Tafuta

Tarehe 14 Machi 1973 kukaanzishwa rasmi “Fondazione della Consociatio Internationalis Studio Iuris Canonici Promovendo” yaani “Mfuko wa Kuendeleza Kanuni na Sheria za Kanisa Kimataifa.” Tarehe 14 Machi 1973 kukaanzishwa rasmi “Fondazione della Consociatio Internationalis Studio Iuris Canonici Promovendo” yaani “Mfuko wa Kuendeleza Kanuni na Sheria za Kanisa Kimataifa.”   (© Vatican Media)

Kanuni na Sheria za Kanisa ni Kwa Ajili ya Wokovu wa Roho Za Watu

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia washiriki ujumbe wa matashi mema kwa kukazia: Shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote hiki, kipaumbele cha kwanza ni mtu na wokovu wa roho za watu: “Salus animarum”; Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kielelezo cha imani tendaji inayojikita katika shughuli za kichungaji na kimisionari mintarafu Kanuni na Sheria za Kanisa. Sheria ni kwa ajili ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, maprofesa wa Kanuni na Sheria za Kanisa kutoka Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Roma “La Sapienza” waliitisha mkutano, ili kukusanya nguvu kazi zitakazozamishwa zaidi katika kanuni na sheria za Kanisa na matokeo yake kunako mwaka 1970 Kongamano la kwanza la Kimataifa likaitishwa kama mtetezi makini wa thamani kubwa ya Kanuni na Sheria za Kanisa. Tarehe 14 Machi 1973 kukaanzishwa rasmi “Fondazione della Consociatio Internationalis Studio Iuris Canonici Promovendo” yaani “Mfuko wa Kuendeleza Kanuni na Sheria za Kanisa Kimataifa.” Kumbe, katika maadhimisho ya Kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tarehe 1 Desemba 2023, Mfuko umeadhimisha Kongamano la Kukuza Kanuni na Sheria Katika Mwelekeo Mpana wa Kimataifa wa Sayansi ya Sheria “Fifty years of promotion of Canon Law in the global panorama of Legal Science.” Ni katika muktadha wa Kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia washiriki ujumbe wa matashi mema kwa kukazia: Shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote hiki, kipaumbele cha kwanza ni mtu na wokovu wa roho za watu: “Salus animarum”; Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kielelezo cha imani tendaji inayojikita katika shughuli za kichungaji na kimisionari mintarafu Kanuni na Sheria za Kanisa.

Kanuni na Sheria za Kanisa zisaidie kukoleza uinjilishaji
Kanuni na Sheria za Kanisa zisaidie kukoleza uinjilishaji

Ni mategemeo ya Baba Mtakatifu kwamba, Kongamano hili limekuwa ni fursa ya kupyaisha ushirikiano na mafungamano yao na Kanisa, kwa kutambua kwamba, kimsingi wao ni vyombo vya sheria ya Mungu inayokita mizizi yake katika huruma na upendo. Jubilei hii ni kielelezo makini cha mchango ambao wameutoa katika kukuza na kudumisha Kanuni na Sheria za Kanisa; kwa kuunganisha Sheria za Kanisa na zile za kiraia. Ikumbukwe kwamba, kiini cha Kanuni na Sheria za Kanisa ni mtu aliyekombolewa na Kristo Yesu na kama mwamini wa Kanisa Katoliki. Kanuni na Sheria, pamoja na mambo mengine zinapania kutafuta na kudumisha ustawi na mafao ya wengi. Zinamwezesha mwamini kutambua haki na wajibu wake kama mwamini. Wito wa kwanza wa mwamini ni kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kumbe ni wajibu wa Wanasheria kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mwanga unaowawezesha waamini kutafsiri na hatimaye kumwilisha sheria hizi kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Sheria za Kanisa ni kwa ajili ya wokovu wa roho za watu wa Mungu “Salus animalum.” Kumbe, msingi wa Kanuni na Sheria za Kanisa ni Ufunuo wa Neno la Mungu pamoja na Mapokeo Hai ya Kanisa, ili kuyapokea na kuyafanyia kazi mapenzi ya Mungu. “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.” Mk 2:27. Watu wa Mungu wanaishi katika wakati na historia, kumbe, Wanasheria wanapaswa kuwasaidia watu wa Mungu kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote wa Mataifa.

Kanuni na Sheria ni kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini.
Kanuni na Sheria ni kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini.

Hekima kutoka kwa Mungu inapokelewa katika sala sanjari na ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza wengine mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Jambo la kujiuliza, “walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, Je, ataiona imani duniani?” Lk 18:8. Baba Mtakatifu amewataka wanasheria kuhakikisha kwamba, “wanapalilia na kukuza imani yao” kwani kuna hatari kubwa kwamba, unaweza kuwa ni Mwanasheria lakini pasi na imani. Kumbe, Kanuni na Sheria za Kanisa zinapaswa kusaidia mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika mwelekeo wa shughuli za kichungaji na kimisionari na kwamba, waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani wabahatike kukutana na Kristo Yesu, mwingi wa huruma na mapendo. Kanuni na Sheria za Kanisa ziwasaidie waamini kutubu na kumwongokea Mungu kwani Kanisa la kimisionari linaendelea kuinjilisha hata kwa kutumia Kanuni na Sheria za Kanisa. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa huduma makini wanayolitendea Kanisa.

50 Yrs Sheria
06 December 2023, 15:24