Papa,wanawake wasiwe vigezo vya kuvutia wengine na kuwatawala
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, ametuma ujumbe wake kwa ajili ya kampeni ya kitaifa dhidi ya vurugu kwa wanawake iliyoandaliwa na na Radio I Rai na Cadmi D.I.Re. Katika ujumbe huo, Papa Francisko anawashukuru wahamasishaji wa mpango huo wa "Masafa ya muda mrefu dhidi ya unyanyasaji wa wanaume juu ya wanawake", ambao unatuwezesha kutafakari juu ya suala la juu sana. Kwa hakika, unyanyasaji dhidi ya wanawake ni gugu lenye sumu ambalo linasumbua jamii yetu na ambayo lazima liondolewe kutoka katika mizizi. Na mizizi hii ni ya kiutamaduni na kiakili, ambayo hukua katika udongo wa ubaguzi, umilki, na udhalimu. Katika maeneo mengi na hali nyingi sana wanawake huwekwa nyuma, huchukuliwa kuwa "duni", kama vitu: na ikiwa mtu amepunguzwa kwa kitu, basi hadhi yake haionekani tena, inachukuliwa kuwa mali ya mtu ambayo inaweza kutumika katika kila kitu, hata kufikia hatua ya kukandamiza.
Wanawake wengi wanaelemewa na uzito wa janga la ukatili
Baba Mtakatifu amekazia kusema kuwa ni wanawake wangapi wamelemewa na uzito na janga la ukatili! Ni wangapi wanaoteswa vibaya, wananyanyaswa, wanafanywa watumwa, waathriwa wa kiburi cha wale wanaofikiri wanaweza kudhibiti miili yao na maisha yao, kulazimishwa kujisalimisha kwa uchoyo wa wanadamu. Kwa bahati mbaya, vyombo vya habari bado vina jukumu lisiloeleweka katika hili. Kwa upande mmoja wanakuza heshima na kuhamasisha wanawake; lakini kwa upande mwingine wanaendelea kusambaza ujumbe mwingi unaoegemezwa juu ya matangazo ya kibiashara na utumiaji, ambao mifano yao, ya kiume na ya kike, inatii vigezo vya mafanikio, kujithibitisha, ushindani, uwezo wa kuvutia wengine na kuwatawala.
Upendo hauna kifungo
Baba Mtakatifu amebainisha kuwa pakini palipo na kutawaliwa kuna unyanyasaji! Sio upendo unaohitaji wafungwa. Papa amebainisha kuwa Bwana anatutaka tuwe huru na katika hadhi kamili! Kwa kukabiliwa na janga la unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia kwa wanawake, kuna haja ya haraka ya kugundua kwa upya aina za mahusiano ya haki na usawa, kulingana na kuheshimiana na kutambuliwa. Masharti ya kila aina lazima yakabiliwe na hatua za kielimu ambazo, kuanzia kwenye familia, na zinamweka mtu huyo na utu wake katikati. Ni jukumu letu, jukumu la kila mtu, kutoa sauti kwa dada zetu wasio na sauti: wanawake ambao ni waathriwa wa unyanyasaji, unyonyaji, kutengwa na shinikizo lisilofaa. Tusibaki kutojali! Ni muhimu kuchukua hatua mara moja, katika ngazi zote, kwa uamuzi, uharaka na ujasiri.
Kiwango cha binadamu kinapimwa jinis tunavyowatendea wanawake
Baba Mtakatifu Francisko amekazia kusema kuwa ni kutoka katika moyo na mwili wa mwanamke wokovu ulikuja ulimwenguni. Na kwa njia hiyo kiwango chetu cha ubinadamu kinafichuliwa kwa jinsi tunavyowatendea wanawake, katika nyanja zake zote. Ni Matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba kampeni ya masafa ambayo yameanza ni marefu sana na yanaweza kuchangia mabadiliko ya fikra. Amewabariki na kuwahimiza wasonge mbele katika ahadi hiyo. Amewapongeza kwa kazi hiyo nzuri na kuhitimisha ujumbe wake.