Tafuta

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lililotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 18 Desemba 2023 Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lililotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 18 Desemba 2023   (Vatican Media)

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa "Fiducia Supplicans" Yaani "Kuomba Baraka Kwa Imani"

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lilijadiliwa katika mkutano wa Baraza na hatimaye, Papa akaridhia lichapwe kwa kuweka saini yake tarehe 18 Desemba 2023. Tamko hili linajadili: Baraka katika Sakramenti ya Ndoa, Maana ya baraka katika Maandiko Matakatifu, Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji, nani anaweza kuomba baraka. Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lililotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 18 Desemba 2023 baada ya kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko limepokelewa kwa hisia tofauti kinyume cha lengo la Tamko lenyewe. Baba Mtakatifu Francisko akijibu mashaka ya Makardinali “Dubia” waliomwandikia kuelezea wasiwasi wao kuhusu masuala makuu matano huku wakiomba tafsiri kuhusiana na: Ufunuo wa Kimungu, juu ya baraka kwa ndoa za watu wa jinsia moja; Kuhusu Sinodi kama mwelekeo wa Kisheria wa Kanisa; Juu ya Upadrisho wa wanawake ndani ya Kanisa Katoliki na juu ya Toba kama sharti la lazima kwa ajili ya msamaha unaotolewa kwenye Sakramenti ya Upatanisho. Mashaka Kuhusu baraka za ndoa ya watu wa jinsia moja Baba Mtakatifu anasema, Ndoa ya Kikristo kama sura inayoakisi muungano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake, inatekelezwa kwa utimilifu katika muungano kati ya mwanaume na mwanamke wanaojitoa mmoja kwa mwenziye kwa upendo ulio huru, wenye uaminifu na wa kipekee, ambamo kila mmoja anakuwa ni mali ya mwenzake hadi kufa, na wanakuwa radhi kuendeleza uzao, tena wamewekwa wakfu kwa Sakramenti inayowaletea neema ya kuwa Kanisa la nyumbani na kuwa chachu ya maisha mapya kwa jamii. Hii ndio maana ya Ndoa ya Kikristo na wala si vinginevyo! Rej. Amoris laetitia 292. Pamoja na msimamo huu wa Kanisa, lakini pia upendo wa kichungaji unapaswa kuoneshwa kwa kujikita katika: uelewa, uvumilivu, huruma na ujasiri bila kuwahukumu waamini wengine kuwa ni wadhambi!

Kiini cha Ndoa ya Kikristo ni maagano na mafao ya watoto
Kiini cha Ndoa ya Kikristo ni maagano na mafao ya watoto

Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lilijadiliwa katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, likapelekwa kwa Baba Mtakatifu na hatimaye, akaridhia lichapwe kwa kuweka saini yake tarehe 18 Desemba 2023. Tamko hili linajadili kwa kina na mapana kuhusu: Baraka katika Sakramenti ya Ndoa, Maana ya baraka katika Maandiko Matakatifu, Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji, nani anaweza kuomba baraka. Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge” na watu wa ndoa za jinsia moja. Kanisa ni Sakramenti ya upendo wa Mungu. Watu wa Mungu wenye imani thabiti wanaweza kupokea baraka za Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ni kielelezo cha baraka kuu kutoka kwa Mungu, baraka ambayo ni chemchemi ya wokovu. Baraka katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Muungano huo wa mume na mke na manufaa ya watoto wao huwataka wawe na uaminifu kamili kati yao. Kwa asili yake ndoa na mapendo ya wenye ndoa yamewekwa kwa ajili ya kuzaa watoto na kuwalea; nao ni taji yao. Kwa kweli watoto ni zawadi kuu ya Ndoa na tunu kubwa ya wazazi wenyewe. Haya ndiyo Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na kamwe hayawezi kubadilishwa. Wakati wa kutoa baraka, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba halichanganyi madhehebu ya kutoa baraka, ili kusitokee mkanganyiko na kwamba, Kanisa halina mamlaka ya kutoa baraka kwa watu wa ndoa za jinsia moja.

