo vuruga matumaini ya binadamu; Kristo Yesu ni njia; Waathirika wa vita sehemu mbalimbali za dunia; Nchi za Balkan ya Magharibi zinazowania kujiunga na Umoja wa Ulaya, Watu wanaoteseka kutokana na vita, ukosefu wa usalama wa chakula pamoja na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Kristo Mfufuka awe ni faraja kwa Rohingya na Myanmar, Amani Barani Afrika; Kristo Mfufuka awaangazie wakimbizi na wahamiaji; Upendo wa Mungu hauna mipaka na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Imegota miaka takribani miaka elfu mbili tangu Kristo Yesu alipoteswa, akafa na kufufuka kwa watu, ushuhuda ulitolewa na wanawake waliokwenda kaburini siku ile ya kwanza ya juma walitambua kwamba, kulikuwa na jiwe kubwa mlangoni pa kaburi la Yesu. Haya ndiyo mawe yanayo vuruga matumaini ya binadamu: mawe ya vita, dharura mbalimbali, ukosefu na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, mawe ya biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake. Ni katika muktadha huu, kama ilivyokuwa kwa wale wanawake, Je, ni nani atakayewaviringishia wanadamu lile jiwe mlangoni pa kaburi? Rej. Mk 16:3. Lakini jambo la kushangaza Siku ile ya kwanza ya juma, wakagundua kwamba, lile jiwe limekwisha ondolewa pale kaburini, kaburi likawa wazi na Kristo Yesu hakuwemo kaburini!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Urbi et Orbi Pasaka 2024
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Urbi et Orbi Pasaka 2024

Jambo hili likawashangaza na huo ukawa ni mwanzo mpya unaoelekea kwenye kaburi tupu. Lakini ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye alikuwa na uwezo wa kulifungua kaburi, kufungua njia mpya ya maisha dhidi ya kifo; njia ya amani na upatanisho dhidi ya chuki, uhasama na vita; njia ya udugu wa ubinadamu kati ya chuki na uadui. Kristo Mfufuka ndiye mwenye nguvu ya kuliondoa jiwe, kwani Yeye ni njia: inayaowaongoza binadamu katika maisha, ni njia ya amani, maridhiano na udugu wa kibinadamu, kwani Kristo Yesu ni Mwanakondoo wa Mungu anayezichukua dhambi za binadamu na kumsamehe. Bila msamaha wa dhambi kutoka kwa Mwenyezi Mungu lile jiwe halitaweza kuondolewa na hivyo kuvuka maamuzi mbele, shutuma, kwa kujihesababia haki na kuwaona wengine kuwa ni wakosaji. Ni Kristo Yesu, peke yake anayewakirimia waja wake msahamaha wa dhambi na hivyo kufungua njia za kupyaisha ulimwengu. Ni Kristo Yesu peke yake, anayeweza kuwafungulia waja wake malango ya maisha dhidi ya vita, kinzani na mipasuko inayoendelea kutokea sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuyaelekeza macho yake kwenye Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, ulioshuhudia Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake kwa waathirika wengi wa vita kati ya Israeli na Palestina, Urusi na Ukraine. Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Mfufuka aweze kuingilia kati na kuwafungulia njia ya amani katika miji hii ambayo imeathirika kwa vita. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, sheria za Kimataifa zinalindwa na kutetekelezeka pamoja na kuonesha utayari wa kubadilishana wafungwa wa kivita.

