Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 22 Oktoba 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Mioyo inayowaka moto, na miguu inayotembea." Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 22 Oktoba 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Mioyo inayowaka moto, na miguu inayotembea."  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwengu 2023

Baba Mtakatifu anabainisha jinsi ambavyo katika kazi ya kimisionari Neno la Mungu huangaza na kubadili mioyo ya waamini. Kristo Mfufuka bado anabaki na kutembea na wafuasi wake ili wasikate tamaa. Umuhimu wa kulifahamu Neno la Mungu, Sakramenti ya Sadaka ya Yesu Msalabani, ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wawe tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwa kujikita katika wongofu wa kimisionari.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam.

Ndugu Wapendwa, Katika Dominika ya Misioni ya mwaka huu, nimechagua mada iliyoongozwa na hadithi ya wafuasi walipokuwa njiani kwenda Emau, katika Injili ya Luka (rej. 24:13-35): "Mioyo inayowaka moto, miguu inayotembea." Wafuasi hao wawili walikuwa wamechanganyikiwa na kufadhaika, lakini kukutana kwao na Kristo katika Neno na katika kuumega mkate kulichochea ndani yao hamu na shauku ya kuanza tena safari kuelekea Yerusalemu na kutangaza kwamba Bwana alikuwa amefufuka kweli. Katika masimulizi ya Injili, tunaona badiliko hili kwa wafuasi kupitia taswira chache zinazodhihirika: mioyo yao iliwaka ndani yao waliposikia Maandiko yakielezwa na Yesu, macho yao yalifunguliwa walipomtambua, na hatimaye, miguu yao ikashika njia. Kwa kutafakari taswira hizi tatu, zinazoakisi safari ya wafuasi wamisionari wote, tunaweza kuhuisha ari yetu ya uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo. Mioyo yetu iliwaka ndani yetu “alipotufafanulia Maandiko.” Katika kazi ya umisionari, Neno la Mungu huangaza na kubadilisha mioyo. Njiani kutoka Yerusalemu kwenda Emau, mioyo ya wafuasi hao wawili ilikuwa imedhoofika, kama inavyooneshwa na nyuso zao zenye huzuni, kwa sababu ya kifo cha Yesu, ambaye walikuwa wamemwamini (taz.17). Wakikabiliwa na kushindwa kwa Bwana aliyesulibiwa, matumaini yao kwamba yeye ndiye Masiha yaliporomoka (rej. aya 21). Basi, “walipokuwa wakizungumza na kujadiliana pamoja, Yesu mwenyewe akakaribia, akatembea pamoja nao” (aya 15). Kama vile alipowaita wafuasi mara ya kwanza, vivyo hivyo sasa, katikati ya mshangao wao, Bwana anachukua hatua; anawakaribia na kutembea pamoja nao. Vivyo hivyo pia, kwa huruma yake kuu, hachoki kuwa pamoja nasi, licha ya udhaifu wetu wote, mashaka, kasoro, na mfadhaiko na kukata tamaa kunakotufanya tuwe “wajinga na wenye mioyo mizito” (aya 25), watu wenye Imani haba. Leo, kama ilivyokuwa wakati huo, Bwana Mfufuka anabaki karibu na wafuasi wake wamisionari na kutembea pamoja nao, hasa wanapohisi kuchanganyikiwa, kukatishwa tamaa, kuogopa fumbo la uovu linalowazunguka na kutaka kuwaelemea. Hivyo, “tusijiruhusu wenyewe kupoteza tumaini!" (Evangelii gaudium, 86). Bwana ni mkuu kuliko shida zetu zote, zaidi ya yote ikiwa tutakumbana nazo katika utume wetu wa kutangaza injili ulimwenguni. Kwa maana mwishowe, utume huu ni wake na sisi si chochote zaidi ya watendakazi wenzake wanyenyekevu, "watumishi tusio na faida" (taz. Lk 17:10).

Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa
Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa

Ninatamani kueleza ukaribu wangu katika Kristo kwa wamisionari wanaume na wanawake wote ulimwenguni, hasa kwa wale wanaovumilia aina yoyote ya shida. Marafiki wapendwa, Bwana Mfufuka yu pamoja nanyi daima. Anaona ukarimu wenu na majitoleo mnayofanya kwa ajili ya utume wa uinjilishaji katika nchi za mbali. Si kila siku ya maisha yetu ni ya utulivu na isiyo na mawingu, lakini tusisahau kamwe maneno ya Bwana Yesu kwa marafiki zake kabla ya mateso yake: "Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu!" (Yn 16:33). Baada ya kuwasikiliza wale wafuasi wawili walipokuwa njiani kuelekea Eamau, Yesu Mfufuka, “akianza na Musa na manabii wote, akawaeleza yaliyonenwa katika Maandiko yote kumhusu yeye” (Lk 24:27). Mioyo ya wafuasi ilichangamka, kama walivyoambiana siri baadaye: "Je! mioyo yetu haikuwa ikiwaka ndani yetu alipokuwa akisema nasi njiani na kutufungulia Maandiko?" (aya 32). Yesu mwenyewe ndiye Neno lililo hai, ambaye peke yake anaweza kuifanya mioyo yetu kuwaka ndani yetu, kama anavyoiangaza na kuibadilisha. Kwa namna hii, tunaweza kuelewa vyema kauli ya Mtakatifu Jerome kwamba, “kutojua Maandiko ni kutomjua Kristo” (Commentary on Isaiah, Prologue). "Bila ya Bwana kututambulisha, haiwezekani kuelewa Maandiko Matakatifu kwa kina; lakini kinyume chake pia ni ukweli vilevile: bila Maandiko Matakatifu, matukio ya utume wa Yesu na ya Kanisa lake ulimwenguni yanabaki kuwa yasiyoweza kuelezeka" (Aperuit Illis 1). Hivyo, ujuzi wa Maandiko ni muhimu kwa maisha ya Kikristo, na hata zaidi kwa kumhubiri Kristo na Injili yake. Vinginevyo, unawashirikisha nini wengine kama sio mawazo yako na mipango yako? Moyo baridi hauwezi kamwe kufanya mioyo mingine kuwaka! Hivyo tuwe tayari kila wakati kuambatana na Bwana Mfufuka anapotufafanulia maana ya Maandiko. Na aifanye mioyo yetu kuwaka ndani yetu; na atuangazie na kutugeuza, ili tuweze kutangaza fumbo lake la wokovu kwa ulimwengu kwa nguvu na hekima itokayo kwa Roho wake.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

2. Macho yetu “yalifunguliwa na kumtambua” katika kuumega mkate. Yesu katika Ekaristi ndiye chanzo na kilele cha utume. Ukweli kwamba mioyo yao iliwaka kwa ajili ya neno la Mungu uliwasukuma wafuasi wa Emau kumwomba Msafiri huyo wa ajabu kukaa nao jioni ilipokuwa inakaribia. Walipokusanyika kuzunguka meza, macho yao yakafumbuliwa na wakamtambua alipoumega mkate. Kipengele mahususi kilichofungua macho ya wafuasi ulikuwa ni mlolongo wa vitendo vilivyofanywa na Yesu: alitwaa mkate, akaubariki, akaumega na kuwapa. Hizo zilikuwa ni ishara za kawaida za mkuu wa kaya ya Kiyahudi, lakini, kwa kufanywa na Yesu Kristo kwa neema ya Roho Mtakatifu, yalihuisha kwa wanameza wanzake wawili ishara ya kugeuza mikate na zaidi ile ya Ekaristi, Sakramenti ya sadaka ya Msalabani. Lakini wakati huo huo walipomtambua Yesu katika kuumega mkate, "alitoweka mbele ya macho yao" (Lk 24:31). Hapa tunaweza kutambua ukweli muhimu wa imani yetu: Kristo, ambaye anamega mkate, sasa anakuwa mkate uliomegwa, walioshiriki wafuasi na kuliwa nao. Haonekani tena, kwa kuwa sasa alikuwa ameingia mioyoni mwa wafuasi, ili kuwafanya kuwaka zaidi, na hii inawasukuma kuondoka mara moja ili kuwashirikisha wengine uzoefu wao wa pekee wa kukutana na Bwana Mfufuka. Kristo Mfufuka, basi, ndiye anayeumega mkate na, wakati huo huo, mkate wenyewe, unaomegwa kwa ajili yetu. Hivyo, kila mfuasi mmisionari ameitwa kuwa, kama Yesu na ndani yake, kwa njia ya kazi ya Roho Mtakatifu, mmoja anayeumega mkate na mkate unaomegwa kwa ajili ya ulimwengu. Hapa ikumbukwe kwamba kuumega mkate wetu wa vitu halisi na wenye njaa kwa jina la Kristo tayari ni kazi ya utume wa kikristo. Ni zaidi sana kuumega mkate wa Ekaristi, ambaye ni Kristo mwenyewe, ni kazi ya utume ulio na ubora zaidi, kwani Ekaristi ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kama Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI alivyosema: "hatuwezi kutunza kwa ajili yetu upendo tunaosherehekea katika Sakramenti (ya Ekaristi). Kwa asili yake, unadai kushirikishwa kwa kila mtu. Kitu ambacho ulimwengu unahitaji ni upendo wa Mungu, kukutana na Kristo na kumwamini. Kwa sababu hiyo Ekaristi si tu chanzo na kilele cha maisha ya Kanisa; bali pia ni chanzo na kilele cha utume wake: “Kanisa la kweli la Kiekaristi ni Kanisa la kimisionari” (Sacramentum caritatis, 84) Ili tuweze kuzaa matunda lazima tubaki tumeungana na Yesu (rej. Yn 15:4-5). Muungano huu unapatikana kwa sala ya kila siku, hasa katika kuabudu Ekaristi, tunapokaa kimya mbele za Bwana, anayebaki nasi katika Sakramenti Takatifu. Kwa kusitawisha kwa upendo ushirika huu na Kristo, mfuasi mmisionari anaweza kuwa mtu wa maisha ya kiroho katika utendaji. Mioyo yetu na itamani daima ushirika wa Yesu, ikirudia ombi la bidii la wafuasi wawili wa Emau, hasa katika saa za jioni: “Kaa nasi, Bwana” (Taz. Lk. 24:29).

