Tafuta

Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2022-2023 amepoteza viongozi 154 kwa kufariki dunia. Kati yao kuna Papa; Makardinali na Mapatriaki 6 pamoja na Maaskofu 147. Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2022-2023 amepoteza viongozi 154 kwa kufariki dunia. Kati yao kuna Papa; Makardinali na Mapatriaki 6 pamoja na Maaskofu 147.   (ANSA)

Katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023: Amefariki Papa, Makardinali 6 na Maaskofu 147

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, Makardinali, Mapatriaki na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023. Jumla ni viongozi 153 na kati yao kuna: Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Makardinali, Mapatriaki 6 pamoja na Maaskofu 147. Hawa ni viongozi waliojisadaka: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023 ameongoza Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto XVI: Makardinali, Mapatriaki, Maaskofu wakuu na Maaskofu waliofariki dunia kuanzia tarehe 31 Desemba 2022 hadi tarehe 23 Oktoba 2023. Hawa ni viongozi waliojisadaka kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amewaita kwenye makao ya uzima wa milele kwani yote yamekamilika, “Consummatum est.” Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2022-2023 amepoteza viongozi 147 kwa kufariki dunia. Kati yao kuna Makardinali na Mapatriaki 6. Pamoja na Maaskofu 147. Kanisa Barani Afrika limewapoteza Maaskofu 21 na Kardinali mmoja. Ibada ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaombea Waamini Wote Marehemu inapata chimbuko lake katika asili ya mwanadamu. Kumbukumbu hii inanogeshwa na Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Rej. Kol 1:18. Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanajiunga na Kristo Yesu na kuanza kutembea katika mwanga wa Pasaka. Rej. Rum 6:3-4. Huu ni ushirika na Kanisa ambalo bado linasafiri huku bondeni kwenye machozi na watakatifu wa mbinguni. Rej. LG 49. Baba Mtakatifu Benedikto XVI amekuwa ni Papa wa 265. Kumbukumbu yake ya kudumu itaendelea kubaki katika sakafu ya moyo wa Kanisa na binadamu wote katika ujumla wao. Joseph Aloisius Ratzinger, aliyechaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 19 Aprili 2005, alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927 huko Markti nchini Ujerumani. Baada ya masomo na majiundo yake ya: Kikristo, kiakili na kiutu akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 29 Juni 1951 wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani.

Papa Benedikto XVI: Chemchemi ya mageuzi Sekretarieti kuu ya Vatican
Papa Benedikto XVI: Chemchemi ya mageuzi Sekretarieti kuu ya Vatican

Tangu wakati huo, vipaji vyake vilianza kung’ara na kuwa ni kati ya wanataalimungu mahiri waliojipambanua katika miaka 1950 ndani na nje ya Ujerumani. Akabahatika kupata nafasi ya kufundisha vyuo kadhaa vya taalimungu nchini Ujerumani. Katika kipindi cha mwaka 1962 akabahatika kuteuliwa kuwa ni msaidizi binafsi wa Kardinali Joseph Fring na hivyo kushiriki katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tarehe 28 Mei 1977, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising na tarehe 27 Juni 1977 akateuliwa kuwa Kardinali. Hili ni tukio ambalo liliwashangaza watu wengi, kwani Askofu mkuu Joseph Ratzinger hakuwa na uzoefu sana katika shughuli za kichungaji kama Askofu. Akaliongoza Jimbo kuu la Munich na Freising kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1982. Tangu mwaka 1982 hadi mwaka 2005 alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa; Rais wa Tume ya Taalimungu Kimataifa pamoja na Tume ya Biblia Kimataifa pamoja na Dekano wa Baraza la Makardinali. Tarehe 8 Aprili 2005 kama Dekano wa Makardinali akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Papa Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo
Papa Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo

Tarehe 19 Aprili 2005 akachaguliwa kuwa Papa wa 265, akiwa na umri wa miaka 78 na kuchagua kuitwa Benedikto XVI. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa iliyosheheni unyenyekevu mkubwa, alisema, baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II aliyekuwa maarufu sana, Makardinali wamemchagua yeye, mtu wa kawaida na mfanyakazi katika shamba la Bwana kuwa Papa, lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatambua jinsi ya kuendeleza kazi yake hata kwa kutumia vyombo dhaifu kama yeye. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akajiweka chini ya sala na maombezi ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tarehe 24 Aprili akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kusimikwa rasmi kuwa ni Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 7 Mei akasimikwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika maisha na utume wake alikazia zaidi: Imani, Matumaini na Mapendo mambo msingi ambayo yangewawezesha waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, (1858) sanjari na Kumbukumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), Baba Mtakatifu Benedikto XVI baada ya Makardinali kuwapigia kura wenyeheri watatu waliokuwa wanatarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu alipoamua kwa hiyari yake mwenyewe, kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Akafariki dunia 31 Desemba 2022.

