Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 11 Februari 2024 anatarajia kumtangaza Mwenyeheri Maria Antonia de San José de Paz y Figueroa, maarufu kama "Mama Antula” Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 11 Februari 2024 anatarajia kumtangaza Mwenyeheri Maria Antonia de San José de Paz y Figueroa, maarufu kama "Mama Antula”   (Vatican Media)

Mtakatifu Maria Antonia de San José: Mama Antula Kutoka Argentina

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Februari 2024 amekutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Argentina na kuwataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu; watangaze na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha; wakuze na kudumisha Ibada kwa Ekaristi Takatifu na kwa Mtakatifu Yosefu. Alijisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote waliosukumizwa pembezoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 11 Februari 2024 anatarajia kumtangaza Mwenyeheri Maria Antonia de San José de Paz y Figueroa, maarufu kama "Mama Antula” kuwa ni Mtakatifu wa kwanza kutoka nchini Argentina. Ni mwanamke aliyejishughulisha sana katika maisha na utume wa Kanisa. Akatangaza na kushuhudia ubunifu na ujasiri wa kimisionari. Ni mwanamke mlei aliyeishi katika kipindi kigumu cha historia na utume wa Kanisa baada ya Mfalme Charles III kuwafukuza Wayesuit kutoka Hispania na kutoka kwa Mtawala wa Río de la Plata, akajikita katika mazoezi ya maisha ya kiroho kama changamoto ya Kiinjili kwa waamini wakati huo, ili kusonga mbele kwa kutiwa ari na moyo wa kimisionari, kwa kukuza na kudumisha ushirika na umisionari, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wote wa Mataifa. Mama Antula alijihusisha kuchukua hatua ya kwanza kwa kujihusisha ili kuzaa matunda ya furaha! Hii ndiyo changamoto kubwa kwa watu wa Mungu kutoka nchini Argentina na Kanisa katika ujumla wake.

Mtakatifu Maria Antonia de San Josè
Mtakatifu Maria Antonia de San Josè

Ni katika muktadha wa kutangazwa Mwenyeheri Maria Antonia de San José de Paz y Figueroa, "Mama Antula” kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Argentina waliofika mjini Vatican kushiriki katika maadhimisho haya na kama kielelezo cha ibada na uchaji wao kwa Mtakatifu Maria Antonia de San Josè, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na “kirusi cha uchoyo na ubinafsi.” Mama Kanisa daima ataendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wale walio wadogo kabisa, wale ambao jamii inawatupilia mbali. Evangelii gaudium 195.

Mtakatifu Maria Antonia shuhuda wa Fumbo la Pasaka
Mtakatifu Maria Antonia shuhuda wa Fumbo la Pasaka

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Februari 2024 amekutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Argentina na kuwataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu; watangaze na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha; wakuze na kudumisha Ibada kwa Ekaristi Takatifu na kwa Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Maria Antonia de San José de Paz y Figueroa, "Mama Antula” ni mfano bora wa kuigwa kwa ajili ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Mahujaji kutoka Argentina: Mtakatifu Maria Antonia de san Josè
Mahujaji kutoka Argentina: Mtakatifu Maria Antonia de san Josè

Ni Mtakatifu aliyejiaminisha katika nguvu na uweza wa Mungu na yote aliyafanya kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Hii ilikuwa ni chemchemi ya tasaufi yake ya Kiinyasiana na hata pale, Wayesuit walipozuiliwa kutekeleza dhamana na wajibu wao, lakini kwake, Mafungo ya Maisha ya Kiroho ulikuwa ni utume uliowasaidia wengi kutambua wito wa kumfuasa Kristo Yesu. Huu ni utume alioufanya kwa kificho! Hii ni changamoto na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha. “Lakini familia na mahali pa kazi panaweza pia kuwa sehemu kame ambapo inabidi imani itunzwe na kuwasilishwa.” Evangelii gaudium 86. Hii ni changamoto ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili pamoja na kukabiliana na changamoto mamboleo. Mtakatifu “Mama Antula” alikuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ambayo kwake ilikuwa ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Rej. SC 10. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutoka nchini Argentina kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumtangaza Mwenyeheri Maria Antonia de San José de Paz y Figueroa, maarufu kama "Mama Antula” kuwa ni Mtakatifu wa kwanza kutoka nchini Argentina. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya kumtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Awasaidie mahujaji kufanya hija ya pekee kuelekea nyumbani kwa Baba wa milele.

Mt. Mama Antula

 

09 February 2024, 15:03