Ushuhuda wa upendo ni kikolezo cha uinjilishaji mpya: Ushuhuda
Ushuhuda wa upendo ni kikolezo cha uinjilishaji mpya: Ushuhuda

3. Miguu yetu inayotembea, kwa furaha ya kuwaambia wengine juu ya Kristo Mfufuka. Ujana wa milele wa Kanisa ambalo daima linasonga mbele. Baada ya macho yao kufunguliwa na kumtambua Yesu “katika kuumega mkate”, wafuasi “waliondoka bila kukawia na kurudi Yerusalemu” (taz. Lk 24:33). Kuondoka huku kwa haraka, kushiriki na wengine furaha ya kukutana na Bwana, kunaonesha kwamba, "furaha ya injili hujaza moyo na maisha yote ya wale wanaokutana na Yesu. Wale wanaojiruhusu kuokolewa naye wanawekwa huru kutoka katika dhambi, huzuni, utupu wa ndani na kutengwa. Pamoja na Yesu Kristo, furaha daima huzaliwa na kuzaliwa upya" (Evangelii gaudium, 1). Mtu hawezi kweli kukutana na Yesu mfufuka bila kuwaka moto kwa shauku ya kumwambia kila mtu habari zake. Hivyo, nyenzo ya msingi na kuu ya utume ni wale watu ambao wamemjua Kristo Mfufuka katika Maandiko na katika Ekaristi, ambao wanabeba moto wake mioyoni mwao na mwanga wake katika macho yao. Wanaweza kushuhudia maisha ambayo hayafi kamwe, hata katika hali ngumu sana na wakati wa giza kuu. Taswira ya "miguu inayotembea" inatukumbusha tena juu ya uhalali wa kudumu wa “missio ad gentes,” utume uliokabidhiwa kwa Kanisa na Bwana mfufuka ili kuinjilisha kila watu binafsi na watu wote, hata miisho ya dunia. Leo kuliko wakati mwingine wowote, familia yetu ya kibinadamu, iliyojeruhiwa na hali nyingi za ukosefu wa haki, migawanyiko mingi na vita, inahitaji Habari Njema ya amani na wokovu katika Kristo. Natumia fursa hii kusisitiza kwamba, "kila mtu ana haki ya kupokea Injili. Wakristo wana wajibu wa kuitangaza bila kumbagua mtu yeyote, si kama mtu anayeweka wajibu mpya, lakini kama mmoja anayeshirikisha furaha, anaashiria upeo mzuri, anatoa karamu inayotamaniwa" (Evangelii gaudium, 14). Wongofu wa kimisionari unabaki kuwa ndilo lengo kuu ambalo ni lazima tujiwekee kwa ajili yetu kama watu binafsi na kama jumuiya, kwa sababu "mawasiliano ya kimisionari ni kielelezo kwa shughuli zote za kanisa" (aya.15).