Papa Benedikto XVI alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2022
Papa Benedikto XVI alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2022

Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., alizaliwa tarehe 21 Juni 1959, Jimboni Wa, nchini Ghana. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, tarehe 5 Desemba 1986 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 18 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, amekuwa ni Paroko msaidizi kwenye Parokia la Livulu, Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1996 alikuwa masomoni kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian akichukua masomo ya Sayansi ya Biblia na baadaye akatunukiwa Shahada ya Uzamivu katika somo la Taalimungu Biblia. Kunako mwaka 1996 hadi mwaka 1999 akatumwa nchini Tanzania kama mlezi kwenye nyumba ya Shirika la Wamissionari wa Afrika, huko Kahangala, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, hapa watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza wanamkumbuka kwa utume wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Hapa ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2004 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa nyumba ya malezi huko Tolosa, nchini Ufaransa. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2010 akachaguliwa kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, maarufu kama “White Fathers.”

Papa Benedikto XVI alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2022
Papa Benedikto XVI alifariki dunia tarehe 31 Desemba 2022

Kunako mwaka 2010 akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, akiwa ni Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuliongoza Shirika hili tangu kuanzishwa kwake! Amekuwa pia ni Makamu mkuu wa Taasisi ya Masomo ya Kiarabu na Kiislam mjini Roma, PISAI. Kunako mwaka 2015 alishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia baada ya kuchaguliwa kuwakilisha Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Duniani kuanzia tarehe 4-25 Oktoba 2015. Tarehe 17 Februari 2016 akateuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Wa nchini Ghana na kuwekwa wakfu tarehe 7 Mei 2016. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, liliadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 huko Accra, nchini Ghana kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Umiliki wa SECAM: Usalama na Uhamiaji Barani Afrika na Visiwani na kumchagua Askofu Richard Kuuia Baawobr, WF., kuwa Rais wa SECAM. Tarehe 27 Agosti 2022, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Kardinali. Tarehe 27 Novemba 2022 akafariki dunia katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Kwa ufupi kabisa, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 35, kama Askofu akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 6 na kama Kardinali, Mshauri wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa muda wa miezi miwili tu, matendo makuu ya Mungu.

Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea Papa Benedikto XVI na Maaskofu
Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea Papa Benedikto XVI na Maaskofu

Maaskofu wakuu na Maaskofu waliofariki dunia kutoka Barani Afrika ni kama ifuatavyo: Askofu José Nambi wa Jimbo Katoliki la Kwito-Bié, Angola; Askofu mstaafu Marie-Edouard Mununu Kasiala, O.C.S.O. wa Jimbo Katoliki la Kikwit, DRC.; Askofu Mstaafu Erasmus Desiderius Wandera wa Jimbo Katoliki Soroti, Uganda; Askofu Mstaafu Mário Lucunde wa Jimbo Katoliki la Menongue, Angola; Askofu Mkuu mstaafu Joseph Edra Ukpo wa Jimbo kuu la Calabar, Nigeria; Bishop Angel Askofu Floro Martínez, I.E.M.E. Jimbo Katoliki la Gokwe, Zimbabwe; Askofu mstaafu José Francisco Moreira dos Santos, O.F.M. Cap. wa Jimbo Katoliki la Uije, Angola; Askofu Mstaafu Albert Edward Baharagate Akiiki wa Jimbo Katoliki la Hoima, Uganda; Askofu Mstaafu Senan Louis O’Donnell, O.S.A. wa Jimbo Katoliki la Maiduguri, Nigeria; Askofu Mkuu mstaafu Francisco Viti wa Jimbo kuu la Huambo, Angola; Askofu Mstaafu Kyrillos Kamal William Samaan wa Jimbo Katoliki la Kikoptik la Assiut {Lycopolis}Misri. Wegine ni: Askofu Mstaafu Macram Max Gassis, M.C.C.I. wa Jimbo Katoliki la  El Obeid, Sudan Kongwe; Askofu mkuu mstaafu Joachim N’Dayen wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati; Askofu mstaafu Wenceslas Compaoré Jimbo Katoliki la Manga, Burkina Faso; Askofu Mkuu mstaafu Paul Kamuza Bakyenga wa Jimbo kuu la Mbarara, Uganda; Askofu Mstaafu Paul Darmanin, O.F.M. Cap. wa Jimbo Katoliki la Garissa, Kenya; Askofu Mkuu Mstaafu Roger Pirenne, C.I.C.M. wa Jimbo kuu la Bertoua, Cameroon; Askofu Mkuu Mstaafu Marcel Honorat Léon Agboton wa Jimbo kuu la Cotonou, Benin; Askofu mkuu Mstaafu Marie-Daniel Dadiet wa Jimbo kuu la Korhogo, Pwani ya Pembe pamoja na Askofu MstaafuManuel Chuanguira Machado wa Jimbo Katoliki Gurué, Msumbiji.

Wasifu BXVI

 

 

 

03 November 2023, 16:42