Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, kuanzia tarehe 20-22 Machi 2024 huko Brasilia wameadhimisha Juma la Sita la Kijamii Nchini Brazil Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, kuanzia tarehe 20-22 Machi 2024 huko Brasilia wameadhimisha Juma la Sita la Kijamii Nchini Brazil  

Maadhimisho ya Juma la Sita la Kijamii Brazil: Mafundisho Jamii ya Kanisa

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, kuanzia tarehe 20-22 Machi 2024 huko Brasilia wameadhimisha Juma la Sita la Kijamii Nchini Brazil “Semana Social Brasileira” kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Brazil tunayoitaka: Maisha Bora ya Watu”: Matarajio ya watu wa Mungu nchini Brazil katika sekta ya makazi ya watu, ardhi, kazi, uchumi, utawala na demokrasia. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kuhusu: Uchumi shirikishi, Ardhi, Makazi na Kazi na Ukosefu wa haki jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.

Mkazo ni kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, heshima na haki msingi
Mkazo ni kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, heshima na haki msingi

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, kuanzia tarehe 20-22 Machi 2024 huko Brasilia wameadhimisha Juma la Sita la Kijamii Nchini Brazil “Semana Social Brasileira” kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Brazil tunayoitaka: Maisha Bora ya Watu”: Matarajio ya watu wa Mungu nchini Brazil katika sekta ya makazi ya watu, ardhi, kazi, uchumi, utawala na demokrasia. Lengo ni kubainisha haki msingi, ili kuliwezesha Kanisa kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Brazil, sanjari na ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya wananchi nchini Brazil. Inaonekana kukosekana mjadala kuhusu uchumi, changamoto ya maji safi na salama, sera bora za nishati, uchimbaji wa madini pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuhusu kazi, wajumbe wanasema, kuna haja kwa Taifa kutokomeza kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo pamoja na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira magumu na hatarishi.

Matumizi sahihi ya teknolojia ya akili mnemba
Matumizi sahihi ya teknolojia ya akili mnemba

Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yanaelekea kukandamiza na kudumaza kazi ya binadamu na hivyo kuathiri ajira kwa vijana na wahamiaji. Kuhusu demokrasia mkazo umekwa kwa ushirikishwaji wa vijana wa kizazi kipya; kuwasaidia na kuwaenzi wazee na watu wasiojiweza na wale watu ambao wamenyimwa uhuru wao. Demokrasia ya mawasiliano ya jamii pamoja na vijana kupewa kipaumbele cha pekee ni kati ya tema ambazo zimepewa kipaumbele cha pekee. Kuhusu uchumi, wajumbe wamekazia umuhimu wa kufanya mageuzi kuhusu usahihi wa kodi wanayolipa watu wa Mungu nchini Brazil. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la Sita la Kijamii Nchini Brazil kwa mwaka 2024, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe maalum washiriki wa maadhimisho haya akikazia kwa namna ya pekee kabisa: umuhimu wa maadhimisho haya; uchumi shirikishi na unaosimikwa katika mshikamano; Uchumi wa Papa Francisko; Ardhi, makazi na kazi pamoja na ukosefu wa haki jamii. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya ulisomwa kwa niaba yake na Monsinyo Avelino Chico, Afisa Mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Baba Mtakatifu amewatakia mafanikio mema katika maadhimisho haya. Tangu mwaka 1991 Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limekuwa likiadhimisha Juma la Kijamii Nchini Brazil, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Brazil kuvunjilia mbali kuta za utengano na utamaduni wa kutupa, usiojali mateso na mahangaiko ya wengine. Kanisa linataka kuona kwamba, watu wanapata haki zao msingi, ikiwa ni pamoja na: ardhi, makazi na kazi.

Mafundisho Jamii ya Kanisa: Mazingira Nyumba ya Wote
Mafundisho Jamii ya Kanisa: Mazingira Nyumba ya Wote

Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu nchini Brazil wanajenga na kudumisha uchumi shirikishi unaosimikwa katika mshikamano na mafungamano ya watu, ili kudumisha tunu msingi za kidemokrasia zinazowawezesha raia kushiriki katika mchakato wa maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati yao ya maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kusimamia kwa vitendo uchumi wa Mtakatifu Francisko wa Assis na Chiara wa Assisi. Binadamu anapaswa kuwa ni kiini na hatima ya sera na mikakati ya maendeleo fungamani kwa kukazia: umuhimu wa ardhi, makazi na ajira. Ardhi ni amana na utajiri wa binadamu wote na matunda yake ni kwa ajili ya wote. Kila mtu anayo haki ya kutumia ardhi kwa ajili ya mafao yake. Hii ni kanuni maadili inayolinda utaratibu wa maisha. Kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya kazi na mazingira na kwamba, kuna baadhi ya shughuli za binadamu zinazosababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira, kwa kuzalisha hewa ya ukaa. Jumuiya ya Kimataifa inapoweka sera na mikakati ya kulinda fursa za ajira, haina budi kuhakikisha kwamba inazingatia mwingiliano kati ya ardhi, makazi na ajira. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, jitihada zote hizi zitaweza kusaidia ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Lengo ni kuwaokoa watu wanaoteseka na umaskini wa kijamii.

Brazil Juma Jamii
23 March 2024, 13:20