Tafuta

COP28 ni mahali ambako dunia inatathimini utekelezaji wa Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi. COP28 ni mahali ambako dunia inatathimini utekelezaji wa Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi.  (ANSA)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Mkutano wa COP28: Kilio cha Maskini

Papa amekazia: Umuhimu wa kusikiliza na kujibu Kilio cha Dunia Mama na Maskini ambao ni waathirika wakuu wa ukame, baa la njaa, Ukosefu wa maji safi na salama; Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula pamoja na uhamiaji wa shuruti, umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga hali ya kuaminika; Utunzaji bora wa mazingira na amani; utashi wa mabadiliko ya kisiasa na kiikolojia yanapaswa kuzingatia njia zinazofaa, za lazima na zinazoweza kufuatiliwa kwa urahisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Viwango vya joto duniani vikiwa vimeongezeka na kuvunja rekodi, na matukio ya kupindukia ya hali ya hewa yakileta madhara kwa binadamu duniani kote, mwaka huu mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, ni fursa ya pekee ya kubadili mwelekeo na kuchochea hatua za kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi. COP28 ni mahali ambako dunia inatathimini utekelezaji wa Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi, mkataba wa aina yake uliopitishwa kunako mwaka 2015 na kuweka mwelekeo wa kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya uzalishaji wa hewa ya ukaa ili kulinda uhai wa binadamu. Wakuu wa Nchi, mawaziri na washauri na wasuluhishi, sanjari na wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi, mameya, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na maafisa watendaji wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanakutana kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023 huko Dubai, Falme za Kiarabu (UAE), ili kujadili mustakabali wa mabadiliko ya tabianchi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema mkutano huu unapaswa kuwa na lengo la kukomesha kikamilifu kwa nishati ya visukuku, lakini kitu pekee ambacho bado kinakosekana ni utashi wa kisiasa. Ikiwa kama joto litaendelea kuongezeka, hili litakuwa ni janga kubwa kwa maisha ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa ina uwezo, teknolojia pamoja na rasilimali fedha inayopaswa kuelekezwa mahali sahihi ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kardinali Pietro Parolin amesoma hotuba ya Papa Francisko, COP28
Kardinali Pietro Parolin amesoma hotuba ya Papa Francisko, COP28

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 2 Desemba 2023 amekazia kuhusu: Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu Kilio cha Dunia Mama na Maskini ambao ni waathirika wakuu wa ukame, baa la njaa, Ukosefu wa maji safi na salama; Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula pamoja na uhamiaji wa shuruti, umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga hali ya kuaminika; Utunzaji bora wa mazingira na amani; utashi wa mabadiliko ya kisiasa; mabadiliko ya kiikolojia yanapaswa kuzingatia njia zinazofaa, za lazima na zinazoweza kufuatiliwa kwa urahisi na kwamba, ufanisi wa nishati lazima uzingatie: vyanzo mbadala, kuondolewa kwa nishani ya mafuta, elimu bora katika mitindo ya maisha na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuungana na kushikamana. Baba Mtakatifu anasema athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya kimataifa ambayo inahusiano wa ndani kabisa na utu, heshima na haki msingi za binadamu, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha utamaduni wa uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kudhibiti ongezeko la joto duniani. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuungana ili kuweza kufikia utekelezaji mzuri unaozingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huu ni uwajibikaji unaoongozwa na dhamiri nyofu kwa ajili ya ujenzi wa matumaini ya Kesho iliyo bora zaidi. Maaskini ndio waathirika zaidi wa mabadiliko ya tabianchi kutokana na ukataji wa miti ovyo, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; ukosefu wa maji safi na salama; Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula pamoja na uhamiaji wa shuruti. Kuhusu ongezeko la idadi ya watu katika nchi zinazoendelea duniani ni mwelekeo sahihi wa kuenzi Injili ya uhai ambayo kwa sasa inakumbana na vikwazo vya ukoloni wa kiitikadi pamoja na deni kubwa la kiikolojia na kwamba, nchi hizi zisiongezewe mzigo wa deni kubwa la kifedha.

Maskini ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi
Maskini ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi

Jambo la msingi kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kujenga na kuimarisha umoja, ushirikiano na mshikamano kwa kuanzisha sheria, kanuni na taratibu zitakazodhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba jambo la msingi kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kujenga hali ya kuaminiana. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na amani duniani ni sawa na chanda na pete. Kuna nguvu na rasilimali nyingi zinazopotea kutokana na vita kama inavyojionesha kati ya Israeli na Palestina, Urusi na Ukraine bila kusahau sehemu mbalimbali za dunia. Kuna rasilimali nyingi inayotumika kwa ajili ya kugharimia vita inayoteketeza maisha ya binadamu pamoja na kuharibu mazingira nyumba ya wote. Kamwe vita haitaweza kuwa ni suluhu ya matatizo na changamoto za Jumuiya ya Kimataifa. Rasimali fedha inayotumika kwa ajili ya vita, ianzishiwe Mfuko wa Kimataifa kwa ajili ya kupambana na baa la njaa duniani. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kilio cha watu wa Mungu wanaotaka mabadiliko ya kisiasa yanayofumbatwa katika wongofu wa kiikolojia sanjari na mabadiliko ya kitamaduni. Kanisa Katoliki ambalo limekuwa mstari wa mbele katika sekta ya elimu, litaendelea kuhamasisha ushiriki wa wote pamoja na mtindo bora wa maisha kwa sababu wote wanawajibika.

COP28 Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Nov. Hadi 12 Desemba
COP28 Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Nov. Hadi 12 Desemba

Baba Mtakatifu anasema, kunako Mwaka 1992, Umoja wa Mataifa uliandaa Mkutano wa Kimataifa huko Rio de Janeiro, Brazil, ambapo Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC ulipitishwa na Wakala wake wa kuratibu; yaani Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi ilianzishwa na Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Mwaka 2015 ulikuwa ni mwanzo mpya wa mwelekeo wa kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya uzalishaji wa hewa ya ukaa ili kulinda uhai wa binadamu. Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, uoneshe utashi wa kisiasa utakaosaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kiikolojia yanayopaswa kuzingatia njia zinazofaa, za lazima na zinazoweza kufuatiliwa kwa urahisi na kwamba, ufanisi wa nishati lazima uzingatie: vyanzo mbadala, kuondolewa kwa nishani ya mafuta, elimu bora katika mitindo ya maisha na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuungana na kushikamana. Huu ni wakati wa kusonga mbele kwa ari na mwamko mkubwa zaidi kwa kutambua kwamba, kuna Mikataba iliyopita haikuweza kutekelezwa katika ubora na ufanisi wake! Kumbe, kunahitajika utashi wa kisiasa utakaoweza kuweka kwa vitendo maamuzi ya COP28 kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, dhamana inayotekelezwa kwa dhati kabisa na vijana wa kizazi kipya. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu anasema, mwaka 2024 kuna tukio la kihistoria la Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako mwaka 1224 alipotunga “Utenzi wake kuhusu mazingira” akimsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu pamoja na viumbe vyake vyote; udugu vikamsaidia kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; upatanisho. Baba Mtakatifu anapenda kuwaachia washiriki wa mkutano wa COP28, Dubai, 2023: mwaliko wa umoja na mshikamano kwa kuunganisha kwa pamoja nguvu zao, ili kuondokana na giza na vita na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, ili kujielekeza katika mwanzo na mng’ao wa siku mpya.

Papa COP28
02 December 2023, 13:44