Papa kwa vijana katika Kongamano la Uongozi:jengeni ndoto kubwa!
Na Angella Rwezaula, Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe washiriki wa Kongamano la Uongozi lilioandaliwa na Chuo cha Mtakatifu Carlo huko Milano Italia, ambayo ni shule ya Kikatoliki kwa siku mbili ya tarehe 13 na 14 Oktoba 2023. Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu anashukuru kwamba vijana wana ndoto kubwa na wanaweza kupata msaada kwa watu wazima. Kisha anawapa pendekezo kwa kusema: kutoa salamu zake na na heri kwao washiriki wote, ambazo zinaambatana na tafakari fupi. Katika wakati huu uliokumbwa na migogoro mikubwa ya kijamii na hali ya tabianchi, pamoja na walimu na waelimishaji wao wanashangaa jinsi ya kuchangia katika kubadilisha ulimwengu. Hii ni chanya sana. Kiukweli, ni muhimu kuwa na ndoto kubwa: hata Mungu anazo! Na ni muhimu kukutana na watu wazima ambao hawazimi ndoto zao, lakini wanawasaidia kutafsiri na kuzifanya kuwa kweli. Siku zote lazima wazilinganishe ndoto zao na zile za Mungu!
Ikiwa basi wanataka kupata mabadiliko kama wahusika wakuu, Papa Francisko anawaalika wagundue uzuri usiyoisha wa nafsi ya Yesu: Yeye anafanya mambo yote kuwa mapya; Anafichua mamlaka tofauti na yale yaliyooneshwa na wenye nguvu wa jana na leo. Mambo yake ni njia ya kubadilisha hali ambayo hailengi lakini inainua, hailazimishi lakini ni huru. Yesu hubadilisha mwanadamu kutoka ndani, ikiwa ni pamoja na kila mmoja wao, ili kwamba waweze kueleza nguvu zao bora na talanta walizo nazo kuzitumia. Baba Mtakatifu amewaomba wamfuate kwa uaminifu kamili, wakifikiria kukua kwao sio kujiinua mwenyewe juu ya wengine, lakini kama kujishusha katika huduma ya wengine. Mkubwa zaidi ni yule anayejua kuinama juu ya wale walioanguka na kuchukua baadhi ya mizigo yao, kwa huruma ambayo ni nguvu ya kweli.
Baba Mtakatifu Francisko akitazama juu ya lengo la Kongamano lao amebainisha wanavyotaka kuwa wahusika wakuu kwa kutumia vyema akili tano ambazo Mungu amewapatia. Hii ni busara, kwa sababu ukweli ni bora kuliko mawazo na inahitaji uwazi, tahadhari, huruma, inahitaji "unyeti" muhimu. Kutokana na hilo, Papa ameomba aruhusiwe kuwakumbusha kwamba unyeti huu pia unajumuisha kile ambacho walimu wa hekima huita "hisia za kiroho". Hapinga wale wa kisaikolojia, lakini huwapa nuru na kuwaimarisha. Papa amewaleza vijana hao kwa sababu taasisi yao ya Elimu ni ya Kikatoliki na “Katoliki” ina maana kamili kwamba ina maono yaliyo wazi na muhimu ya mwanadamu, katika nyanja zake zote, yale ambayo Maandiko Matakatifu yanatufunulia na ambayo Yesu Kristo alitambua kwa ukamilifu.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amewaomba watumie vyema fursa hizi ambazo shule inawapatia! Hazipaswi kuchukuliwa kirahisi. Kwa kuwakumbusha zaidi amesema, vijana wenzao walio wengi duniani hasa wasichana, hawana hata fursa ya kusoma. Kwa hiyo wafanyie kazi pia, na wapambanie haki zao pia. Kwa sababu imani ni cheche la moto linalozidi kuwa hai kadiri wanavyoshirikishwa na kupitishwa, ili kila mtu aweze kumjua, kumpenda na kumkiri Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa uzima na historia. Papa amehitimisha kwa kuwashukuru kujitolea kwao.Aliwabariki kwa moyo wote, walimu na waelimishaji wao na familia zao. Mtakatifu Karoli na Bikira Maria awasaidie kuhisi furaha ya Injili na kujaribu kumwilisha katika maisha yao. Tafadhali wasisahau kumuombea.