Tafuta

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 tangu Jimbo la Casale Monferrato lililoko nchini Italia, lilipoanzishwa rasmi na Papa Sixstus IV tarehe 18 Aprili 1474 Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 tangu Jimbo la Casale Monferrato lililoko nchini Italia, lilipoanzishwa rasmi na Papa Sixstus IV tarehe 18 Aprili 1474  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 ya Jimbo Casale Monferrato: 2023-2024

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 ya Jimbo la Casale Monferrato: Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wateule na watakatifu wa Mungu Jimboni Casale Monferrato kutangaza na kushuhudia upendo wao kwa Kristo Yesu na Injili yake; Iwe ni fursa ya kupyaisha uchaji wa Mungu kwa kuboresha maisha ya Ibada na Sala; Tafakari ya kina ya Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika maisha adili na matakatifu, kielelezo cha mwanga angavu wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye jiwe kuu la msingi, mwaliko wa kutafakari uzuri, ukuu na utakatifu wa Kanisa la Mungu, ili kuamsha na kupyaisha ile kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika Sala, Neno, Sakramenti, maisha na utume wa Kanisa. Jubilei kiwe ni kipindi cha kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu, kwa kutembea pamoja kama Kanisa la Kimisionari na Kisinodi, ili kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika umoja, ushiriki na utume. Ni wakati wa kupyaisha shughuli za kichungaji kwa wakatekumeni, wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wakati muafaka wa kudumisha haki jamii, utawala wa sheria, amani na utulivu. Jubilei ni fursa ya kumwendea Mwenyezi Mungu kwa moyo wa: shukrani, uchaji na ibada sanjari na kuwaelekea jirani kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Hiki ni kipindi muafaka cha kuzingatia mahitaji msingi ya kitaalimungu na kichungaji.

Jubilei ya Miaka 550: Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya Huruma
Jubilei ya Miaka 550: Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya Huruma

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 tangu Jimbo la Casale Monferrato lililoko nchini Italia, lilipoanzishwa rasmi na Papa Sixstus IV tarehe 18 Aprili 1474 sanjari na maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Evasius, Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo hili, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuwa Mwakilishi wake wa Kitume katika Maadhimisho ya Ufunguzi wa Jubilei ya Jimbo la Casale Monferrato, Dominika tarehe 12 Novemba 2023 na maadhimisho haya yatahitimishwa tarehe 12 Novemba 2024. Kardinali Parolin katika hija hii ya kitume ataambatana na Monsinyo Desire Azogou, Makamu Askofu Jimbo la Casale Monferrato pamoja na Padre Francesco Mancinelli, Gambera wa Madhabahu ya Crea. Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Kardinali Pietro Parolin anasema, hiki ni kipindi kwa watu wa Mungu Jimboni Casale Monferrato kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, “Te Deum.” Kumbe, uteuzi huu ni kmwendelezo wa utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wateule na watakatifu wa Mungu Jimboni Casale Monferrato kutangaza na kushuhudia upendo wao kwa Kristo Yesu na Injili yake; Iwe ni fursa ya kupyaisha uchaji wa Mungu kwa kuboresha maisha ya Ibada na Sala; Tafakari ya kina ya Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika maisha adili na matakatifu, kielelezo cha mwanga angavu wa imani.

Jubilei ya Miaka 550 Jimbo Katoliki la Casale Monferrato 2023-2024
Jubilei ya Miaka 550 Jimbo Katoliki la Casale Monferrato 2023-2024

Baba Mtakatifu Francisko anamwomba, Kardinali Parolin, kumfikishia salam na matashi mema kwa watu wote wa Mungu watakaohudhuria sherehe hii ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 tangu Jimbo la Casale Monferrato lililoko nchini Italia, lilipoanzishwa rasmi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anatoa baraka zake za kitume kwa wote watakaoshiriki katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 tangu Jimbo Katoliki la Casale Monferrato. Kwa upande wake Askofu Gianni Sacchi anasema, Jimbo lake linataka kujikita zaidi katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi, Kanisa linalofundisha, tamadunisha na kuinjilisha. Hili ni Kanisa linalojikita katika Injili ya ukarimu na upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 550 iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kipaumbele cha kwanza ni Neno la Mungu, Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi na Injili ya Upendo na Ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Jubilei Miaka 550
07 November 2023, 15:38