Tafuta

Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 11 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi kutoka Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Vatican. Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 11 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi kutoka Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Vatican.  (Vatican Media)

Papa Azungumza na Wafanyakazi wa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Vatican

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 11 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi kutoka Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Vatican na kukazia mambo makuu mtatatu: Uhuru wa ofisi, sheria na kanuni za Kimataifa pamoja na taaluma. Baba Mtakatifu anasema, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Vatican inajitegemea, kumbe inapaswa kuwajibika kwa kunogeshwa na karama ya upendo; kwa kusahihishana, kukosoana na kurekebishana kidugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Februari 2014 alichapisha Barua Binafsi ijulikanayo kama “Fidelis dispensator et prudens” yaani “Wakili Mwaminifu na Mwenye Busara” Lk 12:42, iliyoanzisha kitengo cha Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Vatican kinachoratibu mambo ya uchumi na utawala mjini Vatican kama sehemu ya mageuzi makubwa yaliyokua yameanzishwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI na hatimaye kufanyiwa marekebisho na Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 11 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi kutoka Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Vatican na kukazia mambo makuu mtatatu: Uhuru wa ofisi, sheria na kanuni za Kimataifa pamoja na taaluma.

Papa akutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
Papa akutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Vatican inajitegemea, kumbe inapaswa kuwajibika kwa kunogeshwa na karama ya upendo; kwa kusahihishana, kukosoana na kurekebishana kidugu, hata kama wanapaswa kutoa taarifa kwa matukio ya fedha na mambo ambayo yanakwenda kinyume cha sheria, taratibu na kanuni kama Neno la Mungu linavyofundisha “Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.” Mit 3:12. Mchakato wa kurekebishana kidugu unasimikwa katika maneno yafuatayo: upendo na masahihisho ya kibaba bila kutumbukia kwenye kishawishi cha kutaka kujifanya kuwa ndiye mhusika mkuu. Wakumbuke ari na moyo wa Kisinodi pamoja na kujenga na kudumisha ushirikiano na ofisi nyingine zilizoko chini ya Sekretarieti kuu ya Vatican kwa kuepuka ushindani usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo kwa Kanisa. Ushindani usiokuwa na mvuto unaweza kujenga uadui hata katika ngazi ya mtu binafsi.

Kanuni ya upendo iwe ni dira na mwongozo wa utume wao
Kanuni ya upendo iwe ni dira na mwongozo wa utume wao

Baba Mtakatifu anakazia sheria na kanuni za Kimataifa zisizokinzana na Mafundisho ya Kanisa na tatu ni kuzingatia taaluma na uzoefu kazini; mambo ambayo wanayatumia kwa ajili ya huduma kwa Vatican na hivyo katika hatima ya siku, wanaweza kutumia taaluma yao kwa kiwango cha juu. Ni hitaji la kimaadili kuendelea kupyaisha maarifa na ujuzi wao kwa kuzingatia sheria na kanu zinazoongoza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Vatican. Hii ni Ofisi inayosaidia kupambana na rushwa mintarafu Mktaba wa Mèrida ambao tangu mwaka 2016 Vatican pia imeuridhia. Kumbe, wafanyakazi katika kitengo hiki wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa uaminifu, ukweli, uwazi na kwa kukesha. Yote haya yanapaswa kuwa ni ushuhhuda wa ukweli na uwazi, ili kuepukana na kashfa zinazosheheni magazetini. Kumbe, kuna haja kwa wafanyakazi hawa kujikita kikamilifu katika kuzuia.

Wapambane na harufu ya rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa
Wapambane na harufu ya rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wafanyakazi hawa kuwasaidia wakuu wa Ofisi na Idara za Vatican kuhakikisha kwamba, wanaunda mazingira yasiyokuwa na harufu ya rushwa na ufisadi. Baba Mtakatifu amewashukuru wafanyakazi wanaojitolea kwa ajili ya huduma ya chakula kwa maskini, jambo la kupendezwa linalopaswa kutekelezwa kama sadaka, moyo wazi wa huruma na mapendo pamoja na kujenga mazingira ya kuweza kuzungumza na maskini, wanaohitaji upendo na mshikamano wa dhati, kuliko hata pengine sahani ya chakula. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa kuwashukuru kwa kazi kubwa wanayotekeleza mjini Vatican.

Ofisi ya Mkaguzi Mkuu
11 December 2023, 15:10