Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, ilikuwa ni fursa ya vijana kukutana na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika Kristo Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, ilikuwa ni fursa ya vijana kukutana na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika Kristo  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni: Uinjilishaji na Nguvu ya Ushuhuda wa Vijana

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Novemba 2023 alikutana na kuzungumza na wajumbe, waratibu, washiriki pamoja na wafadhili wakuu wa Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Haya ni maadhimisho yaliyogusa undani wa maisha ya watu wa kawaida, sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji wa watu unaosimikwa katika nguvu ya ushuhuda na furaha ya Injili kutoka kwa vijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yalifunguliwa rasmi kwa Ibada ya Misa takatifu tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Mwenyezi Mungu kwa njia ya mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, anawawezesha kugundua kwamba, wameitwa kukuza na kudumisha kumbukumbu na kutambua uzuri wa kuwa ni sehemu ya historia kubwa zaidi. Urafiki na wazee unaweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuona maisha yao si tu kuwa, ni jambo la mpito na kwamba, si kila kitu kinawategemea wao na uwezo wao. Kwa wazee, uwepo wa kijana katika maisha yao unaweza kuwapa matumaini kwamba, uzoefu wao hautapotea na kwamba ndoto zao zinaweza kupata utimilifu katika maisha ya vijana wa kizazi kipya.

Ushuhuda wa nguvu ya uinjilishaji kutoka kwa vijana
Ushuhuda wa nguvu ya uinjilishaji kutoka kwa vijana

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, ilikuwa ni fursa ya vijana kukutana na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika Kristo, huku wakiongozwa na Bikira Maria ambaye baada ya kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu aliondoka akaenda kwa haraka. Bikira Maria ni nyota angavu ya safari ya Kikristo anayeheshimiwa sana nchini Ureno! Alhamisi tarehe 30 Novemba 2023, Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na wajumbe, waratibu, washiriki pamoja na wafadhili wakuu wa Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Haya ni maadhimisho yaliyogusa undani wa maisha ya watu wa kawaida, sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji wa watu unaosimikwa katika nguvu ya ushuhuda na furaha ya Injili kutoka kwa vijana wa kizazi kipya.

Papa Francisko bado anakumbukumbu hai ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Papa Francisko bado anakumbukumbu hai ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana

Baba Mtakatifu bado ana kumbukumbu hai ya maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, ile zawadi ya Rozari Takatifu aliyopewa na Bibi wa miaka 96 bado anaitunza na yule kijana wa miaka 19 aliyedhani kwamba, angeitupa mkono dunia kabla ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023, bado anaendelea kuishi. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi na watu wa Mungu nchini Ureno waliowezesha kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Katika hotuba aliyokuwa ameandaa kwa ajili ya tukio hili, Baba Mtakatifu amelishukuru Kanisa, amegusia kuhusu Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni pamoja na Bikira Maria.

Bikira maria awe ni mfano bora wa huduma kwa jirani
Bikira maria awe ni mfano bora wa huduma kwa jirani

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu nchini Ureno kwa kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni na kwamba, maadhimisho haya yameacha ushuhuda angavu wa utume, umoja na furaha ya Injili. Huu ni mwaliko kwa Kanisa nchini Ureno kuhakikisha kwamba linakusanya vipande vilivyobaki, na wala kisipotee chochote katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Rej. Yn 6:12. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, wanatoa fursa kwa mbegu ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni iweze kuchanua na kuzaa matunda hata pale ambapo hawakutarajia hata kidogo. Baba Mtakatifu amewawekea mbele ya macho yao ya imani Bikira Maria ili aweze kuwa ni mfano bora wa sadaka na majitoleo katika huduma na kwamba, kwa hakika wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa na waendelee kuwaonesha watu wa Mungu huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote.

Vijana 27
01 December 2023, 14:59