CHARIS Ni Chombo Cha Huduma Cha Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa: Umoja na Ushirika
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” “International Catholic Charismatic Renewal Services.” Katika asili yake, neno hili maana yake ni “Neema au zawadi maalum kutoka kwa Roho Mtakatifu.” Kitengo hiki kinatoa huduma ya kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki na kilizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Siku hii pia ilizinduliwa Katiba inayosimamia shughuli zote zinazoendeshwa na CHARIS kama dira na mwongozo wa kusimamia na kukuza imani ya Kanisa Katoliki. Zote hizi ni kazi za Roho Mtakatifu zinazoendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi kitengo hiki, hakitakuwa na mamlaka juu ya Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, bali wataendelea kutekeleza dhamana na shughuli zao kama kawaida, chini ya usimamizi wa Maaskofu mahalia. Kila tawi linaweza kupata huduma na msaada wa kiufundi utakaokuwa unatolewa na CHARIS sehemu mbalimbali za dunia. Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa Nyumba ya Kipapa ndiye aliyeteuliwa kuwa Baba wa maisha ya kiroho wa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki: “International Catholic Charismatic Renewal Services.” Monsinyo Miguel Delgado Galindo, Mwakilishi wa Mashirika na Vyama vya Kitume katika Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, wengine wanapenda kukiita kama “Mkondo” unaovuviwa na Roho Mtakatifu ambaye ndiye aliyepewa dhamana ya kumshuhudia Kristo Yesu kwa kutakatifuza, kufundisha, kuongoza, kukumbusha pamoja na kuwasaidia waamini kutumia karama zao kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Hiki ni chama kinachopaswa kustawisha karama za binadamu, ili waweze kupata wokovu kwa kuendelea kumakinika na karama zao za kiroho kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ukuaji na ustawi wa Kanisa sanjari na wokovu wa walimwengu wote. Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango wa Wakarismatiki Wakatoliki katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Wakarismatiki wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uekumene wa kiroho, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa. Wanachama wake wanapaswa kujikita katika toba na wongofu wa kichungaji na kimisionari, kwa kuonesha upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe na hatimaye, akombolewe! Hiki ni chama ambacho kina tofautiana kwa mtindo wa maisha ya sala na huduma, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwaunganisha wanachama wake wote katika utofauti wao, ili kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa. Hii ni sehemu ya marekebisho makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umoja na utofauti kadiri ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Ni katika muktadha huu wa kumbukumbu ya miaka mitano tangu Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha lilipopitisha Katiba ya CHARIS, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wanaitwa, Wanabadilishwa na Kutumwa.” Tangu tarehe 2 hadi tarehe 4 Novemba 2023 wajumbe wamekuwa wakishiriki katika makongamano yaliyojadili: mchakato wa uinjilishaji; Ujenzi wa Jumuiya ya Kikristo; Ustawi, maendeleo ya binadamu; Sala; Umoja wa Wakristo pamoja na Vikundi vya Sala.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia ukomavu wa Kikanisa katika maisha ya sala, CHARIS isaidie mchakato wa ujenzi wa ushirika katika tofauti zao msingi; ujenzi wa seminari katika maisha mapya; Katiba ya CHARIS pamoja na mambo mengine inakazia matumizi ya karama ndani ya Kanisa; Utakatifu wa maisha unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo pamoja na kuwa makini kung’amua karama za Roho Mtakatifu na kamwe wasimezwe na uchu wa mali na madaraka na kutaka kujimwambafai. CHARIS ni chombo cha huduma ya Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa katika mchakato wa ujenzi wa ushirika ili kuboresha hali ya maisha na utume wa Wakarismatiki ulimwenguni, kielelezo cha ukomavu wa Kikanisa unaofumbatwa katika maisha ya sala. