Tafuta

Vatican bado ina amini katika amani na kwamba, siku zote Vatican iko tayari kusaidia katika mchakato wa upatanishi, ili suluhu ya amani iweze kupatikana. Vatican bado ina amini katika amani na kwamba, siku zote Vatican iko tayari kusaidia katika mchakato wa upatanishi, ili suluhu ya amani iweze kupatikana.  (ANSA)

Siku ya Kuombea Amani Huko Mashariki ya Kati Oktoba 2023

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Vatican bado ina amini katika amani na kwamba, siku zote Vatican iko tayari kusaidia katika mchakato wa upatanishi, ili suluhu ya amani iweze kupatikana. Anasema, leo hii Jumuiya ya Kimataifa imesambaratishwa na migogoro mikali kama ile inayoyojitokeza sasa ya vita kati ya Israeli na Palestina, lakini kuna haja ya kuamini katika amani. Mwaliko ni kuhisi mateso na mahangaiko ya waathirika wa vita na migogoro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 15 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesikitishwa sana na hali ilivyo huko Ukanda wa Gaza na kwamba, waathirika wakuu ni watoto, wazee na wanawake. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa mwaliko kwa pande zote mbili kuwaachilia mara moja mateka wa vita na kwamba, watoto, wagonjwa na wazee kamwe wasiwe ni chambo cha vita. Kumbe, kuna haja ya kuheshimi sheria za Jumuiya ya Kimataifa, hususan Ukanda wa Gaza ambako kuna haja ya kutoa mwanya ili shughuli za uokoaji zifanyike na msaada uendelee kutolewa kwa waathirika. Baba Mtakatifu ameombea usalama na amani sehemu mbalimbali za dunia, bila kusahau Ukraine na kwamba, kusiwepo tena na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.
Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, sala ni nguvu inayosimikwa katika: Upole, unyenyekevu na ni takatifu ya kupinga nguvu ya kishetani ya chuki, ugaidi na vita. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na Kanisa katika Nchi Takatifu kusali na kufunga ili kuombea amani Ukanda wa Gaza, Jumanne, tarehe 17 Oktoba 2023. Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni alimpigia simu Sr. Nabila Salehe wa Shirika la Masista wa Rozari Takatifu mjini Yerusalemu kutaka kufahamu hali yao. Sr. Nabila Salehe amesema, kwa sasa Parokia yao inatoa hifadhi kwa watu 500 kati yao kuna wagonjwa, familia pamoja na walemavu. Baba Mtakatifu amewatia moyo kuendelea na huduma na kwamba, anawakumbuka katika sadaka na sala zake. Masista Parokiani hapo wanatolea sala na sadaka yao kwa ajili ya kuombea amani, mahitaji msingi ya Kanisa pamoja na Sinodi inayoendelea mjini Vatican. Wanaparokia hao wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujisadaka kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.
Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.

Kwa upande wake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, TV2000 anasema kwamba, Vatican bado ina amini katika amani na kwamba, siku zote Vatican iko tayari kusaidia katika mchakato wa upatanishi, ili suluhu ya amani iweze kupatikana. Anasema, leo hii Jumuiya ya Kimataifa imesambaratishwa na kinzani pamoja na migogoro mikali kama ile inayoyojitokeza sasa ya vita kati ya Israeli na Palestina, lakini kuna haja ya kuamini katika amani. Hayati Kardinali Carlo Maria Martini katika makala aliyoiandika kunako mwaka 2003 baada ya kurejea kutoka Nchi Takatifu, nyakati za mwisho wa maisha yake hapa duniani, alikaza kusema, ili kuwa na amani mwanadamu hana budi kuondokana na “sanamu na vinyago” vilivyomo ndani ya nyoyo zao na zaidi ya yote, ni kujitahidi kuhisi mateso ya wengine katika miili yao wenyewe. Binadamu akifikia hatua hii, ataweza kutafuta na kudumisha amani. Mateso, mahangaiko na machungu ya wengine ni njia muafaka ya ujenzi wa amani duniani.

Mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kuombea amani Mashariki ya Kati
Mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kuombea amani Mashariki ya Kati

Naye Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kanisa la Kilatini la Yerusalemu anasema, Jumanne, tarehe 17 Oktoba 2023 anaungana na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati na kwamba, vitendo vya Wanamgambo wa Hamas vya kuteka nyara watu wasiokuwa na hatia havikubaliki na wapenda amani. Anafarijika sana na mshikamano wa waamini kwa njia ya sala kwa ajili kusali na kuombea amani huko Mashariki ya Kati. Anahofia sana kwamba, vita kati ya Israeli na Palestina inaweza kusambaa ukanda wote wa Gaza. Watu waliokimbilia kwenye nyumba za Ibada huko Ukanda wa Gaza wako salama. Kuna haja ya kuongeza jitihada ili kuhakikisha kwamba, mateka wa vita wanarejea makwao. Mji wa Yerusalemu kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya kidini, kiekumene, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi.

Amani Mashariki ya Kati
17 October 2023, 14:45