Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, Makardinali, Mapatriaki na Maaskofu waliofariki dunia 2022-2023 Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, Makardinali, Mapatriaki na Maaskofu waliofariki dunia 2022-2023  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ibada ya Misa Takatifu Kwa Ajili ya Kumwombea Papa Benedikto XVI, Makardinali na Maaskofu

Papa Francisko, Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, Makardinali, Mapatriaki na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: huruma ya Mungu na kwamba, Mwenyezi mungu atafuta machozi katika nyuso zote; Fadhila ya unyenyekevu ni muhimu sana kwa watenda kazi katika shamba la Bwana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawaombea watoto wake ili watakaswe, ikiwa kama wanahitaji kutakaswa kabla ya kupokelewa mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele wakati miili yao inapobaki ardhini ikingoja kurudi kwa Kristo Yesu na ufufuko wa wafu. “Sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya Kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba, katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu.” (KKK 962). Kanisa linasali na kuwaombea waamini marehemu kusudi wapate msaada wa kiroho na waamini walio bado hai wapate matumaini ya uzima ujao mbinguni. Ni muhimu na vema kuwaombea wafu, kwani hata kama wamekufa katika neema na upendo kwa Mungu, inawezekana bado wanahitaji utakaso wa mwisho ili waweze kuingia katika furaha ya uzima wa milele. Mtakatifu Ireneo anasema utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai. Maisha ya mwanadamu, mkristo, mbatizwa huwa na aina mbili ya kifo. Kifo cha kwanza ni kwa njia ya Ubatizo na imani: Rej. Rum. 1:6 ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo, tumejiunga na Kristo Yesu aliyekufa na kufufuka kwa wafu. Rej. KKK 628. Sakramenti ya Ubatizo ambao alama yake ya asili na timilifu ni kuzamishwa kunako ashiria bayana kushuka kaburini kwa mkristo anayeifia dhambi pamoja na Kristo Yesu ili aishi maisha mapya kwa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka kwa wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na waamini waenende katika upya wa uzima. Rej. Rum. 6:4; Kol. 2:12. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, Makardinali, Mapatriaki na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Papa Benedikto XVI na Makardinali
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Papa Benedikto XVI na Makardinali

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: huruma ya Mungu na kwamba, Mwenyezi Mungu atafuta machozi katika nyuso zote; Fadhila ya unyenyekevu ni muhimu sana kwa watenda kazi katika shamba la Bwana. Mwinjili Luka anaelezea kwa kina na mapana imani kubwa ya akida ilivyopelekea kuponywa kwa mtoto wake wa pekee pamoja na Kristo Yesu kumfufua kijana wa Naini. Rej. Lk 7:1-17. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anasema Injili ya Msamaria mwema ni dira na falsafa ya Kristo Yesu yenye “moyo wenye macho” unaosheheni upendo unaomwilishwa katika huduma. Rej. Deus caritas est, 31. Anakaza kusema, imani ni mchakato unaomwezesha mwamini kukutana na Kristo Yesu, ambaye mapigo ya moyo wake yanaelekezwa kwa waja wake na kwamba, anawaonea huruma waja wake wanaoteseka. Kristo Yesu, mbele ya kifo na uchungu anasimama na kuwaonea huruma waliopatwa na mikasa hii, jambo hili linadhihirisha ukuu wa Kristo Yesu unaodhihirisha kwa kumfufua yule kijana wa Naini na kwamba, Moyo wake Mtakatifu umesheheni huruma. Ufufuko wa kijana wa Naini ni kielelezo cha zawadi ya maisha inayoshinda utamaduni wa kifo, mwaliko kwa waamini kunyanyua macho yao na kuonesha huruma kwa wale wote wanaoishi katika machungu ya kuondokewa na wapendwa wao. Mwinjili Luka anasema, “Yesu akakaribia, akaligusa jeneza.” Kadiri ya Mapokeo ya kale, kugusa jeneza au maiti kilikuwa ni kitendo ambacho hakina mvuto wala mashiko kwa sababu kwa wale waliogusa jeneza au maiti walihesabiwa kuwa ni najisi, lakini Kristo Yesu alivunjilia mbali tamaduni na mapokeo haya, ili kuonesha ukaribu, huruma na upendo wa dhati, tayari kumfariji yule mwanamke wa Naini aliyekuwa anaomboleza kwa kifo cha kijana wake na kumwambia “Usilie.”