Waamini wanaoomba baraka ndani ya Kanisa wanapaswa kuwa waaminifu
Waamini wanaoomba baraka ndani ya Kanisa wanapaswa kuwa waaminifu

Maana ya baraka mbalimbali zinazotolewa na Mama Kanisa. Kimsingi ili kupata baraka inatakiwa mwamini kutekeleza mapenzi ya Mungu kama yanavyofafanuliwa na Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Wapokeaji wakuu wa baraka ni watu, vitu vitakatifu, visakramenti, mahali pa maisha, kazi; mateso na mahangaiko, matunda ya kazi ya mikono ya wanadamu pamoja na mahangaiko yake; kazi ya uumbaji inayofanya rejea yake kwa Mwenyezi Mungu, Muumba kwa kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Sala za baraka mbalimbali zinazotolewa zinalenga kumpatia Mungu utukufu na kuomba upendeleo pamoja na kudhibiti nguvu za giza. Kumbe, kwa waamini wanaoomba baraka kupitia kwa Kanisa wanaalikwa kuwa imara katika imani, na kuendelea kumwamini, kumpenda sanjari na kutekeleza amri zake, ndiyo maana Kanisa daima linamtukuza Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu mintarafu roho ya Injili. Huu ndio uelewa wa baraka kiliturujia. Ili baraka iweze kutolewa haina budi kuendana na mapenzi ya Mungu. Kumbe, baraka inatolewa na Mama Kanisa kwa wanandoa wanaokidhi masharti ya ndoa kimaadili na wale si vinginevyo! Lakini pia, waamini wanapaswa kuwa na uelewa mpana zaidi wa maana ya baraka inayofumbatwa katika upendo wa kichungaji unaopaswa kutawala na kuongoza maamuzi pamoja mitazamo ya waamini na hivyo kuepukana na mtindo wa waamini kuwa ni Mahakimu wanaokatalia, kataza na kuwatenga watu. Baraka katika Maandiko Matakatifu ni kama ile Kanuni ya baraka inayooneshwa kwenye Kitabu cha Hesabu “BWANA akubariki, na kukulinda; BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.” Hes 6:24-26. Aina nyingine ya baraka ni ile inayoonesha kwamba, Mungu ni upendo: “Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote.” Zab 103:1.

Kuna aina mbalimbali za baraka jambo la msingi ni imani.
Kuna aina mbalimbali za baraka jambo la msingi ni imani.

Kumbe katika Maandiko Matakatifu kuna aina mbalimbali za baraka ya: familia, jumuiya; baraka ya sifa na utukufu wa Mungu; baraka ya Kristo Yesu kwa watoto. Ni katika fumbo la upendo, kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu anawasiliana na Kanisa lake na kulipatia nguvu ya kubariki na hivyo baraka inageuzwa kuwa ni nguvu shirikishi, mshikamano na ujenzi wa amani. Baraka zinaonesha huruma na upendo wa Mungu, mwaliko kwa watoto wa Kanisa kuwa na mwelekeo kama huo kwa jirani zao. Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji unajikita katika huruma na upendo wa Mungu na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu inayopata chimbuko lake kutoka katika huruma ya Mungu na inawasaidia waamini kusonga mbele, kuishi vyema zaidi na kujibu utashi wa Mungu katika maisha yao. Mtu anayeomba baraka, ana imani kwa Mwenyezi Mungu na wala hajiamini katika uweza wake mwenyewe ndiyo maana anakimbilia uweza na nguvu ya Mungu; uaminifu kwa Mungu ni chanzo cha neema na baraka. Uelewa wa baraka katika muktadha wa kichungaji unapaswa kueleweka kuwa ni Ibada nje ya Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti za Kanisa na kamwe Ibada hizi zisiwe na mwelekeo wa Kiliturujia. Upendo wa kichungaji unawataka viongozi wa Kanisa kuwa makini na kamwe wasiwahukumu. Mwenyezi Mungu ndiye anaye bariki na mwanadamu pia amepewa uwezo wa kubariki na hata wadhambi bado wanaendelea kuwa ni Watoto wa Mungu. Kuna matukio ambayo kwayo waamini wanaomba baraka: wanapokuwa katika hija, kwenye madhabahu au wanapokutana na Padre barabarani. Kuna baraka kwa ajili ya wagonjwa, wazee, wasafiri, makundi ya watu wa kujitolea pamoja na vyama vya kitume. Hizi ni baraka kwa ajili ya wote na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kukatazwa asizipokee. Wakleri wanaweza kushiriki katika sala za watu wanaotamani kujiaminisha kwa huruma ya Mungu, kwa kuomba msaada wake, ili aweze kuwaongoza.

