Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 8 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 8 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.  (Vatican Media)

Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mabalozi 2024: Amani Duniani

Papa tarehe 8 Januari 2024 amekutana na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya mapokeo ya kutakiana heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2023. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Diplomasia ya Vatican; Ujenzi wa Amani Duniani; Utendaji wa kiuchumi kijamii, na Ufalme wa Kristo Yesu; Biashara haramu ya silaha; Athari za Mabadiliko ya Tabianchi; Maabara ya Amani na Wakimbizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 8 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya mapokeo na utaratibu wa kutakiana heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2024. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Diplomasia ya Vatican; Ujenzi wa Amani Duniani; Utendaji wa kiuchumi kijamii, na Ufalme wa Kristo Yesu; Biashara haramu ya silaha; Athari za Mabadiliko ya Tabianchi; Maabara ya Amani; Wimbi kubwa la Wakimbizi na Wahamiaji; Miaka 75 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu na Ukoloni wa Kiitikadi; Majadiliano katika ukweli na uwazi; Elimu kwa vijana wa kizazi kipya; Akili Mnemba, AI; pamoja na Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 2025. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesema, “Familia ya Diplomasia” ya Vatican imeongezeka baada ya Sultani wa Omani kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican pamoja na kumteuwa Balozi wake wa kwanza na hivyo Vatican kwa sasa ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184. Vatican na Vietnam katika kipindi cha Mwaka 2023 vimekamilisha Mkataba kuhusu Mwakilishi wa Vatican nchini Vietnam, lengo ni kuendeleza mahusiano na ushirikiano kati ya Serikali ya Vietnam na Kanisa mahalia. Mwaka 2023 umeshuhudia kuridhiwa kwa Nyongeza ya Mkataba wa makubaliano wa tarehe 23 Septemba 1998 kati ya Vatican na Kazakhstan unao rahisisha utendaji wa wahudumu katika shughuli za kichungaji. Vatican pia imeafanya kumbukizi ya Miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia na Panama, Miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia Iran pamoja na miaka 60 na Jamhuri ya watu wa Corea sanjari na miaka 50 ya uhusiano ya kidiplomasia na Australia.

Familia ya Diplomasia ya Vatican ina jumla ya nchi 184
Familia ya Diplomasia ya Vatican ina jumla ya nchi 184

Baba Mtakatifu anasema amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu. Zawadi ya amani imesikika kutoka kwa Malaika, alipozaliwa Kristo Yesu na alipofufuka kwa wafu, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kutafuta, kuijenga na kuidumisha amani na kwamba, Vatican itaendelea kuwa ni sauti ya kinabii katika Jumuiya ya Kimataifa ili kuasha dhamiri za watu. Kunako tarehe 24 Desemba 1944, Papa Pio XII alizungumzia umuhimu wa kulinda na kudumisha amani ulimwenguni baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, kwa binadamu kupyaisha maisha kutoka katika undani wao. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata baada ya miaka 80 tangu Vita ya Pili ya Dunia ilipotokea, bado kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kielelezo cha Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu kwa masikitiko makubwa amekumbushia kuhusu shambulizi la kigaidi la tarehe 7 Oktoba 2023, chanzo cha vita kati ya Israeli na Palestina. Ni tukio ambalo lilipelekea zaidi ya watu 1, 139 kuuwawa kikatili, wengine wengi kujeruhiwa, kuteswa na kunyanyaswa na wengine kuchukuliwa kama mateka wa vita. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu analaani vitendo vyote vya kigaidi sanjari na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Vitendo hivi vya kigaidi vimepelekea Israeli kujibu mapigo, kiasi cha kusababisha Wapalestina wengi kupoteza maisha na uharibifu mkubwa Ukanda wa Gaza, bila kusahau mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu ametoa wito kwa pande zote zinazohusika na mgogoro kati ya Palestina, Israeli na Lebanon kuhakikisha kwamba, wanawaachia huru mateka na wafungwa wa kivita huko Ukanda wa Gaza. Misaada ya kiutu iruhusiwe kupelekwa kwenye maeneo ya Wapalestina na kwamba, ulinzi uimarishwe kwenye hospitali, shule na nyumba za Ibada. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha Israeli na Palestina zinatambulika kama Mataifa mawili na mji wa Yerusalemu utambulikane Kimataifa, ili Israeli na Palestina ziweze kuishi kwa amani na utulivu.

