Tafuta

Ni katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 Ni katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sherehe ya Mtakatifu Yosefu: Kumbukizi ya Miaka 11 ya Utume wa Papa Francisko 2024

Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mt. Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mama Kanisa tarehe 19 Machi 2024 anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki, Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu, aliyezaliwa kwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yosefu akamwita jina lake Yesu, maana Yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao na kutambuliwa kisheria kuwa ni Mwana wa Ukoo wa Daudi, Mwana wa Ibrahimu, Baba wa imani. Mtakatifu Yosefu aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi mwaminifu wa Nyumba ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu sanjari na kukubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake, kama alivyoambiwa na Malaika wakati akiwa usingizini. Akamchukua Bikira Maria kama mchumba wake. Katika hali ya hatari, alimchukua Mtoto na Mama yake Bikira Maria, wakakimbilia Misri na kukaa huko hata alipofariki Herode, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema, “Kutoka Misri nalimwita mwanangu.” Rej. Mt 1: 1-25; 2: 1-23. Mtakatifu Yosefu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara ambaye Bwana alimweka juu ya watumishi wake. Rej. Lk 12:42. Ni mfano bora katika maisha ya waamini aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu akailinda na kutunza Familia Takatifu ya Nazareti kwa kazi ya mikono yake. Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya Jubilei ya Huruma ya Mungu
Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya Jubilei ya Huruma ya Mungu

Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hawa pia ni wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake ameendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu na kuendelea kukazia haki na wajibu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kuendelea kukuza ari na mwamko wa ushirikiano na mafungamano ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, anagusia kuhusu: Magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo kwamba ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anajikita kwenye siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni kielelezo cha “familia ya Mataifa.” Watu wa Mungu hawana budi kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana.

Kipaumbele: Ujenzi wa udugu wa kibinadamu
Kipaumbele: Ujenzi wa udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Dini na udugu wa kibinadamu ni chanda na pete; hapa mkazo ni umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umegawanyika katika sura kuu sita: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani Duniani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na jinsi vinavyohusiana na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni kuhusu umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani, Sakramenti za Kanisa pamoja na sala. Waraka huu una mwelekeo wa umoja na mshikamano ambao unadhihirishwa na mchango uliotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Utunzaji wa mazingira unakita mizizi yake katika misingi ya haki na amani
Utunzaji wa mazingira unakita mizizi yake katika misingi ya haki na amani

Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kujikita katika wongofu wa kiikolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.
Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” ulichapishwa tarehe 4 Oktoba 2023, Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na mwanzo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Waraka huu wa Kitume umechapishwa baada ya miaka minane tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Kumbe, Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” unakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi, ufanisi na kuanguka kwake; Yale yaliyokuwa ni Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP 28 huko Dubai, 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji. Kumbe, Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, yataendelea kuwa ni nguzo msingi na rejea kwa Serikali, Jumuiya ya Kimataifa, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.

Mt. Yosefu
18 March 2024, 15:07