Vita kati ya Ukraine na Urusi vimesababisha madhara makubwa
Vita kati ya Ukraine na Urusi vimesababisha madhara makubwa

Jumuiya ya Kimataifa ihakikishe misaada ya kiutu inawafikia walengwa sanjari na kuwaachilia wafungwa wa kivita waliotekwa nyara tarehe 7 Oktoba 2023 pamoja na kusitishwa mara moja mapigano kwenye Ukanda wa Gaza na kamwe mapigano yasiruhusiwe kuendelea kwani yana madhara makubwa katika raia. Lakini kwanini kuna uharibifu mkubwa, vifo vya watu wasiokuwa na hatia, mateso na mahangaiko ya watu? Kuna haja ya kuondokana na falsafa ya vita. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasiisahau Siria, ambayo kwa takribani miaka kumi na nne, inaendelea kuteseka kwa vita. Kuna watu wengi wanapoteza maisha na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha; kuna uharibifu mkubwa unaohitaji uwajibikaji wa kila mtu bila kuisahau Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wa Mungu nchini Lebanon inayoendelea kuteseka kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii; hali ambayo inaendelea kugumishwa kutokana na uhasama kati ya Lebanon na Israeli. Kristo Mfufuka, awe ni faraja kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, ili waweze kujenga na kudumisha wito wao wa kuwakutanisha watu, maridhiano na kuishi katika wingi. Anaziombea nchi za Balkani ya Magharibi ambazo ziko kwenye mchakato wa kujiunga na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Kamwe ukabila, tofauti za kidini na kiimani zisiwe ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii, bali chanzo cha kutajirishana Barani Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anaendelea kutia shime ya kuendeleza majadiliano kati ya Armenia na Azerbaijan, ili kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa waendelee kujikita katika majadiliano, watoe huduma kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa bila kuwasahau waathirika wa mabadiliko ya tabianchi.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu anapenda kutoa faraja kwa wale wote wanaoteseka na kufa kutokana na vitendo vya kigaidi na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea wote waliopoteza ndugu jamaa na marafiki. Anawaombea toba na wongofu wa ndani wale wote wanaosababisha vitendo hivyo. Kristo Mfufuka awasaidie watu wa Mungu nchini Haiti, ili wafikie mwisho wa vitendo vya uvunjifu wa haki na amani na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia, ili hatimaye, Haiti ianze kujielekeza katika ujenzi wa demokrasia na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuwafariji watu wa Rohingya na kuwatia shime kutokana na dharura ya kibinadamu wanayokabiliana nayo, waweze kufungua njia ya upatanisho huko Myanmar baada ya kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka kadhaa sasa, ili hatimaye, mantiki ya vita iweze kuwekwa kando. Baba Mtakatifu ameliombea Bara la Afrika liweze kukumbatia amani, hasa kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini pamoja na Ukanda mzima wa Sahel; Pwani ya Pembe ya Afrika, Mkoa wa Kivu, nchini DRC, Jimbo la Capo Delgado nchini Msumbiji ili hatimaye, watu walioathirika kwa ukame na baa la njaa waweze walau kupata nafuu. Mwanga wa Kristo Mfufuka uwaangazie wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka kutoka na hali ngumu ya uchumi, wapate faraja na matumaini. Kristo Mfufuka awaunganishe watu wenye mapenzi mema ili waweze kuwa wamoja katika mshikamano ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kuziandama familia maskini zinazotafuta furaha na maisha bora zaidi.

Haki na amani nchini DRC
Haki na amani nchini DRC

Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, ni kumbukumbu ya upendo wa Mungu usiokuwa na kifani na kwamba huu ni mwaliko kwa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba; baa la njaa bila kusahau msaada kwa waathirika wa nyanyaso na vita. Inasikitisha kuona kwamba, kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake; vitendo vinavyosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, Baba Mtakatifu ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wale wote wenye mamlaka kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona na biashara ya binadamu pamoja na viungo vyake. Kristo Mfufuka awe ni faraja kwa familia na wale wote wanaosubiria kusikia habari njema za ndugu zao, awajalie faraja na matumaini. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa: Salam, Baraka na Ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, tarehe 31 Machi 2024 ameomba ili mwanga wa Kristo Mfufuka uweze kuziangazia akili na kuzielekeza katika toba na wongofu wa ndani ili kutambua na kuthamini thamani ya kila maisha ya binadamu yanayopaswa kukaribishwa, kulindwa na kupendwa.

Urbi et Orbi 2024
31 March 2024, 14:16