Amani ni zawadi ya Mungu inayomwajibisha binadamu
Amani ni zawadi ya Mungu inayomwajibisha binadamu

Nchi ya Siria ambayo imetumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu hadi sasa, hali ambayo imechangiwa pia na tetemeko la ardhi lililojitokeza Mwezi Februari 2023. Wananchi wa kawaida nchini Siria wanaendelea kuteseka kutokana na vikwazo vya kiuchumi. Baba Mtakatifu anasikitika kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaopata hifadhi nchini Yordan na Lebanon. Lakini hali ya uchumi na kisiasa inaendelea kugumisha maisha ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Lebanon itafanikiwa kumpata rais wake mapema iwezekanvyo. Baba Mtakatifu amegusia pia mateso ya watu wa Mungu nchini Myanmar. Anawashukuru viongozi wa Mongolia kwa mapokezi na ukarimu waliomtendea kiasi kwamba, hii ni nchini ya matumaini. Vita kati ya Urusi na Ukraine ikomeshwe kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimu na kuzingatia sheria za Kimataifa. Baba Mtakatifu anasikitishwa na hali tete kati ya Armenia na Azerbaigian na kuwatakatia hija njema itakayowawezesha kufikia suluhu ya amani na upatanisho; iwe ni fursa ya wakimbizi na wahamiaji kurejea tena kwenye makazi yao ya zamani, kwa kuheshimu nyumba za ibada. Hatua zote hizi zitawasaidia wananchi kuwa na imani, ili hatimaye, kuweza kufikia utulivu na amani, zawadi wanayoitamani sana. Akizungumzia kuhusu Bara la Afrika, Baba Mtakatifu anasema, kuna watu wanateseka kutokana na baa la njaa, umaskini na magonjwa, lakini kibaya zaidi ni baadhi ya nchi kutumbukia katika vita, vitendo vya kigaidi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi; mambo yanayokwamisha mchakato wa demokrasia kwa kukuza vitendo vya rushwa, hofu na madhulumu.

Makubaliano ya Amani Pretoria, Afrika ya Kusini
Makubaliano ya Amani Pretoria, Afrika ya Kusini

Makubaliano Amani kati ya Serikali ya Ethiopia na Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray, TPLF ya tarehe 2 Novemba 2022 huko Pretoria, Afrika ya Kusini: “Pretoria Peace Agreement of 2nd November 2022” yanaainisha hatua muhimu za kuwalinda raia, kuendelea kutolewa kwa huduma muhimu, kutolewa kwa misaada ya kiutu bila vikwazo na kuwawezesha wakimbizi wa ndani kurejea makwao pamoja, na kutekeleza dhamira ya serikali ya nchi hiyo ya kutengeneza sera ya haki. Sera hiyo inalenga kudumisha uwajibikaji, haki, ukweli, upatanisho na uponyaji. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ni wajibu wa pande zote mbili kuhakikisha kwamba, zinatekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Amani ya Pretoria, kwa kuendelea kujikita katika majadiliano, ili amani ya kweli na utulivu viweze kupatikana. Baba Mtakatifu amezitaja nchi za Cameroon, Msumbiji, DRC na Sudan ya Kusini ambako Baba Mtakatifu alibahatika kufanya hija ya kiekumene, ili kukazia pamoja na mambo mengine: haki, amani na upatanisho. Amerika ya Kusini hata kama hakuna vita ya moja kwa moja, lakini kuna machafuko ya hali ya hewa kama inavyojionesha: Venezuela, Guyana na Perù ambako kuna matukio yanayokwamisha mafungamano ya kijamii na mchakato wa demokrasia ya kweli. Machafuko ya kisiasa nchini Nicaragua yanaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu wa Mungu katika ujumla wake, lakini kwa namna ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki. Huu ni mwaliko wa kujikita katika majadiliano ya kidiplomasia, kwa kuheshimu ustawi, maendeleo na mafao ya waamini wa Kanisa Katoliki na wananchi katika ujumla wao. Katika vita, machafuko ya kisiasa na mipasuko ya kijamii, kuna watu wengi wanao endelea kuathirika na pengine kusahaulika. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, uvunjwaji wa sheria za Kimataifa ni uhalifu wa kivita unaopaswa kuzuiliwa usitendeke, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mpango wa Nyuklia wa Iran wa mwaka 2015
Mpango wa Nyuklia wa Iran wa mwaka 2015

