Tafuta

Jumanne tarehe 28 Novemba 2023 amekutana na kuzungumza na wahanga wa nyanyaso za kijinsia kutoka Jimbo Katoliki la Nantes, nchini Ufaransa. Jumanne tarehe 28 Novemba 2023 amekutana na kuzungumza na wahanga wa nyanyaso za kijinsia kutoka Jimbo Katoliki la Nantes, nchini Ufaransa.  (©JenkoAtaman - stock.adobe.com)

Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia Ni Usaliti wa Utu na Heshima ya Binadamu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kashfa ya usaliti wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, ambazo Mwenyezi Mungu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa wahalifu kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kuwa watu wema na wa kweli. Changamoto na mwaliko kwa wahalifu hawa ni kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili waweze kuwa ni watu wema na wa kweli katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa.

Wahanga wa nyanyaso za kijinsia kutoka Ufaransa
Wahanga wa nyanyaso za kijinsia kutoka Ufaransa

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 28 Novemba 2023 amekutana na kuzungumza na wahanga wa nyanyaso za kijinsia kutoka Jimbo Katoliki la Nantes, nchini Ufaransa. Wahanga hawa walikuwa wamesindikizwa na baadhi ya viongozi wa Kanisa kutoka nchini Ufaransa. Kikundi hiki, kilipata nafasi ya kuzungumza na Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM. Mkazo ukiwa ni umuhimu wa Kanisa kulinda utu, heshima na haki msingi za watoto; shuhuda zilizotolewa na wahanga wa nyanyaso za kijinsia; kwa kukutana na kuwasikiliza kama kielelezo makini cha utekelezaji wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiuu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Wahanga hawa wamepata pia fursa ya kusikiliza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; shuhuda; kumbukumbu pamoja na jitihada za Kanisa kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena katika maisha na utume wa Kanisa.

Nyanyaso za kijinsia ni ukatiliki dhidi ya utu, heshima na haki msingi
Nyanyaso za kijinsia ni ukatiliki dhidi ya utu, heshima na haki msingi

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kashfa ya usaliti wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, ambazo Mwenyezi Mungu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa wahalifu kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kuwa watu wema na wa kweli. Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM kwa niaba ya Baba Mtakatifu imesikiliza shuhuda, ili kulisaidia Kanisa kuendelea kujizatiti katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto, jukumu linalopaswa kutekelezwa kwa ushirikiano wa watu wote wa Mungu, kwanza kabisa kwa kuvunjilia mbali ukimya ambao umetawala kwa muda mrefu, tayari kuanza mchakato wa kusikiliza sanjari na kuwaheshimu wahanga wa nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hii ni shughuli pevu ambayo wadau mbalimbali wanapaswa kujifunza ili kutembea kwa pamoja na kuendelea kujikita katika majadiliano ya kweli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana inayopaswa kuvaliwa “njuga” na Mama Kanisa. Sera na mbinu mkakati vinapaswa kuibuliwa, ili iweze kutekelezwa kwa weledi mkubwa, tayari kuanzisha mazingira yatakayokuwa ni rafiki na salama kwa malezi na makuzi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu amewaambia wahanga kwamba, watambue kuwa Kanisa lipo tayari kuwasikiliza na kwamba, kuanzishwa kwa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, kunapania kuwalinda wahanga wa nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Nyanyaso
30 November 2023, 15:03