Tafuta

2023.12.17 Papa amefikisha miaka 87 ya kuzaliwa kwake. 2023.12.17 Papa amefikisha miaka 87 ya kuzaliwa kwake.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe kutoka Makanisa kumpongeza Papa kwa miaka 87

Baba Mtakatifu amepokea Ujumbe wa matashi mema wa kufikisha miaka 87 ya kuzaliwa kutoka makanisa mbali mbali kuanzia na Jimbo Kuu la Roma,Baraza la maaskofu katoliki Italia (CEI) na wakuu wa Nchi kama Rais Mattarella wa Italia.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Dominika tarehe 17 Desemba 2023, Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu katika siku yake ya kuzaliwa. Kati ya ujumbe mwingi ulifika  kutoka Jimbo Kuu la Roma, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia (CEI), Rais wa Jamhhuri ya Italia na wengine. Kutoka Vikarieti ya Roma inbainisha kuwa: “Katika siku yako ya  miaka 87 ya kuzaliwa tunayo sababu nyingi za kusherehekea na kushukuru kwa maisha yako na mafundisho yako, zawadi ya kweli na chemchemi ya matumaini kwa Kanisa na kwa wanadamu wanaosumbuliwa na migawanyiko, vita na magonjwa ya milipuko. Kama jumuiya ya jimbo tunatuma salamu za joto kwa Mchungaji wetu na kumkumbuka kwa upendo wa kinugu katika novena hii ya Noeli: tunaomba kila baraka kutoka kwa Bwana kwa ajili yako na kwa ajili ya huduma unayofanya katika Kanisa letu la Roma na ulimwenguni.”

Papa akisalimiana na  na mikumbatio ya watoto
Papa akisalimiana na na mikumbatio ya watoto

Na kutoka kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Italia kwa niaba ya Maaskofu wote, ameandika Barua kwa Papa Francisko katika siku yake ya kuzaliwa. Barua hiyo inaanza na kifungu cha kiinjili kisemajo: “Nafsi yangu yamtukuza Bwana, na roho yangu inamfurahia Mungu mwokozi wangu, kwa sababu ameutazama unyenyekevu wa mtumishi wake” (Lk 1:46-48). Baba Mtakatifu, katika siku yako ya kuzaliwa tunainua wimbo wa sifa wa Magnificat pamoja na jumuiya zetu kutoa shukrani na kutuma mawazo ya upendo kwako. Kwa mafundisho yako na kwa ishara zako za kila siku unatualika kwenye uongofu, kuacha uhakika tulioupata, ili kurudi kwenye kumtumaini Mungu na wengine. Kwa sababu hiyo ni muhimu kufuata njia za maombi na huduma. Hakuna upinzani, lakini maelewano. Huu ndio mzizi wa hatua yetu. Ni Injili ya furaha!"

Papa amesalimiana na watoto
Papa amesalimiana na watoto

Baraza la Maaskofu Italia aidha wanabainisha kuwa: "katika wakati huu ambapo ubinadamu wote unateseka na janga vurugu, tunakusanyika karibu nawe, tukiomba zawadi ya amani. Tunaamini kwamba hii inaweza kuwa zawadi bora kutoka kwa Makanisa yetu. Tunataka kuwa mafundi wa amani pamoja nawe ili kukabiliana na utamaduni wa vita, chuki, ujinga na ubaguzi. Ni vigumu kubeba upumbavu wa migogoro mingi ambayo inamwaga damu maeneo yote ya sayari, na kusababisha maumivu, taabu na umaskini. Ni watu wangapi wanalazimika kuacha nyumba zao! Ni wangapi wanaendelea kupoteza maisha katika Mediterania! Ni wangapi ambao bado wanateseka na udanganyifu wa maisha bora ya baadaye na badala yake wameishia kwenye utumwa!

Rais wa CEI akwa niaba ya  Maaskofu wote anabainisha kuwa: “Leo, zaidi ya hapo awali, kukemea uovu inakuwa dhamira thabiti ya kuwa Kanisa mama, lenye upendo na ukaribishaji. Tunataka kutoa mabembelezo ya faraja kwa nyuso zilizo na alama ya mateso, kwa wale wanaoishi pembezoni, kwa wale waliotupwa na wasiosikilizwa. Na pamoja na Maria tunataka kuimba wimbo: “Amewaangusha wenye nguvu katika viti vyao vya enzi, amewainua wanyenyekevu; amewashibisha wenye njaa vitu vyema, matajiri amewafukuza mikono mitupu” (Lk 1:52-53). Kwa kuhitimisha maaskofu wa Italia waandika kuwa: “katika siku hii ya maadhimisho, tunatumaini unahisi shukrani za Makanisa yetu. Na kwa kutenda kama wasemaji wa jumuiya zote za kikanisa nchini Italia, tunaitikia kwa hiari mwaliko wako usiokoma wa kutosahau kukuombea. Tunakutakia heri kutoka mioyoni mwetu Baba Mtakatifu.”

Papa awasalimia watoto
Papa awasalimia watoto

Kwa upande wa Ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Italia, Bwana Sergio Mattarella anaandika kuwa: “Katika hafla ya siku yako ya kuzaliwa ya themanini na saba, kwa niaba ya watu wa Italia na mimi, matakwa ya dhati na ya upendo ya ustawi na mwendelezo mzuri wa Majisterio yako yenye matunda yanakufikia. Katika ulimwengu ambao, kwa bahati mbaya, mashindano mapya yanaongezwa kwa migogoro isiyoisha, hatua yako ya kichungaji isiyokwisha inaendelea kuwakumbusha kila mtu haja ya kujenga ufumbuzi wa kurejesha amani kwa kumweka mtu na heshima yake isiyoweza kuondolewa katikati ya  hatua za jumuiya ya kimataifa." Bwana mattarella vile vile anabainisha kuwa: "Ombi lako la mara kwa mara na la kutoka moyoni la kuanzisha tena uhusiano wa heshima na mazungumzo katika jamii zetu unajumuisha upeo wa juu wa maadili kwa wanawake na wanaume wote na wenye mapenzi mema. Vile vile mwaliko huo ulifanywa upya na wewe wakati wa ziara zako za  kitume Afrika, Ulaya na Asia - pamoja na uingiliaji kati wa COP28 - ili usawa sahihi uimarishwe kati ya Mwanadamu na Asili, na kuacha mantiki ya upotevu kwa neem ya uchaguzi thabiti na jumuishi ambao unapendelea manufaa ya pamoja ya kimataifa.

Wakati wa sarakasi kwa ajili ya watoto
Wakati wa sarakasi kwa ajili ya watoto

Kama ambavyo umesisitiza mara nyingi, kila mmoja wetu, kulingana na jukumu na uwezo wetu, anaitwa kujihusisha katika kuelewana na katika mazoezi madhubuti ya udugu wa kibinadamu, bila kujali tofauti za utaifa, hali ya kijamii na kiuchumi au uhusiano wa kidini." Rais Mattarrella aidha amesisitiza  kuwa: “Ninaamini kwamba ujumbe wa hali ya juu ambao utauhutubia ulimwengu kwa ajili ya ukumbusho muhimu wa Kuzaliwa kwa Yesu utaleta faraja kwa wale wanaoteseka kutokana na migogoro, kuanzia “Ukraine iliyoteswa na Mashariki ya Kati, ambapo hitaji la kutozima matumaini linahitajika. Kwa matakwa haya ninarudia kukutakia  heri njema kwa siku yako ya kuzaliwa na siku kuu njema zinazokuja."

Ujumbe kutoka makanisa na Rais Mattarella kwa Papa
17 December 2023, 11:38