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu kuhamasisha amani na kustawisha Jumuiya ya Kimataifa wanasema, kuna haja ya kuepukana na vita sanjari na kuzuia ukatili wa kivita. Mintarafu vita, yapo maafikiano ya Kimataifa yaliyotiwa saini na nchi nyingi; nayo hulenga katika kupunguza ukatili wa matendo ya kivita na matokeo yake. Maafikiano hayo yanahusu namna ya kuwatendea askari waliojeruhiwa au kutekwa na haya lazima yahifadhiwe na kutekelezwa ili kuzuia ukatili wa kivita na kuendelea kujikita katika sheria zinazothamini utu wa binadamu na kwamba, nchi inayo haki ya kujilinda. Madhara ya vita ni makubwa kwa watu na mali zao; ni chanzo cha baa la njaa linalosigina, utu, heshima na haki zao msingi; ni chanzo cha umaskini, utupu na vilema wengi. Rej. Gaudium et spes, 79. Kimsingi vita haina mafao kwa binadamu na kwamba, haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani yanayoondoa hali ya kuaminiana na kuendelea kukomba rasilimali ambazo zingetumika kwa ustawi na maendeleo ya watu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika usalama wa Kimataifa kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha hii inatumika katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; utunzaji wa mazingira bora nyumba ya wote sanjari na maboresho makubwa katika sekta ya uchumi, elimu na afya bora pamoja na kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu duniani kote. Mpango wa Nyuklia wa Iran wa Mwaka 2015, “JCPOA” ulifikiwa kati ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Pamoja na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi yanaendelea pia kuwatumbukiza watu wengi katika magonjwa, ujinga na umaskini wa hali na mali. 

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi
Madhara ya mabadiliko ya tabianchi

Baba Mtakatifu ametaja madhara makubwa yaliyosababishwa na matetemeko ya archi yaliyotokea Morocco na China; Uturuki na Siria; Maporomoko ya udongo yaliyotokea nchini Libya; pamoja na athari za mazingira zinazofanywa kwenye Ukanda wa Amazonia. Viwango vya joto duniani vikiwa vimeongezeka na kuvunja rekodi, na matukio ya kupindukia ya hali ya hewa yakileta madhara kwa binadamu duniani kote, mwaka huu mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, imekuwa ni fursa ya pekee ya kubadili mwelekeo na kuchochea hatua za kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi. COP28 ni mahali ambako dunia imethamini utekelezaji wa Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi, mkataba wa aina yake uliopitishwa kunako mwaka 2015 na kuweka mwelekeo wa kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya uzalishaji wa hewa ya ukaa, ili kulinda uhai wa binadamu. Takwimu zinaonesha kwamba, Mwaka 2023 ulikuwa na kiwango cha juu zaidi cha joto duniani kuliko miaka 174 iliyopita. Changamoto ya athari za mabadiliko ya tabianchi inahitaji uwajibikaji wa Jumuiya nzima ya Kimataifa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, makubaliano yaliyofikiwa COP28 yatasaidia kuleta mabadiliko ya kiikolojia kwa kujikita katika: Ufanisi wa nishati, vyanzo rafiki vya nishati, kuondoa kabisa matumizi ya vyanzo vinavyozalisha hewa ya ukaa; pamoja na kuwekeza katika elimu kuhusu mfumo bora zaidi wa maisha. Baba Mtakatifu amezungumzia pia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wanaohatarisha maisha kwa kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Hawa ni wale wanaotembea katika Jangwa la Sahara, kwenye Msitu wa Darièn ulioko mpakani kati ya Colombia na Panama, Mexico na Marekani, lakini zaidi ni wale wanaofariki dunia kwenye Bahari ya Mediterrania, ambayo inapaswa kuwa ni mahali pa watu kukutana, kutajirishana kati ya watu na tamaduni mbalimbali lakini kwa bahati mbaya, Bahari hii imegeuka kuwa ni kaburi lisilo na kielelezo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani
Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani

Baba Mtakatifu ametoa wito kwa Jumuiya ya Ulaya kufikia muafaka kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, kwa kutekeleza kwa vitendo “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018” unaopania pamoja na mambo mengine: Kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa! Mwanasayansi daima anapendelea kutumia vifupisho kama IVF akimaanisha mtoto ametengenezwa kwenye chupa ya kioo ikilinganishwa na njia ya asili. Ni neno linalotumika hususani kwenye matibabu ya ujuzi wa juu sana ambapo mtu binafsi anasaidiwa kutunga mimba kwa kuchanga mbegu za kiume (manii) na yai la mwanamke nje ya mfuko wa uzazi. Na baada ya hapo upandikizaji wa kiinitete ndani ya tumbo la kuruhusu mimba. Inachukua wiki mbili kabla ya kujua kama zoezi hilo limefanikiwa au la kwa kufanya kipimo cha ujauzito kutumia njia ya mkojo ila sana sana madaktari wanapendelea kipimo kwa njia ya damu. Baba Mtakatifu anasema, vitendo hivi ni kupandikiza utamaduni wa kifo na udhalilishaji wa wanawake kwa sababu za kiuchumi. Baba Mtakatifu anatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kupiga rufuku vitendo kama hivi, kwa sababu mtoto daima ni zawadi kutoka kwa Mungu na wala si kichokoo cha mkataba.

Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote
Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote

Tamko la Haki za Binadamu Duniani (The Universal Declaration of Human Rights, 1948, UDHR) lilitiwa mkwaju tarehe 10 Desemba 1948 na Mataifa yalikubaliana kulinda haki msingi za binadamu hasa haki ya kuishi ambayo ndiyo msingi wa haki nyingine zote. Tamko hili la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2023 linaadhimisha Miaka 75 tangu kuridhiwa kwake na Jumuiya ya Kimataifa. Tamko hili ni matokeo ya tafakari ya kina iliyofanywa na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu: Athari zilizokuwa zimesababishwa na Vita kuu ya kwanza na ile ya Pili ya dunia; ambapo kuna watu wengi walipoteza maisha na mali; utu na heshima yao vikawekwa rehani. Walitaka kuweka kanuni msingi ambazo zimengefuatwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hizi ni haki ambazo zinafumbatwa katika uhuru, haki na amani duniani. Huu ni urithi wa binadamu wa nyakati zote na mahali pote bila ubaguzi, kwani zinapata chimbuko lake kutoka kwa binadamu mwenyewe aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba ni sehemu ya asili ya binadamu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, nadharia ya jinsia ni hatari kabisa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani inapania kufuta tofauti msingi kati ya mwanaume na mwanamke na kwamba, huu ni ukoloni wa kiitikadi unaoendelea kusababisha donda kuu pamoja na kuyagawa Mataifa, badala ya kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani duniani. Kumbe majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ndio yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika Jumuiya ya Kimataifa, ili kulinda na kudumisha haki, amani na kwamba, taasisi zilizopewa dhamana ya kulinda na kudumisha amani zitekeleze vyema malengo yake. 

