Tafuta

Mateso yanaendelea huko Gaza Mateso yanaendelea huko Gaza  (AFP or licensors)

Papa atoa wito wa kuacha vita mara moja na kuombea waathirika wa Nepal

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana,Baba Mtakatifu ameomba usitishaji wa vita huko Israel naPalestina.Amewakumbuka waathiriwa wa tetemeko la Ardhi huko Nepal,na vile vile watu wa Ukraine.Ni matumaini ya Papa kwamba msaada wa kibinadamu unaweza kupatikana.Pia amewaombea watu wa Italia kutokana na mafuriko na Nchi nyingine.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya tafakari na sala ya Malaika wa Bwana akiwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 5 Novemba 2023 amesema: “Ninaendelea kufikiria juu ya hali mbaya ya Palestina na Israel, ambapo watu wengi wamepoteza maisha. Tafadhali acha, kwa jina la Mungu: sitisha moto! Ninatumaini kwamba njia zote zitafuatwa ili mzozo huo uweze kuepukwa kabisa, waliojeruhiwa wasaidiwe na misaada iweze kuwafikia wakazi wa Gaza, ambako hali ya kibinadamu ni mbaya sana. Waachilie mateka mara moja. Miongoni mwao pia kuna watoto wengi, warudi kwenye familia zao! Ndiyo, hebu tufikirie kuhusu watoto, watoto wote waliohusika katika vita hivi, pamoja na Ukraine na migogoro mingine: hivi ndivyo maisha yao ya baadaye yanavyouawa. Tuombe nguvu ya kusema “inatosha,” alisisitiza Papa kwa masikitiko.

Tetemeko kali nchini Nepal

Baba Mtakatifu Francisko akiendelea pia amekumbuka majanga ya asili katika Nchi ya Asia ambapo amesema: Niko karibu na watu wa Nepal wanaoteseka kutokana na tetemeko la ardhi; pamoja na wakimbizi wa Afghanistan ambao wamepata hifadhi nchini Pakistan lakini sasa hawajui tena pa kwenda. Na pia ninaombea waathrika wa dhoruba na mafuriko, huko Italia na katika nchi zingine.

Salamu kwa mahujaji na waamini kutoka pande za dunia

Akiwageukia mahujaji, Baba Mtakatifu  Francisko amesema: "Ninawasalimuni nyote kwa upendo, Waroma na mahujaji kutoka nchi mbalimbali. Hasa ninawasalimu waamini wa Vienna na Valencia, kikundi cha Parokia ya Cagliari, Bendi na Kwaya ya Longomoso, ya Alto Adige. Nawasalimu vijana wa Rodengo Saiano, Ome na Padergnone; makatekista wa Cassina de' Pecchi na wale wa Parokia ya Mtakatifu Giovanni Bosco ya Trieste; Ninawasalimia Kamati ya "Acha Vita". "Ninawatakia wote Dominika njema. Tafadhali msisahau kuniombea. Mlo mwema na mchana mwema. Kwaheri ya  kukuona."

Kuhusiana na tetemeko la ardhi nchini Nepal 

Takwimu zilizotolewa tarehe 4 Novemba 2023 na wizara ya mambo ya ndani ya Nepal wakati vikosi vya usalama vikifanya juhudi kusaidia katika juhudi za uokoaji ni kuwa, waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililotikisa magharibi mwa Nepal Ijumaa usiku tarehe 3 Novemba ilikuwa imefikia watu 138. Naye msemaji wa polisi katika mji mkuu Kasmandu alisema kuwa idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka kadiri ya waokoaji wanavyozidi kuokoa.

Takwimu za majeruhi na vifo katika baadhi ya maeneo yaliyopatwa na tetemeko hilo bado zilikuwa hazijapatikana. Awali msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Narayan Prasad Bhattarai alisema miongoni mwa waliokufa, 92 ni wa wilaya ya Jajarkot na 40 ni kutoka Rukum. Maeneo hayo mawili ndiyo yaliyoathiriwa vibaya zaidi na tetemeko hilo. Waziri Mkuu Pushpa Kamal Dahal alitembelea eneo la mkasa, baada ya kuelezea kusikitishwa kwake na vifo, na uharibifu uliosababishwa na janga hilo. Nepal imekuwa ikikumbwa mara kwa mara na matetemeko ya ardhi. Mwaka 2015, karibu watu 9,000 walikufa na wengine 22,000 walijeruhiwa baada ya tetemeko kubwa kuipiga nchi hiyo. Tetemeko hilo liliharibu takribani shule 8,000 na kuwaacha watoto wasiopungua milioni moja bila madarasa.

Wito wa Papa kwa ajili ya Gaza
05 November 2023, 12:59