Tafuta

Liturujia Neno la Mungu Dominika 5 ya Mwaka B: Nguvu ya Sala Katika Huduma

Injili inawafunulia waamini kwamba, Yesu baada ya kuwa amewafundisha watu kule kwenye Sinagogi, anatoka ili Neno alilolitangaza na liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, na hatimaye, watu waweze kuona na kumshuhudia, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anayejishusha ili kuwaendelea waja wake, kuwatembelea katika makazi yao, kwani anapenda kuwaganga na kuwaponya na magonjwa pamoja na udhaifu wao wa kiroho na kimwili. Nguvu ya Sala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tano ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tarehe 4 Februari 2024 inamwonesha Kristo Yesu akidhihirisha uweza wake wa kuponya katika Sinagogi, anamponya pia mkwewe Petro aliyekuwa kitandani hawezi homa na aliwaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Kristo Yesu akatoka Kapernaumu akaenda akihubiri katika Masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya. Hii ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kristo Yesu kwani inazungumzia juu ya umuhimu wa Mungu pamoja na kutoa maswali juu ya imani ya Kanisa. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika ya tano ya Mwaka B wa Kanisa wakati wa tafakari kwenye Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Nguvu ya sala katika huduma
Nguvu ya sala katika huduma

Kristo Yesu alitoka ili kuwaendea binadamu waliojeruhiwa, ili kuwafunulia Uso wa Baba wa milele. Pengine katika sakafu ya nyoyo za waamini bado wanayo dhana ya Mungu ambaye yuko mbali sana na waja wake; Mungu ambaye ni mgumu wala hajiangaishi na matatizo yanayomkumba binadamu. Lakini, Injili inawafunulia waamini kwamba, Kristo Yesu baada ya kuwa amewafundisha watu kule kwenye Sinagogi, anatoka ili Neno alilolitangaza na kulishuhudia liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, na hatimaye, watu waweze kuona na kumshuhudia, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anayejishusha ili kuwaendelea waja wake, kuwatembelea katika makazi yao, kwani anapenda kuwaganga na kuwaponya na magonjwa pamoja na udhaifu wao wa kiroho na kimwili. Baada ya kushughuli zote hizi, Kristo Yesu, aliondoka na kwenda kusali, ili kuwabeba wote katika moyo wa Baba yake wa mbinguni. Sala inamkirimia tena nguvu ya kurejea tena ili kuwahudumia ndugu zake.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini

Baba Mtakatifu anawauliza waamini Je, katika safari yao ya imani, wamewahi kugundua kwamba, Kristo Yesu ni ndiye ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba, au bado wamebaki na mawazo mgando kuhusu Mwenyezi Mungu kwamba, yuko mbali na waja wake. Je, imani inawafanya waamini kuwa na wasi wasi au inawaachia faraja na utulivu wa ndani? Je, wanaposali wanahisi imani, au Neno la Mungu linawasukuma kutoka ili kwendaa kukutana na wengine, tayari kueneza faraja ya Mungu? Changamoto kubwa ya maisha ya kiroho ni kuachana na Mungu wanaye fikiri kwamba, wanamjua na hivyo kumgeukia kila siku, Mungu ambaye kila siku Kristo Yesu anawaletea katika Injili kama ufunuo wa Baba wa huruma na upendo, ili kukomaza imani na kamwe wasibaki kuwa ni Wakristo wa Sebuleni” bali wawe ni vyombo na mashuhuda wa tumaini la Mungu na uponyaji wake. Bikira Maria Mtakatifu sana, Mwanamke anayesafiri, awasaidie waamini kutoka katika ubinafsi wao ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu.

Nguvu ya Sala
04 February 2024, 14:37

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >