Tafuta

Jukwaa la Wakimbizi Duniani “Global Refugee Forum” lilifungulia rasmi tarehe 13 Desemba na kuhitimishwa tarehe 15 Desemba 2023 huko Geneva, nchini Uswis. Jukwaa la Wakimbizi Duniani “Global Refugee Forum” lilifungulia rasmi tarehe 13 Desemba na kuhitimishwa tarehe 15 Desemba 2023 huko Geneva, nchini Uswis.  (ANSA)

Jukwaa la Wakimbizi Duniani Kwa Mwaka 2023: Haki Msingi za Binadamu; Utu na Heshima Yake

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Kimsingi, kulinda na kuokoa maisha ya binadamu lazima iwe ni kipaumbele cha kwanza kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba watu waamue!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jukwaa la Wakimbizi Duniani “Global Refugee Forum” lilifungulia rasmi tarehe 13 Desemba na kuhitimishwa tarehe 15 Desemba 2023 huko Geneva, nchini Uswis kwa kuhudhuriwa na wajumbe 4, 200 kutoka katika nchi 168 na zaidi ya watu 10, 000 wameshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, ndilo lililokuwa mwenyeji wa mkutano huu. Washiriki wameshirikishana kuhusu shughuli mbalimbali wanazofanya mintarafu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Nchi wanachama wa UNHCR zimetangaza michango na ahadi zao kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi kama vile; elimu, upatikanaji wa soko la ajira, ujenzi wa amani, mabadiliko ya tabianchi pamoja na makazi mapya. Bwana Filippo Grandi Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, amesema kwamba, washiriki wameonesha uongozi, dira na ubunifu katika kutafuta suluhu, fursa, changamoto na matatizo sugu na kwamba, wameonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi ili kuboresha maisha ya mamilioni ya wakimbizi kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kiasi cha zaidi ya dola bilioni 2.2 zimetangazwa na serikali, sekta binafsi, Mashirika ya hisani na yale ya kidini pamoja na ahadi muhimu za kuzingatia. Mataifa yameahidi kutoa makazi kwa wakimbizi milioni moja ifikapo mwaka 2030. Wajumbe wameahidi kukuza uchumi na jamii kupitia shughuli za uwekezaji katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi, msaada kwa wajasiriamali wakimbizi, fursa za ajira, mafunzo pamoja na huduma za kisheria. Sekta binafsi imeahidi kutoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 250.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR miongoni mwa miradi bunifu ilikuwa ni ahadi ya wadau mbalimbali kuhusu ulinzi wa kidijitali kutoka kwa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, Umoja wa Mataifa na watendaji wengine, ili kusaidia kuzuia athari mbaya zinazotokana na kauli za chuki, habari potofu na upotoshaji wa makusudi. Jukwaa la Wakimbizi Kimataifa linapania kutekeleza kwa vitendo malengo yaliyowekwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi, mfumo wa ushirikishwaji wa uwajibikaji unaotabirika zaidi na sawa kati ya Mataifa, ambao ulipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mwezi Desemba 2018. Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika Jukwaa hili ulisomwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Kimsingi kulinda na kuokoa maisha ya binadamu lazima iwe ni kipaumbele cha kwanza kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, watu wawe na uwezo wa kuamua kuhama au kubaki katika nchi zao asilia na kwamba, wakimbizi wanahaki ya kuwa na maisha bora zaidi nchini mwao. Lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, leo hii kuna zaidi ya watu milioni 114 wasiokuwa na makazi maalum, kati yao kuna wakimbizi milioni 36.4 ambao ni wakimbizi wa shuruti, vita, nyanyaso na madhulumu bila kusahau madhara ya tabianchi, ndiyo maana hata leo hii kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Nchi zinazoongoza kwa kuwa na wakimbizi wengi duniani ni pamoja na: Ukraine, Sudan ya Kusini, Afghanistan na Venezuela.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.
Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.

Idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji inabeba sura za watu, wenye historia zao pamoja na mateso wanayokumbana nayo, hawa ni ndugu wanaohitaji msaada wa hali na mali; utu, heshima na haki zao msingi kulindwa na kuheshimiwa. Kamwe asiwepo mkimbizi anayelazimishwa kurejeshwa nchini mwake kama huko kuna uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Mkimbizi anapaswa kutambuliwa utu na heshima yake na kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kumbe anapaswa kupokelewa, kushirikishwa, kulindwa na kupendwa, ili aweze kupata fursa ya kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi husika. Ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni muhimu sana. Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Wakimbizi wa mwaka 1951 ulitiwa mkwaju hapo tarehe 1 Agosti 1951 na unalenga katika utekelezaji wa mambo makuu manne nayo ni: “Kupunguza mzigo kwa nchi zinazowahifadhi wakimbizi wengi; Kuwawezesha wakimbizi kujitegemea; Kuwezesha wakimbizi kufikia nchi ya tatu kupitia uhifadhi na njia zingine za kuingia nchini; Kusaidia juhudi zinazowawezesha wakimbizi kurudi katika nchi walikotokea. Viongozi wa kidini waliohudhuria Jukwaa la Wakimbizi Duniani “Global Refugee Forum” wanasema kuomba hifadhi ya ukimbizi ni sehemu ya haki msingi za binadamu.

Jukwaa la Wakimbizi Duniani
16 December 2023, 15:50