Tafuta

Baba Mtakatifu ametia nia ya kwenda na kushiriki kwenye Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28. Baba Mtakatifu ametia nia ya kwenda na kushiriki kwenye Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28.  (AFP or licensors)

Papa Francisko Kushiriki Mkutano wa COP28 Dubai, Falme za Kiarabu: 1-3 Desemba 2023

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan wa Falme za Kiarabu. Kumbe, Baba Mtakatifu ametia nia ya kwenda na kushiriki kwenye Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 kuanzia tarehe Mosi Desemba hadi 3 Desemba 2023. Mkutano unafunguliwa rasmi tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023: Matarajio ya Jumuiya ya Kimataifa kwa COP28 Dubai.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” unakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu wa mazingira na hatari zake; Kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Waraka huu unapembua kwa kina na mapana Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi, ufanisi na kuanguka kwake; Matarajio ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 huko Dubai, 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi anasema na kwamba, watu wengi wanaathrika sana mintarafu afya ya binadamu, kazi, upatikanaji wa rasilimali, makazi pamoja na uhamiaji wa nguvu. Haya ni matatizo ya kijamii yanayogusa na kutikisa utu, heshima, haki msingi na maisha ya binadamu. Athari za mabadiliko ya tabianchi duniani zimepelekea ongezeko la kiwango cha joto duniani na matokeo yake ni mvua kubwa zinazoambatana na mafuriko na sehemu nyingine ukame wa kutisha. Ongezeko la kiwango cha joto duniani kunapelekea kuyeyuka kwa barafu na matokeo yake ni ongezeko la kina cha maji baharini, hatari kubwa kwa wakazi wanaoishi kwenye fukwe za Bahari.

COP28 Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Nov. Hadi 12 Desemba
COP28 Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Nov. Hadi 12 Desemba

Kumekuwepo na upinzani pamoja na hali ya kuchanganyikiwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari hali ambayo kwa siku za usoni, itawalazimisha watu kuhama kutoka kwenye fukwe za bahari. Taarifa kamili ya matokeo haya zinapaswa kutolewa na kwamba, waathirika wengi zaidi ni maskini, ingawa asilimia 50% ya watu matajiri na nchi tajiri ndio wanaochafua zaidi mazingira nyumba ya wote. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika teknolojia rafiki na mazingira, changamoto kwa wanasiasa na wafanyabiashara kutenda kwa haraka. Baba Mtakatifu katika Warake wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anakaza kusema, shughuli za binadamu zimechangia sana katika uchafuzi wa mazingira bora nyumba ya wote: kwa kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani na kwamba, matukio ya milipuko ya volcano ni kwa sababu ya ongezeko la shughuli za binadamu pamoja na uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa! Uharibifu wa mazingira na hatari zake unazidi kuongezeka kiasi cha chumvi kuongezeka pia na hivyo kuathiri maisha ya viumbe vya majini pamoja na kuyeyuka kwa barafu. Ukataji wa miti ovyo ni hatari sana, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kuwajibika zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wachunguzi wa mambo wanasema, kumekuwepo na uhusiano wa karibu sana katika kuenea kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, maisha ya binadamu pamoja na mazingira kwani kila kitu kinamwingiliano na hakuna anayeweza kujiokoa mwenyewe.

Papa Francisko Kushiriki Mkutano wa COP28, Dubai, Falme za Kiarabu.
Papa Francisko Kushiriki Mkutano wa COP28, Dubai, Falme za Kiarabu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Warake wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anachambua kuhusu: Matarajio ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, huko Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023. COP28 ilete mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha mpito, mabadiliko ya kudumu kwa kujikita katika matumizi ya nishati ya upepo na jua ili hatimaye, kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta. Huu ni uwajibikaji wa pamoja, utakaoirejeshea tena Jumuiya ya Kimataifa uwezo wa kuaminika tena katika maamuzi yake; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Itakumbukwa kwamba, Falme za Kiarabu ni mojawapo ya Mataifa 10 yanayoongoza duniani kwa uzalishaji wa mafuta na imemteua mtendaji mkuu wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, Sultan Al Jaber kuwa Rais wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28. Mafuta, kama gesi na makaa ya mawe, hizi ndizo sababu kuu za mabadiliko ya tabia nchi kwa sababu hutoa gesi chafu zinazopasha joto sayari kama vile kaboni dioksaidi zinapochomwa kwa ajili ya nishati. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan wa Falme za Kiarabu. Kumbe, Baba Mtakatifu ametia nia ya kwenda na kushiriki kwenye Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 kuanzia tarehe Mosi Desemba hadi 3 Desemba 2023. 

Papa CO28 Dubai
04 November 2023, 14:46