Mkataba wa Ijumaa kuu: Amani ya Kudumu
Mkataba wa Ijumaa kuu: Amani ya Kudumu

Uingereza na Ireland ya Kaskazini mwaka 2023 zimeadhimisha kumbukizi ya miaka 25 ya Mkataba wa Ijumaa Kuu (Good Friday Agreement) yaliyokuwa makubaliano ya amani ambayo kwa kiasi kikubwa yalimaliza miongo mitatu ya ghasia ambazo ziliisumbua Ireland Kaskazini tangu mwishoni mwa miaka ya 1960. Ilitiwa saini Aprili 10, 1998, na kusimamiwa kwa sehemu na Serikali ya Marekani ya Rais wa wakati huo Bill Clinton. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mkataba wa Ijumaa Kuu ni mfano bora wa kuigwa kwa waamini kujiaminisha katika mchakato wa amani, licha ya matatizo na changamoto zilizomo! Mwaka 2024 ni mwaka ambao unashuhudia nchi nyingi zikifanya chaguzi ili kuimarisha demokrasia na ushiriki wa wananchi katika maamuzi na ni muhimu kwa vijana wa kizazi kipya watakaoshiriki kwa mara ya kwanza katika chaguzi hizi watambue kwamba, wanawajibika barabara. Ikumbukwe kwamba, Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi. Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kumbe, wanasiasa watambue kwamba, wanatekeleza huduma ya upendo wa hali ya juu kabisa kwa jirani na Jumuiya iliyowachagua. Ujenzi wa njia ya amani unaimarishwa kwa njia ya majadiliano ya kidini yanayopania pamoja na mambo mengine kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, ambao kwa sasa unakabiliana na changamoto nyingi. Misimamo mikali ya kidini na vitendo vya kigaidi vimekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa amani, mashambulizi ya nyumba za ibada na sanaa na hata kwa kiasi kikubwa kuingilia demokrasia ya nchi. Wakati mwingine, mashambulizi haya yametumika kama sehemu ya wongofu wa shuruti, kuvuruga demokrasia na kutafuta fedha kwa nguvu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la chuki dhidi ya Wayahudi kwa miaka ya hivi karibuni. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika elimu, ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ukarimu na upendo. Dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo zimeongezeka maradufu, kiasi cha hata kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kuna zaidi ya Wakristo milioni 360 wanao nyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, wengine wamelazimika kuzikimbia nchi zao kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Ili kudumisha haki na amani  kuna haja ya kuwekeza kwa vijana
Ili kudumisha haki na amani kuna haja ya kuwekeza kwa vijana

Ujenzi wa amani unajikita katika elimu, kwa kuwekeza katika vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anasema bado anayo kumbukumbu hai ya Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia ulikuwa ni wimbo wa amani na ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano na kwamba, unavuka mipaka ya vita na kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga ushirika katika utofauti. Hii ni changamoto pia ya kuhakikisha kwamba, kanuni maadili na utu wema unatumika barabara ili kuondokana na habari za kughushi. Maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace: Au “Akili Mnemba na Amani.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa akili mnemba: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye ni changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa. Baba Mtakatifu anasema teknolojia ya akili mnemba ni kati ya changamoto changamani kwa miaka ijayo. Ni muhimu kwamba maendeleo ya kiteknolojia yafanyike kwa njia ya kimaadili na ya uwajibikaji, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kukazia utu wa ndani unaowaunganisha binadamu wote na kuheshimu haki ya kuchangia ili kuleta na kukoleza amani. Kwa hivyo, tafakari ya uangalifu inahitajika katika kila ngazi, kitaifa na kimataifa, kisiasa na kijamii, ili maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba yabaki kwenye huduma ya mwanadamu, kwa kutia moyo, kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya watu, ujenzi wa roho nzuri na udugu wa kibinadamu pamoja na fikra zenye uwezo wa utambuzi.

Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu ilindwe
Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu ilindwe

Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2024. Kumbe huu ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Mama Kanisa anaona umuhimu wa kuadhimisha Jubilei kutokana na mahangaiko na mateso makubwa yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo; kuwatengenezea vijana mazingira ya kuwa na ndoto ya matumaiani; kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Jubilei ni kipindi cha neema na baraka ili kuona huruma, upendo na msamaha wa Mungu; upatanisho unaovuka ukosefu wa haki!

Diplomasia 2024

 

08 January 2024, 15:11