Papa,"vita daima ni kushindwa hakuna anayepata faida bali wauza silaha tu"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika kuwasalimu mahujaji wanaozungumza lugha ya Kiitaliano, Jumatano tarehe 6 Desemba 2023 katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican,aliwakaribisha kwa moyo mkunjufu wakufunzi wa semina wanaoshiriki katika kozi iliyohamasishwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji. Papa amesema Mafunzo yawasindikize “ili siku hizi za mafunzo ziweze kufufua huduma zenu kwa Kanisa.” Aidha aliwakaribisha wanaparokia ya Mtakatifu Antonio wa Padova huko Terni na parokia ya Mama wa Pompei huko Andria, akitumaini kwamba kutembelea makaburi ya Mitume kutaamsha ndani kila mtu ari mpya ya kiroho.
Tulinde hadhi ya kila mtu na kuepuka utamaduni wa kutupa
Baba Mtakatifu amewasalimia wanachama wa Mfuko wa Telethon, kutoka Mexico kwamba: “Wamexico wapendwa, ninawaalika kushirikiana kwa ajili ya waathirika huko Acapulco; Ninawaalikwa mjumuishe watu wote wenye ulemavu nchini Mexico. Tupambane dhidi ya jamii ya kutupa na, tulinda hadhi ya kila mtu.”
8 Desemba ni Siku Kuu ya Maria Mkingiwa dhambi ya Asili
Hatimaye, salamu zake ziliwaendea wazee, wagonjwa, wenye ndoa wapya na vijana, na mawazo maalum kwa wanafunzi wa Taasisi ya Leonardo da Vinci ya Mtakatifu Maria Capua Vetere na Milazzo. Baba Mtakatifu Francisko akikumbusha juu ya siku kuu inayokaribia ya Mama Mkingiwa dhambi ya Asili itakayofanyika tarehe 8 Desemba amesema: “Maria ‘aliamini’ katika upendo wa Mungu na akamjibu ‘ndiyo tazama mimi hapa’. Tujifunze kutokana na imani yake kamili katika Bwana kushuhudia wema na upendo wa kiinjili kila mahali.”
Tusisahau watu wa Ukraine, Israel na Palestina
Na hatimaya Papa amesema “Na tusisahau kuwaombea wale wanaopatwa na janga la vita, hasa idadi ya watu wa Ukraine, Israel na Palestina. Vita daima ni kushindwa. Hakuna anayeshinda, kila mtu anashindwa. Watengenezaji wa silaha pekee ndio wanaopata faida.” Amehitimisha kwa kuwabariki wote.