Tafuta

Ufufuko wa Kristo Yesu ni ushindi dhidi ya kifo na kwamba, kifo hakiwezi kuwa na sauti ya mwisho, kwani alikuwa amekufa, lakini sasa yu hai. Ufufuko wa Kristo Yesu ni ushindi dhidi ya kifo na kwamba, kifo hakiwezi kuwa na sauti ya mwisho, kwani alikuwa amekufa, lakini sasa yu hai.   (Vatican Media)

Mkesha wa Sherehe ya Pasaka: Ushuhuda wa Wanawake

Papa megusia kuhusu: Miamba inayoelemea nafsi za waamini, Pasaka ya Kristo Yesu ni nguvu ya Mungu, mwaliko kwa waamini kumwinulia macho Yesu aliyefufuka na kwamba, katika kiza kinene cha matarajio na vifo vyao, tayari kuna uzima wa milele ambao Yesu alikuja kuwaletea waja wake. Baba Mtakatifu anasema, hata alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza, lakini ndani ya nyoyo zao walikuwa na giza na simanzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Maadhimisho ya Mkesha wa Pasaka yamegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni Liturujia ya Mwanga inayopambwa kwa kuwashwa Mshumaa wa Pasaka na kupigwa kwa mbiu ya Pasaka, kwa kuyakumbuka na kuyatafakari maajabu ya Mwenyezi Mungu aliyolitendea Taifa lake teule tangu mwanzo. Pili ni Liturujia ya Neno yenye masomo tisa yanayosimulizia historia ya mwanadamu tangu kuumbwa kwa ulimwengu mpaka hatima ya ukombozi wake kwa njia ya Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Tatu ni adhimisho la Sakramenti ya Ubatizo wa Wakatekumeni, ishara ya ukamilifu wa Agano Jipya na la milele. Na nne Kanisa pamoja na Wakristo wapya waliozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu wanashiriki Karamu ya Bwana kwa kuumega mkate ulioshuka kutoka mbinguni. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkesha wa Pasaka tarehe 30 Machi 2024 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwabatiza, kuwapatia Sakramenti ya Kipaimara na hatimaye, Komunyo ya kwanza, wakatekumeni nane kutoka: Italia, Korea, Japan na Albania. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amegusia kuhusu: Miamba inayoelemea nafsi za waamini, Pasaka ya Kristo Yesu ni nguvu ya Mungu, mwaliko kwa waamini kumwinulia macho Kristo Yesu aliyefufuka kwa wafu na kwamba, katika kiza kinene cha matarajio na vifo vyao, tayari kuna uzima wa milele ambao Kristo Yesu alikuja kuwaleeta waja wake.

Jiwe kubwa mahali pa kaburi la Yesu kilikuwa ni kizingiti cha matumaini
Jiwe kubwa mahali pa kaburi la Yesu kilikuwa ni kizingiti cha matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza, lakini ndani ya nyoyo zao walikuwa wamebanwa na giza nene, walibaki chini ya Msalaba, wakiwa wamegubikwa na uchungu mkubwa na kwamba, maisha na utume wa Kristo Yesu, yalikuwa yamefungwa kwa jiwe kubwa pale mlangoni pa kaburi. “Wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Mk 16:3. Lakini walipofika kaburini, wakashangazwa na nguvu ya Pasaka kwani walikuwa wanaulizana ni nani atakayeviringisha lile jiwe mlangoni pa kaburi? Furaha ya Pasaka ya Bwana inabubujika baada ya wale wanawake kuona kwamba, lile jiwe limekwisha kuviringishwa. Jiwe ni kielelezo cha hatima ya maisha, utume na historia ya Kristo Yesu. Kristo aliyekuja ulimwenguni ili kutoa uhai wake, aliyetangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu; aliyewasamehe na kuwaondolea watu dhambi zao, amehukumiwa adhabu ya kifo. Mfalme wa amani aliyemwokoa yule mwanamke aliyefumaniwa akizini, wakataka apige na mawe hadi kufa ndiye huyu anayelala kaburini. Haya yalikuwa ni mahangaiko yanayokita mizizi yake katika nyoyo za wale wanawake, kiasi cha kufifisha matumaini yao na hatimaye, kuzima ndoto ya maisha yao. Hali na mazingira kama haya yanaweza kumtokea mwamini kiasi kwamba, jiwe linaingia katika moyo wa mtu, linakatisha maisha na kuzima imani, kiasi cha kukuza hofu na machungu ya moyoni yanayovuruga furaha na matumaini, kielelezo cha kifo, kinachowapoka watu ari na nguvu ya kusonga mbele.

Wakatekumeni nane wamebatizwa, kupewa Kipaimara na kukomunika
Wakatekumeni nane wamebatizwa, kupewa Kipaimara na kukomunika

Ni kifo kinachogusa maisha ya ndugu na jamaa na hivyo kuacha machungu moyoni; ukarimu na upendo unaofunikwa na choyo, hali ya kutowajali na kuwathamini wengine; haki na amani, vinavyovurugwa na chuki, uhasama na vita. Haya ni mambo yanayoacha maswali yasiyokuwa na majibu: “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Mk 16:3. Lakini wanawake walipotazama, waliona kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa, hii ndiyo nguvu ya Pasaka, nguvu ya Mungu, ushindi dhidi ya dhambi na kifo, chemchemi ya matumaini, changamoto na mwaliko kwa waamini kuinua macho yao na kumtazama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa nguvu za Utatu Mtakatifu. Ufufuko wa Kristo Yesu ni ushindi dhidi ya kifo na kwamba, kifo hakiwezi kuwa na sauti ya mwisho, kwani alikuwa amekufa, lakini sasa yu hai. Kristo Yesu ndiye Pasaka ya waja wake, chemchemi ya msamaha na maisha ya uzima wa milele, kinyume kabisa cha kukata na kujikatia tamaa ya maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia maisha na uzima wa milele. Usiku huu mtakatifu waamini wanaalikwa kuimba juu ya ufufuko wa Kristo Yesu, Yeye ndiye Bwana wa maisha mapya kwa wale wasiokuwa na haki, wakimbizi na wahamiaji, mashuhuda na waungama imani. Kristo Yesu amefungua mikono yake, amefufuka, yu hai. Kwa hakika hii ni Pasaka ya Bwana, Sherehe ya walio hai.

Mkesha wa Pasaka
31 March 2024, 12:39