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Roho Mtakatifu kwa kipindi hiki cha neema, ujenzi wa ushirika pamoja na kuwa na mwono wa mbali kwa kutambua na kuthamini karama na mapaji yanayoibuliwa na Roho Mtakatifu mintarafu mazingira, kitamaduni, kijamii na kikanisa. Ni katika muktadha wa mang’amuzi, ushirikishwaji na ufahamu, CHARIS inaweza kuwasaidia waamini kuwa na mwono mpana zaidi wa karama na wa kikanisa. Baba Mtakatifu anawatia shime Wakarismatiki kupanua na kuendeleza seminari za maisha mapya, mahali muafaka pa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu yaani: Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Kristo Yesu anaendelea kuishi kwa njia ya Neno lake, Roho wake Mtakatifu na katika Kanisa lake, waamini wanaweza kukutana naye ikiwa kama wataunda mazingira ya ukarimu, neema na baraka, upatanisho na upyaisho wa maisha.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Seminari hizi za maisha mapya zisaidie majiundo ya waamini katika medani mbalimbali za maisha zinazoweza kutekelezwa hata katika ngazi ya Kiparokia na waamini katika hali na mazingira yao, tayari kupambana na hali yao, ili kujipatia toba na wongofu wa ndani. Huu ni moto wa kuotea mbali ambao hauna budi kukolezwa kwa njia ya hija za majiundo yanayosaidia kupyaisha ile neema ya utakaso, tayari kukuza na kukomaza imani kwa njia ya sala, maisha adili na matakatifu; kwa ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa; matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na ushiriki wa maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuendeleza karama na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa zima na kwamba, CHARIS inapaswa kuelekeza huduma yake kwa ajili ya Kanisa zima, lakini kipaumbele cha kwanza ni karama zile zinazosaidia mchakato wa uinjilishaji, shughuli za kimisionari; utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Pili ni kuhimiza ongezeko la maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha kwa waamini wanaoishi uzoefu na mang’amuzi ya Ubatizo katika Roho Mtakatifu, wanapaswa kuendeleza toba na wongofu wa mtu binafsi na katika zawadi ya ukarimu ya mtu mwenyewe kwa Kristo Yesu na wengine. Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe wa CHARIS kwa huduma makini ya usaidizi, ushauri kwa Makanaisa mahalia ili kurejesha tena upyaisho wa kikarismatiki. Baba Mtakatifu anatoa angalisho kwa wanakarismatiki ili kamwe walisutumbukie katika majaribu ya uchu wa mali, madaraka na kutaka kujimwambafai.
Ni vyema, ikiwa kama viongozi wa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki kujiandaa kuwaachia vijana madaraka kwa kuwapatia mafunzo. Kumbe, vijana wapewe mafunzo ya mara kwa mara, kama sehemu ya maandalizi ya kuja kushika madaraka kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu amekuwakumbusha wajumbe kwamba, mwezi Juni 2019 walikutana katika ukimya kwa ajili ya kuombea amani, kama sehemu ya kumbukizi ya Mkutano wa Marais wa Palestina na Israeli waliokutana kwa ajili ya kusali pamoja mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, vita huharibu kumbukumbu ya hatua kubwa iliyopigwa kuelekea upatikanaji wa amani. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kamwe wasiruhusu kumbukumbu hii kupokwa. Kwa upande wake Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa Nyumba ya Kipapa, ambaye ndiye Baba wa maisha ya kiroho wa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki na tafakari yake imenogeshwa na maneno ya Nabii Isaya yasemayo “Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani” Is 43:18 yaani baada ya maadhimisho ya ya takribani miaka 56 ya uwepo na huduma za Chama cha Huduma ya Upyaisho ya Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa: “International Catholic Charismatic Renewal Services”, Chama cha Kidugu cha Wakarismatiki wa Jumuiya za Agano: “Fraternity of Charismatic Covenant Communities” pamoja na Chama cha Umoja wa Wakarismatiki, “Fellowship” umekoma na hivyo kutoa fursa kwa CHARIS kuratibu na kutoa huduma Kimataifa, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja wa Wakristo na kuendelea kuwatia moyo wakristo kuanza sura mpya ya uinjilishaji yenye mhuri wa furaha. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kila mahali, katika wakati huu, wao binafsi wakutane upya na Kristo Yesu na wawe tayari kumruhusu kukutana nao, changamoto ya kumwilisha mwaliko huu, kila siku ya maisha.