Tafuta

2023.12.03 Kardinali Parolin, Katibu wa Vatican akiwa anasoma ujumbe wa Papa katika COP 28 huko Dubai. 2023.12.03 Kardinali Parolin, Katibu wa Vatican akiwa anasoma ujumbe wa Papa katika COP 28 huko Dubai. 

Papa:Kulinda amani pia ni kazi ya dini pamoja na mazingira

Kardinali Parolin,Katibu wa Vatican amesoma ujumbe wa Papa wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya "Faith Pavillon"huko Dubai,kama sehemu ya Cop28:Papa amejikita juu ya uharaka wa kuchukua hatua kwa ajili ya mazingira:“janga la tabianchi pia ni ya kidini.Haitoshi kutumia rasilimali zaidi,tunahitaji kuelimisha maisha ya kiasi na ya kindugu.Na "kulinda amani pia ni kazi ya dini na sio kwa maneno tu bali kuwa sehemu dhidi ya chuki."

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tukio la uzinduzi wa Banda la Imani, kama sehemu ya Mkutano wa COP28 kwenye maonesho ya Jiji la Dubai, yaliyohamasishwa na Baraza la Wazee wa Kiislamu, Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa(UNEP) na washirika wengine katika lengo kuu la kuwa ishara inayoonekana ya ushirikiano na kujitolea kati ya dini kwa ajili ya hatua zinazofaa za tabianchi, Kardinali Pietro Parolin,Katibu wa Vatican, tarehe 3 Desemba 2023, amesoma ujumbe wake. Katika ujumbe huo anaanza kumshukuru Dr. Ahmad Al-Tayyeb, Imam Mkuu wa Al-Azhar, ambaye alimuonesha ukaribu wake; Baraza la Wazee wa Kiislamu, ambao alikutana nao mwaka mmoja uliopita, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) na washirika wote walioandaa na kuendeleza banda hili la kidini. Ni la kwanza la aina yake katika moyo wa COP na linaonesha kwamba kila imani ya kweli ya kidini ni chanzo cha kukutana na kuchukua hatua.

Mkutano

Baba Mtakatifu anabainisha kuwa kwanza kabisa, mkutano. Ni muhimu kujikuta sisi wenyewe, zaidi ya tofauti zetu, kama kaka na dada katika ubinadamu, na zaidi ya yote kama waamini, tujikumbushe sisi wenyewe na ulimwengu kwamba, kama mahujaji wanavyongoja katika nchi hii, tunatakiwa kulinda makao yetu ya pamoja. Dini, kama dhamiri za ubinadamu, zinatukumbusha kuwa sisi ni viumbe wenye ukomo, wanaokaliwa na hitaji la kutokuwa na mwisho. Ndiyo, sisi ni watu wa kufa, tuna mipaka, na kulinda uhai pia kunamaanisha kupinga upotovu wa uweza wa nguvu unaoharibu sayari.

Baba Mtakatifu anafafanua kuwa “Inatokea wakati mwanadamu anapojiona kuwa bwana wa ulimwengu; wakati, akiishi kana kwamba Mungu hayupo, anajiachia atekwe na mambo yanayopita. Kisha mwanadamu, badala ya kuwa na teknolojia katika uwezo wake, anajiruhusu kutawaliwa nayo, "anajitengenezea" mwenyewe na anakuwa asiyejali: hawezi kulia na kuhurumia, anabaki peke yake na, akiinuka juu ya maadili na busara, anafikia kuharibu hata kile kinachomruhusu kuishi. Ndiyo maana janga la hali ya tabianchi pia ni janga la kidini: kwa sababu mzizi wake upo katika dhana ya kujitosheleza kwa kiumbe. Lakini "kiumbe [...] bila Muumba hutoweka" (rej. Gaudium et spes, 36). Banda hili kwa maana hiyo  liwe mahali pa kukutania na dini ziweze kuwa "mahali pa ukarimu" ambapo, kwa unabii unaoshuhudia hitaji la upitaji mipaka, huzungumze na ulimwengu wa udugu, heshima na kujali kila mmoja, bila kuhalalisha kwa njia yoyote unyanyasaji wa kazi ya uumbaji. (rej.Hati juu ya Udugu wa Kibinadamu kwa ajili ya Amani ya Dunia na Ushirikiano wa Pamoja, Abu Dhabi, 4 Februari 2019).”

Hatua za haraka zichukuliwe

Katika hiyo, Baba Mtaktifu kwenye ujumbe huo amesema “inatuleta kwenye mada nyingine muhimu ya banda hili ni hatua ya imani ya kidini:Kwa sababu  ni haraka kuchukua hatua kwa ajili ya mazingira, lakini haitoshi tu kutumia rasilimali zaidi za kiuchumi: njia ya maisha lazima ibadilishwe na kwa hiyo ni muhimu kuelimisha katika maisha ya kiasi na ya kindugu. Ni hatua muhimu kwa dini, ambazo pia zinaitwa kuelimisha katika kutafakari, kwa sababu uumbaji sio mfumo tu wa kuhifadhiwa, lakini  ni zawadi ya kukaribishwa”. Na dunia maskini katika kutafakari itakuwa dunia iliyochafuliwa katika nafsi, ambayo itaendelea kutupa watu na kuzalisha ubadhirifu; ulimwengu usio na maombi utasema maneno mengi lakini, bila huruma na machozi, utaishi tu juu ya kupenda mali iliyotengenezwa kwa pesa na silaha.

Kulinda amani pia ni kazi ya dini

Baba Mtakatifu amekazia kusema kuwa “katika suala hili, tunajua jinsi amani na usimamizi wa kazi ya uumbaji unavyotegemeana: ni wazi kwa wote kuona jinsi vita na migogoro inavyoharibu mazingira na kugawanya mataifa, kuzuia ahadi ya pamoja kwa masuala ya kawaida, kama vile kulinda sayari. Kiukweli, nyumba inaweza kuishi kwa kila mtu ikiwa hali ya amani tu imeanzishwa ndani. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Dunia yetu, ambayo udongo wake unaonekana kuungana na kilio cha watoto na maskini kufanya ombi moja kufikia mbinguni: amani! Kulinda amani pia ni kazi ya dini. Tafadhali kusiwe na kutofautiana katika hili.” Papa amekazia.

Onyo la wachochea vurugu

Papa aidha amesema Msikatae na ukweli kile mnachosema kwa midomo yenu: msijiwekee kikomo katika kuzungumza juu ya amani, lakini kuchukua msimamo wazi dhidi ya wale ambao, kwa kujitangaza kuwa waamini, wanachochea chuki na hawapingi vurugu. Katika hilo, Papa amebainisha kuwa “Ninakumbuka maneno ya Fransis wa Assisi: “Amani mnayoitangaza kwa vinywa vyenu, iweni nayo kwa wingi zaidi mioyoni mwenu” (rej. Historia ya Ndugu watatu, XIV,5: FF 1469).” na kwa kuhitimisha ujumbe wake, Baba Mtakatifu amebainisha kuwa, “Mwenyezi Mungu aibariki mioyo yetu ili kwa pamoja tuwe wajenzi wa amani na walinzi wa viumbe. Asante.”

Ujumbe wa Papa kwa COP28 uliosomwa na Kardinali Parolin wakati wa uzinduzi wa Banda la Imani
03 December 2023, 16:02