Tafuta

“Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko nchini Ufaransa. “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko nchini Ufaransa. 

Waraka wa Papa Francisko: Uaminifu Miaka 150 Kuzaliwa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko Alençon nchini Ufaransa anasema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anaonesha jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa: Upendo na imani katika huruma ya Mungu. Yaani upendo wa Mungu hauna kikomo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D., alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 huko Alençon, Ufaransa, na baadaye akahamia mjini Lisieux, Ufaransa, na kufariki dunia tarehe 30 Septemba 1897. Jina lake la kitawa ni Thérèse Françoise Marie Martin, maarufu pia kama Theresa wa Lisieux. Anaheshimiwa na Mama Kanisa kama Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Hata katika udogo wake Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alijitokeza kama mtaalam wa elimu ya upendo inayosimikwa katika unyofu wa hali ya juu na jinsi ambavyo kwa neema alivyoelewa na kutekeleza Injili ya Kristo Yesu katika maisha yake ndani ya monasteri ya Wakarmeli Peku. Theresa alitamani sana kuwa mtume ili kuokoa roho za watu wengi. Alitamani awe mhubiri, mmisionari na shuhuda. Hata hivyo ilikuwa tu baada ya yeye kujitoa mwenyewe na kujikabidhi kwa upendo wenye huruma ndipo alipogundua wito ambao Mungu alimwitia. Alisema hivi “Nimelewa kwamba upendo hushikilia miito yote. Natambua kwamba tamaa zangu zote zimetimilika. Nimepata wito wangu. Katika moyo wa Kanisa, mama yangu, mimi nitakuwa upendo.” Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko Alençon nchini Ufaransa anasema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anaonesha jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa: Upendo na imani katika huruma ya Mungu. Katika waraka wake wa “Njia ndogo ya tumaini na upendo” anawahimiza Wakristo kuamini katika upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo sanjari na kujipatia uzoefu wa kukutana na Kristo Yesu kwa uwazi kwa njia ya wengine. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 25 na Papa Pio XI akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 17 Mei 1925 na tena Mama Kanisa akamtangaza kuwa ni Mlinzi na Msimamizi wa Utume wa Kanisa.

Masalia ya Mt. Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Masalia ya Mt. Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa

“Njia ndogo ya tumaini na upendo”, njia ya "utoto wa kiroho” yaani njia ya maisha ya kiroho inayofundisha kufuata Injili ya Kristo Yesu kwa kujifanya wadogo aliyoielekeza inafundisha kutimiza sharti la Yesu: “Akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi.” Mt 18:3-5. Njia hiyo inatia moyo wa kujitoa kikamilifu bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Mwenyewe aliifuata hata akasema: “Kupenda ni kutoa yote, na kujitoa pia”. “Sijawahi kumnyima chochote Mungu mwema!” Siri yake ni nguvu ya upendo, ambao Theresa alitambua ndio wito wake katika Kanisa: kuwa moyo wa Mwili wa Kristo ili kusaidia viungo vyake vyote kufanya kazi vizuri. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu na kuchapishwa rasmi tarehe 15 Oktoba 2023, katika kumbukumbu ya Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa, huyu ni mtawa aliyebahatika kuwa na mwanga angavu wa hekima inayosimikwa katika utakatifu wa maisha, ukweli na imani thabiti, zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Theresa wa Avila, alikirimiwa nguvu na upendo wa ajabu unaojionesha katika sala na maandiko yake. Kwa hakika alikuwa ni “mwanamke wa shoka” katika maisha ya: Sala, Liturujia ya Kanisa na Mafundisho yake, kiasi cha kujisikia kuwa pamoja na Kanisa, kama shuhuda na chombo cha upatanisho na mageuzi makubwa ndani ya Kanisa. Utume wake katika maisha ya kiroho, ni amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa unaowafanya waamini wote kujisikia kuwa ni sehemu ya watoto wa Mungu na Kanisa. Mtakatifu Theresa wa Avila, anatambulika na kupendwa na watu wengi, sehemu mbalimbali za dunia. Huyu ni amana na utajiri wa Kanisa anayeshuhudia  ukomavu wa imani.

Papa Francisko akitoa heshima zake kwa Masalia ya Mt. Theresa wa Mtoto Yesu
Papa Francisko akitoa heshima zake kwa Masalia ya Mt. Theresa wa Mtoto Yesu

