Tafuta

Papa Francisko:Tujishughulishe kuishi maisha ya ndani kuliko kuishi ndumila kuwili

Katika tafakari ya Baba Mtakatifu kabla ya sala ya Malaika wa Bwana,amejikita na maneno ya Yesu kuhusu waandishi na Mafarisayo wasemayo lakini bila ktenda wafanyayo,ambapo Papa ametualika sote na hasa wenye wajibu katika jamii au katika Kanisa,kutokuwa na moyo wa ndumila kuwili na wasiwasi wa kujionesha wakamilifu kwa nje,wakati ndani tunaishi kinyume.

Na Angella Rwezaula, Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ametoa tafakari yake ya Dominika, kabla ya sala ya Malaika wa bwana kwa mahujaji na waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 5 Novemba 2023. Akianza tafakari hiyo amesema kutoka katika Injili ya Liturujia ya leo tunasikia baadhi ya maneno ya Yesu kuhusu waandishi na Mafarisayo, yaani, viongozi wa dini za watu. Yesu anatumia maneno makali sana kwa mamlaka haya, kwa sababu wanasema lakini hawatendi (Mt 23,3) na matendo yao yote watendayo  wanafanya ili waweze kusifiwa na watu Mt 23,5. Hayo andiyo anasema Yesu, kuwa wanasema na hawafanyi na kila wanachofanya wanafanya ili waonekane, Papa amerudia tena.

Umati wa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu petro 5 Novemba
Umati wa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu petro 5 Novemba

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amependa kuelezea mantiki mbili, kuhusiana na hilo kwamba kuna,  umbali kati ya kusema na kufanya na ubora wa nje juu ya mambo ya ndani. Papa ameanza na Umbali kati ya kusema na kutenda. Kwa waalimu hawa wa Israel, wanaodai kuwafundisha wengine Neno la Mungu na kuheshimiwa kama mamlaka ya Hekalu, Yesu anapinga uwili yaandi ndumila kuwili, wa maisha yao: wanahubiri jambo moja, lakini wanaishi lingine. Maneno haya ya Yesu yanakumbuka yale ya manabii, hasa Isaya: “Watu hawa hunijia kwa vinywa vyao tu na kuniheshimu kwa midomo, lakini mioyo yao iko mbali nami”(Isa 29:13). Hii ndio hatari ya kuangalia: uwili wa moyo. Sisi pia tuna hatari hii: uwili huu wa moyo ambao unaweka hatarini ukweli wa ushuhuda wetu na pia uaminifu wetu kama watu na kama Wakristo.

Hakika umati wa waamini na mahujaji katika kusali sala ya Malaika wa Bwana Novemba 5,2023
Hakika umati wa waamini na mahujaji katika kusali sala ya Malaika wa Bwana Novemba 5,2023

Baba Mtakatifu amekazia kusema kuwa "Kwa sababu ya udhaifu wetu, sote tunapata umbali fulani kati ya kusema na kutenda; lakini jambo jingine, badala yake, ni kuwa na mioyo miwili, kuishi na “mguu mmoja katika viatu viwili” bila kufanya tatizo. Hasa tunapoitwa -katika maisha, katika jamii au katika Kanisa - kubeba jukumu la wajibu, tukumbuke hili: hapana kuwa ndumila kuwili! Kwa padre, mhudumu wa kichungaji, mwanasiasa, mwalimu au mzazi, sheria hii inatumika daima kwa : kile unachosema, unachohubiri kwa wengine, lazima ujitoe kukiishi kwanza. Ili kuwa walimu wenye mamlaka lazima kwanza uwe mashuhuda wa kuaminika."

Papa Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana 5 Novemba 2023
Papa Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana 5 Novemba 2023

Kipengele cha pili Papa amesema kinakuja kama matokeo ya ubora wa nje juu ya mambo ya ndani. Kiukweli, kwa kuishi katika unafiki, waandishi na Mafarisayo wana wasiwasi juu ya kuficha kutopatana kwao ili kuokoa sifa yao ya nje. Kwa hakika, ikiwa watu wangejua kilichomo mioyoni mwao, wangeaibika, na kupoteza sifa yao yote. Na kwa hivyo wanafanya mambo ili waonekane kuwa waadilifu, "kuokoa uso", kama wasemavyo. Vipodozi ni vya kawaida sana: hupodoa uso, hupodoa maisha, hupodoa moyo. Watu hawa walipodoleka hawajui jinsi ya kuishi ukweli. Na mara nyingi sisi pia tuna kishawishi hiki cha uwili yaani ndumila kuwili.

Kutokana na hilo, ndipo Baba Mtakatifu amekuja na maswali kwamba, kwa kukubali onyo hili kutoka kwa Yesu, hebu pia tujiulize: je, tunajaribu kutekeleza yale tunayohubiri, au tunaishi ndumila kuwili? Je, tunasema jambo moja na kufanya lingine? Je, tunajishughulisha tu na kuonekana wazuri kwa nje, kujipodoa, au tunajali maisha yetu ya ndani kwa unyofu wa moyo? Kwa njia hiyo Papa amesema ebu Tumgeukie Bikira Mtakatifu: Yeye aliyeishi kwa uadilifu na unyenyekevu wa moyo kadiri ya mapenzi ya Mungu atusaidie kuwa mashuhuda wa kuaminika wa Injili, Papa amehitimisha tafakari yake.

Tafakari ya ya Papa 5 Novemba 2023
05 November 2023, 12:58