Kuna aina mbalimbali za baraka
Kuna aina mbalimbali za baraka

Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge” na watu wa ndoa za jinsia moja: Wakleri wanaweza kuwabariki watu wenye ndoa tenge na ndoa za jinsia moja kwa kutambua ukuu, huruma na msamaha wa Mungu unaowatajirisha, ganga na kuwaponya na hivyo kuinuliwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Na katika mwelekeo huu uaminifu kwa Injili hauna budi kukua, ili kuwasaidia kuondokana katika hali ya dhambi na hivyo kuongeza upendo wao kwa Mungu. Neema ya Mungu inatenda kazi kwa wale wanaojitambua kwa unyenyekevu kuwa ni wadhambi na wanahitaji kuonja huruma na upendo wa Mungu. Mbegu hii ya Roho Mtakatifu inapaswa kukuzwa na kuendelezwa na wala isikwamishwe. Liturujia ya Kanisa inawaalika waamini, licha ya dhambi na unyonge wao wanaweza kukimbilia huruma na msamaha wa Mungu. Kumbe, Wakleri wanahimizwa kutoa baraka hata kama hazionekani katika Vitabu vya Baraka, ili kunogesha uaminifu wa watu wa Mungu na kuwasindikiza katika maisha yao na kwamba, utaratibu huu hauwezi kugeuzwa na kuwa kama Sheria. Watu wenye “ndoa tenge” na watu wa ndoa za jinsia moja wanaweza kupata baraka kwa kuwaombea: amani, afya njema, moyo wa uvumilivu, majadiliano, moyo wa kusaidiana pamoja na mwanga na nguvu za Mungu, ili iwasaidie kutekeleza mapenzi yake kwa ukamilifu zaidi. Jambo la msingi ni kuepuka makwazo, Mapadre wanapotoa baraka hizi na kamwe baraka hizi zisifanane na zile zinatolewa kwenye Sakramenti ya Ndoa Takatifu.

Baraka ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Baraka ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kanisa ni Sakramenti ya upendo wa Mungu: Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu mwenye rehema kwani Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu. Rej. Ebr 5:7. Mama Kanisa anatenda sit u katika upendo, mifano na kazi za toba, bali pia kwa njia ya jumuiya ya waamini kutekeleza utume wa Kimama wa kuzirejesha nyoyo za waamini kwa Kristo Yesu. Kanisa ni Sakramenti ya upendo mkamilifu wa Mungu, hata pale mwamini anapokuwa ameelemewa na dhambi, bado anaweza kuomba baraka, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro aliokuwa anazama baharini akamwomba, Kristo Yesu aweze kumwokoa. Kutoka katika kiini hiki cha msingi, kinachong’ara ni uzuri wa upendo wa Mungu unaookoa, uliodhihirishwa katika Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Rej. Evangelii gaudium, 36. Kila baraka inayotolewa ni fursa ya kutangaza na kushuhudia Injili, yaani “Kerygma” tayari kukaribia upendo wa Kristo Yesu katika maisha. Kanisa ni chombo cha baraka ya Mungu kwa kumpokea Kristo Yesu na hivyo kumtangaza. Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na amani. Ulimwengu unahitaji baraka, kumbe, waamini wanaweza kutoa na kupokea baraka. Watambue kwamba, Baba wa mbinguni anawapenda, jambo la msingi ni wao kuwa na furaha ya baraka kutoka kwake, furaha ya kumshukuru na kuendelea kujifunza kutoka kwake ili kutoa baraka, ili watu waweze kung’amua kwamba, ndani ya Kanisa waamini wote ni mahujaji, wahitaji, lakini wanapendwa licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu na kwamba, wanabarikiwa!

Tamko Kuomba Baraka
19 December 2023, 13:48