Baba Mtakatifu anabainisha utambuzi uliofanywa na viongozi wakuu wa Kanisa kama ushuhuda na amana ya maisha ya kiroho kama yalivyotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu. Papa Leo wa XIII ndiye aliyemruhusu kuingia utawani akiwa na umri wa miaka 15. Papa Pio XI akamtangaza kuwa Mtakatifu mwaka 1925 na  mwaka 1927 Mlinzi na Msimamizi wa Utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 19 Oktoba 1997 akamtangaza kuwa Mwalimu wa Kanisa. Theresa ni mtoto wa tisa kuzaliwa na kitinda mimba kwenye familia ya Mzee Luigi Martin na Zeria Guerin ambao sasa Kanisa limewaweka kuwa mfano na kioo kwa familia zote za Kikristo. Tarehe 19 Oktoba 2008 Papa Benedikto XVI aliwatangaza kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 katika Maadhimisho ya Mwaka wa Familia Baba Mtakatifu Francisko akawatangaza kuwa ni watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto wao kiimani na katika maadili ya kikiristo na hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amefanya Katekesi ya kina kuhusu maisha na utume wao ndani ya familia. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alikuwa na upendo wa dhati kabisa kwa Kristo Yesu na kama sehemu ya mang’amuzi yake ya maisha ya kiroho, kiasi cha kuwa kweli ni chemchemi ya furaha ya ndani, kwani alitambua kwamba, Kristo Yesu alimfahamu kutoka katika undani wa maisha yake, akampenda upeo, akawa ni kioo cha tafakari yake, kiasi cha kumwezesha kumwilisha fadhila hii ya upendo katika udogo wa maisha yake, huku akisindikizwa na Bikira Maria, na kuendelea kujifunza kupenda na kujisadaka bila ya kujibakiza. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alikuwa na upendo mkubwa kwa Kanisa uliokuwa unabubujika kutoka katika undani wa maisha yake kama alivyoshuhudia mwenyewe kwamba siri yake ni nguvu ya upendo, ambao Theresa aliutambua kuwa ndio wito wake katika Kanisa: kuwa moyo wa Mwili wa Kristo ili kusaidia viungo vyake vyote kufanya kazi vizuri.

Madhabahu ya Mt. Tehesa wa Mtoto Yesu
Madhabahu ya Mt. Tehesa wa Mtoto Yesu

Huu ni moyo wa Kanisa lisilokuwa na makuu, bali Kanisa linalopenda na kusimikwa katika fadhila ya unyenyekevu na huruma ya Mungu; Kanisa linalong’ara hata katika ulimwengu mamboleo bila kushangazwa na kashfa pamoja na mapungufu yake ya kibinadamu, lakini watu wanaweza kupenya katika kiini cha moyo wake ambao unawaka upendo unaopata chimbuko lake katika Sherehe ile ya Pentekoste ya kwanza, zawadi ya Roho Mtakatifu. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alitamani sana kwenda mbinguni, akasimama kidete kukutafuta na kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zake, yaliyosheheni matumaini na upendo, kiasi cha kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Francisko upendo ulimsukuma Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zake. Katika hali ya mateso, akitekeleza upendo wa hali ya juu katika mambo madogo madogo ya maisha ya kila siku, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alitimiza wito wake wa kuwa upendo katika moyo wa Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa la kimisionari halina budi kuzingatia mambo msingi, yale yaliyo mazuri zaidi, makubwa zaidi, ya kuvutia zaidi na wakati huo huo ya lazima zaidi, kwa kufanya ujumbe uwe rahisi bila kupoteza kina na ukweli wake na hivyo kuwa na nguvu pamoja na ushawishi mkubwa zaidi, lakini upendo ndicho kito cha thamani zaidi. Mchango madhubuti wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D., Bikira na Mwalimu wa Kanisa ni kuwawezesha waamini kuzingatia mambo msingi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika wanataalimungu, wana maadili wasomi wa maisha ya kiroho kujifunza mchango wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuteka matokeo ya kinadharia na ya vitendo, ya mafundisho ya Kanisa, ya shughuli za kichungaji, kibinafsi na kijamii kutoka kwayo. Kunahitajika ujasiri na uhuru wa ndani ili kuweza kutekeleza hayo!

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alitimiza wito wake kwa upendo kwa Kanisa
Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alitimiza wito wake kwa upendo kwa Kanisa

Baba Mtakatifu anabainisha umuhimu wa “Njia ndogo ya tumaini na upendo”, njia ya "utoto wa kiroho” ili kuondokana na masilahi ya mtu binafsi, ubinafsi na uchoyo, kwa kugeuza maisha kuwa ni zawadi, kwa kuonesha thamani ya urahisi, udogo na ukuu wa upendo unaoshinda uhalali wa sheria na mantiki za kimaadili zinazojaza maisha ya Kikristo na maagizo na hivyo kufungia nje ile furaha ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu na kuchapishwa rasmi tarehe 15 Oktoba 2023, kwa sala fupi anapomsihi Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu kwa kusema, "Mpendwa Mtakatifu Theresa, utusaidie daima kuamini kama ulivyofanya, katika upendo mkuu alionao Mwenyezi Mungu kwetu, ili tuweze kuiga kila siku njia ndogo ya tumaini na upendo kuelekea kwenye utakatifu wa maisha."

Waraka Theresa wa Mtoto Yesu
16 October 2023, 07:38