Moyo wa macho unasheheni upendo usiokuwa na kikomo
Moyo wa macho unasheheni upendo usiokuwa na kikomo

Katika sehemu mbalimbali za Injili zinamwonesha Kristo Yesu akilia! Wito huu wa kumnyamazisha mwanamke wa Naini ulionesha ukomo wa kilio chake na kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya kwenye Agano la Kale akisema, “Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote.” Rej. Is 25: 8. Kristo Yesu alitokwa machozi, ili kukausha machozi ya waja wake. Muujiza huu unaonesha huruma ya hali ya juu aliyokuwa nayo Kristo Yesu kwa wajane, yatima na wageni waliokuwa wakijiaminisha mbele ya Mungu, ambaye alikuwa ni mtetezi wao wa daima, changamoto na mwaliko kwa waamini hata leo hii kuwapatia kipaumbele cha kwanza, ili mwisho wa safari ya hapa duniani, waweze kuwapokea huko mbinguni. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, anazidi kufafanua kwamba, wajane, yatima na wageni; kwa asili ni watu wanyenyekevu. Hata waswahili wanasema, “Yatima hadeki.” Hawa ni watu walioweka imani na matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kumpatia kipaumbele cha kwanza. Hawa ndio maskini wa roho wanaompendeza Mwenyezi Mungu na hivyo kuonesha ile njia iendayo mbinguni. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaangalia imani na unyenyekevu wa waja wake. Unyenyekevu wa Kikristo unafumbata ile hali ya mtu kujisikia kuwa mhitaji mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kutengeneza mazingira yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kumjibu Mungu kwa imani. Mwenyezi Mungu ni mnyenyekevu na asili ya unyenyekevu wenyewe kama ilivyo kwa Mwanaye wa pekee, Kristo Yesu na kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini sana wanyenyekevu wa moyo! “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Lk 14:11.

Mungu anawapenda na kuwathamini sana wanyenyekevu wa moyo
Mungu anawapenda na kuwathamini sana wanyenyekevu wa moyo

Baba Mtakatifu Benedikto XVI baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa alisikika akisema kwamba, baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II, Makardinali tarehe 19 Aprili 2005 walimchagua yeye mtumishi mnyenyekevu katika shamba la Bwana kuliongoza Kanisa.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, Papa, Makardinali na Maaskofu wanaitwa kuwa watumishi wanyenyekevu, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuhudumia na wala si kuhudumiwa, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa shamba la Bwana, yaani Kanisa la Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake, akiwataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie uso wenye huruma na moyo wa unyenyekevu na kamwe wasichoke kumwomba Mwenyezi Mungu zawadi hizi kwani ni katika huruma na moyo wa unyenyekevu, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake zawadi ya maisha inayoshinda kifo. Huu ni mwaliko wa kuendelea kusali na kuwaombea ndugu, jamaa, na marafiki wote marehemu. Kanisa limewakumbuka na kuwaombea viongozi wa Kanisa waliofariki dunia kati yam waka 2022 hadi Novemba 2023. Hawa walikuwa ni wachungaji, mwenye huruma na wanyenyekevu wa moyo, kwa maana maisha yao yalipigwa chapa ya uwepo wa Mungu, chemchemi ya amani ya kweli. Sasa wanafurahia pamoja na Bikira Maria aliyenyanyuliwa juu kutokana na unyenyekevu wake.

Papa B16 Maaskofu
03 November 2023, 16:17