Tafuta

Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu hapo tarehe 8 Febuari 2024. Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu hapo tarehe 8 Febuari 2024. 

Mtakatifu Josefina Bakhita: Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari: Biashara ya Binadamu

Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Febuari 2024 kwa utashi na busara za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho ya Mwaka huu 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu, kusikiliza, kuota ndoto na kutenda.” Mtakatifu Bakhita alizaliwa Mwaka 1868, akafariki dunia 8 Februari 1947 na kutangazwa Mtakatifu mwaka 2000.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anawatia shime wale wote wanaosimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaweza kufanya kazi kwa dhati kuondoa visababishi vya janga hili linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kila mtu anapaswa kuwa ni sauti ya wale wote wanaodhalilishwa katika utu wao! Mtakatifu Josefina Bakhita, “Mwanamke wa shoka” alibahatika kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu kugeuza mateso na mahangaiko yake yote kuwa ni chemchemi ya Injili ya matumaini iliyogeuka hatimaye, na kuwa ni mbegu ya matumaini.  Mtakatifu Josefina Bakhita “Fortunata” maana yake “Bahati” alizaliwa kunako mwaka 1868 huko mjini Darfur, Sudan Kongwe. Akatekwa nyara na “watu wasiojulikana” akauzwa utumwani, na hatimaye, akanunuliwa na Balozi wa Italia mjini Khartoum aliyempeleka mjini Venezia. Akafundishwa katekesi na hatimaye, kubatizwa. Baadaye alijiunga na Shirika la Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Madgalena wa Canossa akijitoa sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma. Alifariki dunia tarehe 8 Februari 1947 huko Schio, nchini Italia. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe Mosi Oktoba, mwaka 2000 katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Siku ya Kumi Kimataifa ya Kusali na Kutafakari Kuhusu Biashara ya Binadamu
Siku ya Kumi Kimataifa ya Kusali na Kutafakari Kuhusu Biashara ya Binadamu

Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko likaanzisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni muda muafaka kwa ajili ya kusali na kuwaombea waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Februari 2023 yalinogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.” Huu ni mwaliko hasa kwa vijana kusaidia kuragibisha maadhimisho haya dhidi ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu na kama sehemu ya maandalizi ya Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku hii hapo tarehe 8 Febuari 2024 kwa utashi na busara za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho ya Mwaka huu yananogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu, kusikiliza, kuota ndoto na kutenda.”

Kau mbiu: Kutembea katika utu, kusikiliza, kuota ndoto na kutenda
Kau mbiu: Kutembea katika utu, kusikiliza, kuota ndoto na kutenda

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni “donda ndugu” linalosababishwa na utafutaji wa aibu wa maslahi ya kiuchumi bila kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna umati mkubwa wa wanawake na wasichana wanaoendelea kutumbukizwa kwenye biashara ya ngono na ukahaba barabani; wanaoshinikizwa kujiuza barabarani na fedha inayopatikana, inachukuliwa na wafanyabiashara ya binadamu. Wasipoleta kile kiwango kinachotakia, cha moto wanakiona! Baba Mtakatifu anasema, haya ni matukio yanayotendeka kwenye barabara za majiji na miji mingi duniani, jambo ambalo watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kulitafakari kwa makini na hatimaye, kuchukua hatua stahiki. Hii ni kashfa dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuonesha uchungu na masikitiko yake makubwa na hivyo kuwataka viongozi wanaohusika kutenda kwa haraka, ili kuzuia na hatimaye, kukomesha biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo, unaodhalilisha na kuwatweza kwa namna mbaya zaidi wanawake na wasichana. Wanawake ambao ni waathirika wakuu wa biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo wanao mchango mkubwa katika mchakato wa kuleta mabadiliko katika sekta ya uchumi, ikiwa kama watajengewa utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Mwaka 2015 Siku ya sala na tafakari biashara haramu ya binadamu
Mwaka 2015 Siku ya sala na tafakari biashara haramu ya binadamu

Wanawake wenye umri kati ya miaka 24-54 wanachangia asilimia 90% ya nguvu kazi katika uzalishaji. Lakini takwimu zinazonesha pia kwamba, kuna wasichana asilimia 30% hawajui kusoma wala kuandika; na wengi wao hawana fursa za ajira. Itakumbukwa kwamba, “Talita Kum” ambao ni Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 sehemu mbalimbali za dunia, tarehe 8 Februari 2024 umeandaa Siku ya Sala na Tafakari kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, ukipewa ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kumbe kuna haja kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.

Mtakatifu Bakhita 2024
07 February 2024, 15:46