Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote, tarehe 2 Novemba 2023, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Jumuiya ya Madola Roma. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote, tarehe 2 Novemba 2023, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Jumuiya ya Madola Roma.  (Vatican Media)

Papa: Kumbukumbu ya Waamini Wote Marehemu: Kumbukumbu na Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote, tarehe 2 Novemba 2023, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Jumuiya ya Madola Roma yanayotoa hifadhi kwa marehemu 426 waliozikwa mahali hapa. Hawa ni askari na mateka wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kuanzia mwaka 1939 hadi mwaka 1945. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amejikita katika mawazo makuu mawili: Kumbukumbu na Matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanajiunga na Kristo Yesu na kuanza kutembea katika mwanga wa Pasaka. Rej. Rum 6:3-4. Huu ni ushirika na Kanisa ambalo bado linasafiri huku bondeni kwenye machozi na watakatifu wa mbinguni. Rej. LG 49. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, anawakumbuka na kuwaombea waamini wote marehemu “Commemoratio Omnium Fidelium Defunctorum” waliotangulia mbele ya haki wakiwa na alama ya imani na sasa wanapumzika kwenye usingizi wa amani. Kumbukumbu hii inawasaidia waamini kuwatambua, kuwakumbuka na kuwaombea wale waliowatangulia mbele za haki, wakiwa na imani na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Hii ni kumbukumbu ya umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki kikamilifu katika hija ya maisha ya hapa duniani, lakini leo hii hawapo tena! Kumbukumbu ya kuwaombea waamini wote marehemu ilianza kushika kasi kwenye monatseri na nyumba za kitawa kunako Karne VII na hivyo kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 2 Novemba ya kila mwaka, baada ya kuadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote, hapo tarehe Mosi Novemba. Alikuwa Papa Benedikto XV kunako tarehe 10 Agosti 1915 katika Katiba ya Kitume ya “Incruentum Altaris Sacrificium” alipotoa ruhusa kwa Mapadre kuweza kuadhimisha Misa tatu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Waamini Wote. Misa ya kwanza ni kwa ajili ya marehemu wote, misa ya pili ni kwa nia ya Baba Mtakatifu na misa tatu ni kwa ajili ya Padre mwenyewe! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wale, Kristo Yesu amefungua lango la matumaini, linalowawezesha waamini kuingia ndani mwake, ili kulitafakari Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbukumbu hii inasimikwa katika imani na matumaini yanayowawezesha watu kukutana na Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, aliyewakirimia zawadi ya maisha.

Kumbukumbu ya waamini  wote marehemu, tarehe 2 Novemba 2023
Kumbukumbu ya waamini wote marehemu, tarehe 2 Novemba 2023

Haya ni matumaini yanayobubujika kutoka Yerusalemu ya mbinguni, kielelezo cha: uzuri na upendo mkuu ambao Bwana arusi anautoa kwa bibi arusi wake. Kumbe, kumbukumbu na matumaini yawawezeshe waamini kukutana na Mwenyezi Mungu, Muumbaji na Mkombozi, ambaye daima anasubiri kukutana na waja wake! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote, tarehe 2 Novemba 2023, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Jumuiya ya Madola Roma “Rome War Cemetery” yanayotoa hifadhi kwa marehemu 426 waliozikwa mahali hapa. Hawa ni askari na mateka wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kuanzia mwaka 1939 hadi mwaka 1945. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amejikita katika mawazo makuu mawili: Kumbukumbu na Matumaini. Hii ni kumbukumbu ya wale waliotangulia, walioishi na wengine kukatishwa maisha yao. Hii ni kumbukumbu ya watu wengi waliowatendea mema ndugu na jirani zao. Katika kumbukumbu hii, Baba Mtakatifu anasema, waamini wanawakumbuka hata wale ambao hawakuweza kutenda mema mengi, lakini wamepokelewa katika kumbukumbu na rehema na huruma ya Mungu. Matumaini ni mwaliko wa kutazama yajayo kwani mwanadamu daima yuko safarini anakokutana na jirani zake, lakini hii ni safari ya kukutana na Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya matumaini ambayo kamwe hayakati tamaa. Hili ni tumaini linalosimikwa katika utu wema unaowasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusonga mbele licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali za maisha. Hili ni tumaini linalozaa wema na kamwe tumaini hili haliwezi kukatishwa tamaa. Baba Mtakatifu anasema, alipoingia makaburini hapo, amegundua kwamba, marehemu wengi ni wale waliofariki dunia wengi wao wakiwa na umri wa miaka kati ya 20 na 30, lakini maisha yao yalikatishwa kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Makaburi ya Askari na Mateka wa Vaita Kuu ya Pili ya Dunia
Makaburi ya Askari na Mateka wa Vaita Kuu ya Pili ya Dunia

Hawa wanaweza kuonekana kuwa ni mashujaa wa Jumuiya ya Madola, lakini kwa wazazi na walezi, waliwapoteza watoto wao katika vita! Hii ndiyo hali ilivyo hata leo hii, kuna vijana na wazee wengi wanaoitupa mkono dunia kutokana na vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Leo hii, bado kuna watu wengi wanatema zawadi ya maisha. Katika kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi kuendelea kuombea amani duniani, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kukomesha vita, ili watu wasiokuwa na hatia wasipoteze tena maisha yao kutokana na vita. Vita ni kielelezo makini cha kushindwa kwa binadamu na wala hakuna mshindi katika vita, bali kushindwa kunako lipwa kwa gharama kubwa ya maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wao, askari wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita; wote hawa wapokelewe na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu apende kuwarehemu na kuwakirimia tumaini la kuweza kusonga mbele ili kuweza kukutana na wote katika Kristo Mfufuka anakapowaita wote kwake.

Mwezi Novemba ni kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Wote
Mwezi Novemba ni kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Wote

Mama Kanisa anawaombea watoto wake ili watakaswe, ikiwa kama wanahitaji kutakaswa kabla ya kupokelewa mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele wakati miili yao inapobaki ardhini ikingoja kurudi kwa Kristo Yesu na ufufuko wa wafu. “Sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya Kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba, katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu.” (KKK 962). Kanisa linasali na kuwaombea waamini marehemu kusudi wapate msaada wa kiroho na waamini walio bado hai wapate matumaini ya uzima ujao mbinguni. Ni muhimu na vema kuwaombea wafu, kwani hata kama wamekufa katika neema na upendo kwa Mungu, inawezekana bado wanahitaji utakaso wa mwisho ili waweze kuingia katika furaha ya uzima wa milele. Mtakatifu Ireneo anasema utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai. Maisha ya mwanadamu, mkristo, mbatizwa huwa na aina mbili ya kifo. Kifo cha kwanza ni kwa njia ya Ubatizo na imani: Rej. Rum. 1:6 ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo, tumejiunga na Kristo Yesu aliyekufa na kufufuka kwa wafu. Rej. KKK 628. Sakramenti ya Ubatizo ambao alama yake ya asili na timilifu ni kuzamishwa kunako ashiria bayana kushuka kaburini kwa mkristo anayeifia dhambi pamoja na Kristo Yesu ili aishi maisha mapya kwa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka kwa wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na waamini waenende katika upya wa uzima. Rej. Rum. 6:4; Kol. 2:12.

Papa Marehemu Wote
02 November 2023, 15:05