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Kama vile Mtume Paulo anavyothibitisha, upendo wa Kristo unatufunga na kutusukuma (taz. 2Kor 5:14). Upendo huu ni wa pande mbili: upendo wa Kristo kwetu, ambao huita, huchochea na kuamsha upendo wetu kwake. Upendo unaolijenga Kanisa, katika kuanza upya daima, daima hai. kuweka upya daima kuwa changa. Kwa maana viungo vyake vyote vimekabidhiwa utume wa kutangaza Injili ya Kristo, kwa kusadiki kwamba “alikufa kwa ajili ya wote, ili wanaoishi wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa kwa ajili yao na kufufuliwa" (aya.15). Sisi sote tunaweza kuchangia harakati hii ya kimisionari: kwa njia ya sala na shughuli zetu, kwa majitoleo ya vitu halisi na majitoleo ya mateso yetu, na kwa ushuhuda wetu binafsi. Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ni nyenzo zilizopewa kipaumbele katika kukuza ushirikiano huu wa kimisionari kwa ngazi zote mbili za kiroho na kimwili. Kwa sababu hii, mchango unaotolewa siku ya Dominika ya Misioni ni kwa ajili ya Shirika la Kipapa la Uenezaji wa Imani. Umuhimu wa kazi ya umisionari ya Kanisa kwa kawaida unahitaji ushirikiano wa karibu zaidi wa kimisionari kwa upande wa washiriki wote na katika kila ngazi. Hili ndilo lengo muhimu la safari ya kisinodi ambayo kanisa limeifanya, likiongozwa na maneno muhimu: Umoja, Ushiriki na Utume. Safari hii kwa hakika si kugeuka kwa kanisa ndani yake lenyewe; wala si kura ya maoni kuhusu kile tunachopaswa kuamini na kutenda, wala si suala la mapendeleo ya kibinadamu. Badala yake, ni mchakato wa kushika njia na, kama wafuasi wa Emau, kwa kumsikiliza Bwana Mfufuka. Kwa maana yeye huja daima kati yetu ili kueleza maana ya Maandiko na kuumega mkate kwa ajili yetu, ili tuweze, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kutekeleza utume wake duniani.

wongofu wa kimisionari ni muhimu katika uinjilishaji mpya
wongofu wa kimisionari ni muhimu katika uinjilishaji mpya

Kama vile wanafunzi wawili wa Emau walivyowaambia wengine mambo yaliyokuwa yametukia njiani (rej. Lk 24:35), vivyo hivyo utangazaji wetu utakuwa ni usimuliaji wa furaha juu ya Kristo Bwana, maisha yake, mateso yake, kifo na ufufuko wake, na maajabu ambayo upendo wake umetimiza katika maisha yetu. Hivyo, tuanze safari mara nyingine tena, tukiangazwa na kukutana kwetu na Bwana Mfufuka na kuchochewa na Roho wake. Hebu tuanze safari tena kwa mioyo inayowaka, macho yetu yakiwa wazi na miguu yetu katika mwendo. Na tuanze safari ili kuifanya mioyo mingine iwake kwe Neno la Mungu, ili kuifungua mioyo ya wengine kwa Kristo katika Ekaristi, na kumualika kila mmoja kutembea pamoja katika njia ya amani na wokovu ambao Mungu, katika Kristo, amewakirimia binadamu wote. Bikira Maria wa Mwongoza Njia, Mama wa Wafuasi Wamisionari wa Kristo na Malkia wa Misioni, utuombee!

Roma, Mtakatifu Yohane wa Laterano, 6 Januari 2023, Sherehe ya Tokeo la Bwana.

FRANCISKO.

Papa Ujumbe Siku ya Kimisionari
19 October 2023, 16:05